Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Frateri Tutti: Yaani "Wote Ni Ndugu": Kuhusu Udugu na Ufariki wa Kijamii utazinduliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2020 wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Mt. Francisko wa Assisi. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Frateri Tutti: Yaani "Wote Ni Ndugu": Kuhusu Udugu na Ufariki wa Kijamii utazinduliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2020 wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Mt. Francisko wa Assisi.  Tahariri

Waraka Mpya: "Frateri Tutti": Yaani: Wote Ni Ndugu: Urafiki Wa Kijamii

Dr. Andrea Tornielli anasema, Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Fratelli Tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”, utawekwa mkwaju tarehe 3 Oktoba na kuzinduliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2020, saa 6:00 mchana kwa saa za Ulaya wakati wa Maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi. Ni Waraka wa kitume kwa watu wote bila ubaguzi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 3 Oktoba 2020 majira ya jioni baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa lililoko chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Francisko wa Assisi, mjini Assisi, nchini Italia, atatia mkwaju kwenye Waraka wake wa Kitume ambao umepewa kichwa cha habari "Fratelli Tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”. Waraka huu utatolewa hadharani, tarehe 4 Oktoba 2020 katika maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi aliyekazia: amani, utunzaji bora wa mazingira pamoja na huduma makini kwa maskini, aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni somo wake katika maisha na utume kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. “Fratelli Tutti” yaani “Wote ni Ndugu” kama Waraka huu wa kitume utakavyojulikana ni utajiri wa maneno kutoka kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi, anayewaalika ndugu zake watawa wote, kuchukuliana kama ndugu; na kwa mchungaji mwema, ili kuweza kuwaokoa kondoo wake anavumilia mateso ya Msalaba.

Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika Tahariri yake kuhusu Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Fratelli Tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”, anasema, wakati ambapo watu wa Mungu wanaendelea kusubiri ili kutambua maudhui yaliyomo kwenye waraka huu wa kitume anasikitika kusema kwamba, kuna watu ambao wameanza kuonesha wasi wasi na kutaka kupotosha ukweli wa mambo kwa kudhani kwamba, kwa vile anazungumzia “Fratelli Tutti” anataka kuwabagua wanawake. Lakini, ikumbukwe kwamba, Waraka huu ni kwa ajili ya waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Ni waraka unaotoa fursa kwa watu wa Mataifa kutafakari kuhusu udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii unaowafunga na kuwaambata watu wote bila ubaguzi. Ulimwengu mamboleo unakabiliwa na changamoto kubwa ya vita, umaskini, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, athari za mabadiliko ya tabianchi, myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa pamoja na janga la Virusi vya Corona, COVID-19!

Hapa kuna umuhimu wa kutambuana kama ndugu wamoja na kuwaona wale wote wanaoteseka kuwa ni ufunuo wa Sura ya Kristo Yesu anayeteseka kati yao. Lengo ni kujizatiti kikamilifu ili kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Huu ni wakati wa kujenga na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa kutambua kwamba, watu wanategemeana na kukamilishana; wale wa Kaskazini wanawahitaji watu wa Kusini; kama ilivyo pia hata kwa matajiri na maskini. Itakumbukwa kwamba, tarehe 27 Machi 2020, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko alisali kwa ajili ya wokovu wa walimwengu wote na hapo watu wote wakagundua kwamba wote ni ndugu wamoja.

Kiini cha ujumbe kutoka katika Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko “Fratelli Tutti” ni baraka za utambulisho wa pamoja unaowafanya watu wote walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu kujisikia kuwa ni ndugu wamoja. Udugu na urafiki wa kijamii ni tema inayowaunganisha watu wote, wanaume kwa wanawake, si tu katika masuala ya udugu wa damu, bali kwa kutakiana mema ya nchi na kusaidiana wakati wa raha na uchungu. Tabia ya kujaliana inavuka mipaka ya utambulisho na mahali anapotoka mtu. Kumbe, “Fratelli Tutti” ni ujumbe unaowakumbatia na kuwaunganisha watu wote ili waweze kujisikia kuwa ni ndugu wamoja!

Frateri Tutti
17 September 2020, 15:21