Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha lasema, kuelekea Uchumi wa Francisko: Vipaumbele: Soko linalozingatia. Soko, Utu, Heshima na Ustawi wa Watu wa Mungu. Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha lasema, kuelekea Uchumi wa Francisko: Vipaumbele: Soko linalozingatia. Soko, Utu, Heshima na Ustawi wa Watu wa Mungu. 

Kuelekea Uchumi wa Francisko: Soko, Ustawi Na Mafao ya Wengi

Kuelekea Uchumi wa Francisko: Mafundisho Jamii ya Kanisa yanaongozwa na kanuni ya: Manufaa kwa wote, (mafao ya wengi) auni na mshikamano wa udugu wa kibinadamu; muhtasari wa Amri kuu ya upendo kwa Mungu na jirani, jibu makini katika changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo. Ni kanuni zinazokita mizizi yake katika heshima, umoja na usawa wa watu wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, “Economy of Francesco” yaani “Uchumi wa Francisko” ni tukio ambalo linatarajiwa kuwakusanya wachumi na wajasiriamali wachumi vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kuanzia tarehe 19-21 Novemba, 2020 huko Assisi, nchini Italia. Hii ni sehemu ya mbinu mkakati wa utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, unaotekelezwa kwa namna ya pekee, na Baba Mtakatifu Francisko. Dr. Gabriella Gambino, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, katika ujumbe wake kwa njia ya video aliowatumia waandaaji wa tukio hili hivi karibuni amekazia umuhimu wa sera na mikakati ua uchumi kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanaongozwa na kanuni ya: Manufaa kwa wote, (mafao ya wengi) auni na mshikamano wa udugu wa kibinadamu; muhtasari wa Amri kuu ya upendo kwa Mungu na jirani, jibu makini katika changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo.

Ni kanuni zinazokita mizizi yake katika heshima, umoja na usawa wa watu wote. Jamii ambayo inataka na ina nia ya dhati kabisa ya kubaki katika kumhudumia binadamu katika medani mbali mbali za maisha, hiyo ni jamii inayojali na yenye mafao ya wengi. Haya ni mafao ya watu wote na ya mtu kamili kama ndio lengo msingi. Binadamu hawezi kufikia ukamilifu katika yeye mwenyewe, pamoja na ukweli kwamba, anaishi na wengine na kwa ajili ya wengine. Dr. Gabriella Gambino anasema, mafao ya wengi hayawezi kugeuzwa na kuwa ni kwa ajili ya ustawi wa kiuchumi na kijamii peke yake. Kuna uhusiano na mafungamano ya dhati kabisa kati ya: Uchumi, mafao ya wengi na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Neno “Economy” kwa lugha ya Kigiriki ni “Oikia-nomos” maana yake “sanaa ya kuratibu maisha ya familia, maisha ya nyumbani.” Familia inayo nafasi muhimu sana katika mchakato wa ukuaji wa uchumi na maendeleo fungamani ya binadamu, mintarafu soko, umoja na mshikamano kati ya kizazi kimoja na kingine, kwa njia ya uzalishaji mali na huduma, nguvu inayoongoza na kuratibu mfumo mzima wa uchumi.

Janga kubwa la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 imedhihirisha wazi kwamba, familia ndiyo iliyobeba mzigo wote wa athari ambazo zimesababishwa na gonjwa hili: kiutu, kijamii, kiuchumi, kitamaduni na kiafya. Familia imekuwa ni ngome salama kwa watu waliokuwa wanateseka kwa taharuki ya gonjwa hili, ambalo limeacha maafa makubwa kwa watu sehemu mbali mbali za dunia. Kumbe, sera na mikakati ya uchumi isiwe ni kwa ajili ya starehe za watu wachache tu ndani ya jamii, bali sera na mikakati hii ijielekeze zaidi katika mchakato wa ujenzi wa uchumi fungamani, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali za maisha. Dr. Gabriella Gambino anaendelea kufafanua kwamba, utajiri na furaha ya kweli ni mambo mawili tofauti kabisa. Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, utajiri, amana na rasilimali za dunia, zinatumika kwa ajili ya huduma kwa mtu mzima, ili binadamu aweze kufikia utimilifu wa maisha yake. Kamwe familia isigeuzwe kuwa ni mzigo mzito usioweza kubebeka hata kidogo, kiasi cha kuwakatisha tamaa vijana wa kizazi kipya wanaotamani kuanzisha na hatimaye kujenga msingi bora wa maisha ya ndoa na familia.

Tunu msingi za familia ni nguzo katika kukuza na kuimarisha: umoja, mshikamano na mapendo; kwa kujitoa bila kujisabakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mambo yote haya ni muhimu sana katika mchakato wa kudumisha uchumi fungamani. Dr. Gabriella Gambino anakaza kusema, hii ni changamoto kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia kuondokana na saratani ya uchoyo na ubinafsi; kwa kutambua na kuenzi tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu na kwamba, familia ni msingi wa mafao ya wengi. Ikumbukwe kwamba, kazi ni sehemu muhimu sana ya utilimifu wa utu na heshima ya binadamu. Fursa za ajira ziwajengee wanafamilia uwezo wa kutekeleza dhamana na nyajibu zao za kila siku. Kumbe, sera na mikakati ya uchumi fungamani zilenge zaidi kutekeleza mahitaji msingi ya binadamu, kwa kuimarisha mafungamano ya kijamii, yanayotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, utoe upendeleo wa pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kudumisha mafungamano ya kijamii.

Dr. Gabriella Gambino, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, anahitimisha ujumbe wake kwa waandaaji wa tukio la uchumi wa Francisko huko Assisi kuanzia tarehe 19-21 Novemba 2020 kwa kukazia umuhimu wa: soko kama mahali pa kuwakutanisha watu katika imani na ukweli, huku wakizingatia kanuni ya umoja na mshikamano. Soko halina budi kuratibiwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kamwe haliwezi kuongozwa na mikono ya “watu wasiojulikana” na waswahili wangechombeza kwa kusema, soko haliwezi kuongozwa “kwa roho za wajumbe”, bali kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Tukio la Uchumi wa Francisko ni nafasi kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kukutana na kuzungumza na vijana wanaojifunza uchumi unaotekelezwa katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu! Anataka kuzama zaidi katika uchumi unaohuisha na wala si ule unaowatumbukiza watu katika kifo. Uchumi fungamani unaojikita katika tunu msingi za utu na heshima ya binadamu; uchumi unaojikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Baba Mtakatifu Francisko anataka kuzama zaidi katika uchumi unaohuisha na wala si ule unaowatumbukiza watu katika kifo. Uchumi fungamani unaojikita katika tunu msingi za utu na heshima ya binadamu; uchumi unaojikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Francisko katika barua ya mwaliko kwa wachumi na wajasiriamali vijana, anawataka kujikita katika mchakato wa kupyaisha mchakato wa uchumi duniani, kwa kujikita katika udugu kama alivyokazia Mtakatifu Yohane Paulo II, kwa kuuchagua mji wa Assisi kuwa ni kitovu cha amani na kwa sasa yeye anataka mji wa Assisi uwe ni jukwaa la mchakato wa mfumo mpya wa uchumi mpya duniani. Mji wa Assisi ni mahali ambapo, Mtakatifu Francisko wa Assisi alipouvua utu wake wa kale na kumchagua Mwenyezi Mungu kuwa ni dira na mwongozo wake wa maisha; na hivyo kuwa maskini kati ya maskini na ndugu ya wote. Baba Mtakatifu anakaza kusema, maamuzi haya machungu, yakaibua dira na mwelekeo mpya kuhusu mwono wa kiuchumi unaotoa matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu katika ujumla wake.

Mwelekeo huu ni muhimu sana katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kama anavyokazia Mtakatifu Francisko wa Assisi katika “Utenzi wake wa ndugu Jua”. Mazingira na maisha ya binadamu vinategemeana na kukamilishana, ili haki iweze kupatikana kwa ajili ya maskini pamoja na kupata majibu muafaka wa matatizo ya muundo wa uchumi kimataifa. Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kuwa na mfumo ya uchumi unaolinda na kutunza mazingira; uchumi unaoenzi  zawadi ya maisha; kwa kudumisha tunu msingi za maisha ya familia; usawa wa kijamii, utu, heshima na haki msingi za wafanyakazi, pamoja na kuwahakikishia vijana haki zao msingi ili kuwa na maisha bora zaidi kwa siku za mbeleni. Kwa bahati mbaya, ni watu wachache sana ambao wamesikiliza na kutambua matatizo ya uchumi mamboleo kiasi hata cha kuthubutu kuweka mifumo mipya ya uchumi ambayo ni matunda ya utamaduni wa umoja unaojikita katika udugu na usawa. Mtakatifu Francisko wa Assisi ni mfano bora wa kuigwa katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote sanjari na ekolojia fungamani.

Ni Mtakatifu Francisko aliyethubutu kufanya ukarabati mkubwa wa “Nyumba ya Mungu” iliyokuwa inaporomoka. Huu ni wajibu wa watu wote yaani: Kanisa jamii na kwa kila mtu binafsi. Utunzaji bora wa mazingira unahitaji uchumi makini na maendeleo fungamani yanayoweza kuponya madonda, na hivyo kuwahakikishia watu matumaini kwa siku za mbeleni. Ili kuweza kutekeleza kwa dhati changamoto hii, kuna haja kwa kila mtu kuanza kufikiri na kujikita katika kanuni maadili, Amri za Mungu na mafao ya wengi. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwaalika vijana, wanaotamani maisha bora na yenye furaha, vijana ambao ni alama ya kinabii, ili waweze kuonesha dira ya uchumi ambao uko makini kwa binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, vijana wa kizazi kipya, kutoka katika undani wa maisha yao, wamesikiliza kilio cha Mama Dunia na watoto wake maskini, wanaohitaji msaada, unao wawajibisha na kamwe wasikimbie dhamana hii, bali wasimame kidete kujenga na kudumisha utamaduni wa ujasiri, tayari kuthubutu kuanza ujenzi wa jamii mpya.

Kristo Mfufuka ndiye nguzo yao na kwamba, vijana wanapaswa kuwa ni wadau wakuu katika mchakato wa mageuzi, ili kuwa na kesho iliyo bora zaidi. Vyuo vikuu, shughuli mbali mbali za biashara, makongamano na warsha ni mahali muafaka pa kujenga njia za uelewa mpya wa uchumi na maendeleo, ili kuweza kukabiliana na utamaduni wa kutupa, kwa kuwa ni sauti ya wale wasiokuwa na sauti na hatimaye, kuwa na mtindo mpya wa maisha, ili watu wote katika umoja wao, waweze kufurahia udugu wa kiulimwengu. Mkutano wa Uchumi wa Francisko huko Assisi una pania kuragibisha “Agano la pamoja” kama sehemu ya mchakato wa mabadiliko ulimwenguni kwa kuwakumbatia na kuwaambata watu wote bila ya kujali tofauti za imani wala utaifa wao, bali watu ambao wanaongozwa na dhana ya udugu, kwa kuwajali maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anawaalika vijana kujenga ndoto ya ubinadamu mpya ili kujibu matarajio ya watu kadiri ya mpango wa Mungu.

Katika mchakato huu, Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyejitahidi kumwilisha Injili katika maisha yake, alisaidia kuleta mabadiliko katika masuala ya kijamii na kiuchumi. Anatoa mawazo na programu katika utekelezi wa mazingira, amani na maskini ndiyo maana alimchagua kuwa ni Msimamizi katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu akiwa ameshikamana na vijana, atawahamasisha magwiji wa sera na mipango ya uchumi duniani kuunda mwelekeo mpya wa uchumi na anatumaini kwamba, wataitikia mwaliko huu. Lakini, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, ana matumaini makubwa kwa vijana, wenye uwezo wa kuota ndoto, wanaojiandaa kwa msaada wa Mungu kujenga ulimwengu unaosimikwa katika haki na uzuri.

Uchumi wa Francisko

 

 

 

20 August 2020, 13:28