Mahubiri ya Kipindi cha Majilio kwa Mwaka 2020: Fumbo la Umwilisho: Kielelezo cha Upendo na Unyenyekevu wa Mungu unaokomboa! Mahubiri ya Kipindi cha Majilio kwa Mwaka 2020: Fumbo la Umwilisho: Kielelezo cha Upendo na Unyenyekevu wa Mungu unaokomboa! 

Mahubiri ya Kipindi Cha Majilio 2020: Fumbo la Umwilisho!

Sherehe ya Noeli ni kielelezo cha unyenyekevu wa Mungu, ni Sakramenti ya ufukara wa Kristo Yesu anayeteseka kati ya waja wake, lakini zaidi kati ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mama Kanisa anawaalika waja wake kumwendea Kristo Yesu ili aweze kufanya makazi yake kati yao. Unyenyekevu wa Mungu unajionesha katika Umwilisho na Pasaka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa katika Mahubiri ya Kipindi cha Majilio kwa Mwaka 2020 anapenda kujielekeza zaidi katika tafakari juu ya Fumbo la Kifo katika maisha ya binadamu. Tafakari hii inaongozwa na kauli mbiu “Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu, tujipatie moyo wa hekima”, Zaburi ya 90:12. Haya ni maneno yanayowatia waamini matumaini badala ya kujisikia kuwa wanyonge wanapoyaona maisha yao yana yoyoma na kutoweka mara kama ndoto ya mchana. Kifo kinayaanika maisha ya binadamu na kumwondolea kiburi na hivyo kuwahimiza watu kujenga na kudumisha upendo, kutafuta na kuambata mambo msingi katika maisha, ili sadaka na majitoleo yao yaweze kuwapatia amani na utulivu wa ndani wanapokabiliana na Fumbo la Kifo! Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu ameliangazia Fumbo la Kifo cha binadamu, kwa njia ya ushuhuda wa maisha na matendo yake, hasa pale, watu wanapoondokewa na wapendwa wao!

Maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 yamekuwa ni changamoto inayogusa na kutikisa imani ya watu wengi duniani. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kuendelea kutafakari kuhusu gonjwa hili mintarafu changamoto za kiimani, kichungaji, maisha ya kiroho na kijamii. Mwanadamu amegundua udhaifu wa maisha yake, kiasi cha kujikatia tamaa. Takatika mahubiri yake sehemu ya kwanza, Kardinali Raniero Cantalamessa aligusia kuhusu maana ya Fumbo la Kifo katika maisha ya mwanadamu. Awamu ya pili akajipambanua kwa kukazia umuhimu wa waamini kushikamana kwani wote ni wanandani wa safari kuelekea maisha na uzima wa milele, chemchemi ya matumaini na ukweli unaofumbatwa katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka wafu!

Kardinali Raniero Cantalamessa, katika Mahubiri ya Awamu ya Tatu, Kipindi cha Majilio, Ijumaa tarehe 18 Desemba 2020 ambayo yamehudhuriwa pia na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na waandamizi wake, ameongozwa na kauli mbiu “Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi”. Huu ni mwangwi wa maneno ya Yohane Mbatizaji, changamoto na mwaliko wa kuendelea kuimarisha imani, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu anawapenda na kuwajali waja wake kuliko mtu mwingine yeyote yule! Sherehe ya Noeli ni kielelezo cha unyenyekevu wa Mungu, ni Sakramenti ya ufukara wa Kristo Yesu anayeteseka kati ya waja wake, lakini zaidi kati ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mama Kanisa anawaalika waja wake kumwendea Kristo Yesu ili aweze kufanya makazi yake kati yao.

Kardinali Cantalamessa amewarejesha wasikilizaji wake kwenye Injili ya Marko sura ya 4:38, wanafunzi wa Yesu walipomwamsha na kumwambia “Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia? Wanafunzi walidhani kwamba, Kristo Yesu alikuwa hawajali hata kidogo na kusahau kwamba, Yesu ni Mwana wa Mungu kamwe hawezi kuangamia. Hii ni changamoto kwa waamini kutambua kwamba, hata katika mawimbi mazito ya maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kamwe hawawezi kuzama kwani wanasongwa pia na mawimbi ya huruma ya Mungu. Neno wa Mungu aliyetwaa mwili na kukaa kati ya waja wake hawezi kuangamia hata kidogo. Ndiyo maana Mzaburi anasema Mungu yu pamoja nasi. Mwenyezi Mungu ni kimbilio na nguvu, msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso, kwa hiyo hawataogopa ijapobadilika nchi, ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yanapovuma na kuumuka, ijapopepesuka milima kwa kiburi chake. Rej. Zab. 46:2-4. Huyu ni Imanueli, yaani “Mungu pamoja nasi”. Hii ndiyo kashfa ya Fumbo la Umwilisho, kwa baadhi ya wasomi kushindwa kukiri na kutambua unyenyekevu wa Mungu. Yesu mwenyewe anasema ni njia, ukweli na uzima, hakuna mtu anayeweza kwenda kwa Baba yake ila kwa njia yake!

Fadhila ya unyenyekevu ni msingi wa tafakari kuhusu Fumbo la Umwilisho. “Hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba”. Flp. 2:7-8. Mwenyezi Mungu ni upendo na kielelezo cha hali ya juu kabisa cha unyenyekevu, mwaliko ni kumjifunza Kristo Yesu kwani Yeye ni mpole na mnyenyekevu wa moyo! Kumbe, Sherehe ya Noeli ni kielelezo cha unyenyekevu wa Mungu, mwaliko kwa waamini kujishusha na kumwabudu.

Yohane Mbatizaji alisema: “Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi”. Kiini cha Fumbo la Umwilisho ni uwepo endelevu wa Mungu kati ya waja wake, kiasi kwamba, katika Agano Jipya, amekuwa ni dira ya Unabii wa Kikristo. Yesu anatambuliwa kama: Nabii wa Mungu aliye hai, aliyetangazwa kwa vinywa vya Manabii. Yohane Mbatizaji akamtambulisha kwa watu kama Mwanakondoo wa Mungu kwa kuonesha uwepo wake hadi utimilifu wa nyakati. Ni Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, chanzo cha uinjilishaji. Katika mambo yote alikuwa sawa na binadamu, lakini hakutenda dhambi. Leo hii, Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa limekuwa ni sehemu ya kashfa kutokana na kuandamwa na dhambi za watoto wake. Ni wajibu na dhamana ya waamini kumtambulisha Kristo Yesu katika ufukara wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa, na katika udhaifu na karama za watoto wa Kanisa.

Kanisa linapaswa kuwa ni Sakramenti ya Ufukara! Wakristo wanapaswa kuwa ni Sakramenti ya Ekaristi Takatifu inayonafsishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walilitaka Kanisa liwe ni kielelezo makini cha mshikamano na maskini pamoja na mashuhuda wa imani wanaoendelea kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Kimsingi anasema Kardinali Cantalamessa, hili ni Kanisa kwa ajili ya binadamu wote. Hii ni dhamana inayotekelezwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na waandamizi wake, wanaopaswa kuwa ni “Mababa wa Maskini.” Kwa hakika, Baba Mtakatifu Francisko kamwe hajawasahau maskini. Maandiko Matakatifu yanasema kwamba, Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni! Hata leo hii, maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” hawana nafasi”. Kuwajali na kuwasaidia maskini ni njia muafaka ya kuiga unyenyekevu wa Mungu. Upendo usaidie kuwanyanyua kwa vitendo wale wote wanaoteseka kwa umaskini.

Kristo Yesu anasema: “Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake” Yn. 14:23. Kwa hakika, Kristo Yesu yuko ulimwenguni na katika Kanisa lake, lakini yuko pia katika “sakafu” ya moyo wa kila mwamini” ili kuleta mwanga angavu katika maisha. Katika kipindi hiki ambacho waamini wengi wanakabiliwa na changamoto ya maambukizi makubwa ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kiasi cha kushindwa kwenda kuhudhuria Ibada Kanisani, bado wanayo nafasi ya kumwabudu Mwenyezi Mungu katika roho na kweli na hivyo kuendelea kujadiliana na Kristo Yesu, ambaye anaendelea kuwa ni mwandani wa maisha yao hata kama wamefungiwa majumbani au vyumbani mwao!

Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni muhimu kwa maisha ya Mkristo na Jumuiya ya waamini, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, kila mwamini anajitahidi kukutana na Kristo Yesu katika undani wa moyo wake, vinginevyo ni bure kabisa! Mababa wa Kanisa wanawahimiza waamini kuhakikisha kwamba, Kristo Yesu anazaliwa tena katika roho na nyoyo zao. Neno wa Mungu anatamani tena kurudia Fumbo la Umwilisho katika kila moyo na roho ya mwanadamu. Huu ni ukweli wa kiekumene! Maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho iwe ni nafasi nyingine tena ya kumwalika Kristo Yesu, Mfalme wa Mataifa, Kiongozi anayetarajiwa na wengi, Jiwe kuu la pembeni linalowaunganisha na kuwashikamanisha watu wote, aje kuwaokoa watu wote; watu ambao amewaumba kutoka kwenye udongo. Waamini wamwalike Yesu ili aweze kuwaokoa kutoka katika janga la Virusi vya Corona, COVID-19.

Mahubiri Majilio
18 December 2020, 15:23