Caritas Internationalis kwa kushirikiana na Caritas Lebanon, inaendelea kuratibu misaada ya hali na mali kutokana na mlipuko mkubwa uliojitokeza tarehe 4 Agosti 2020 na kusababisha maafa makubwa. Caritas Internationalis kwa kushirikiana na Caritas Lebanon, inaendelea kuratibu misaada ya hali na mali kutokana na mlipuko mkubwa uliojitokeza tarehe 4 Agosti 2020 na kusababisha maafa makubwa. 

Mlipuko wa Beirut, Lebanon: Juhudi za Caritas Internationalis!

Mlipuko, Beirut: 4 Agosti 2020 umekwisha kusababisha watu zaidi ya 140 kupoteza maisha na wengine 5, 000 kujeruhiwa vibaya na watu 3, 000 hawana makazi maalum baada ya nyumba zao kuharibiwa vibaya na mlipuko huo. Serikali ya Lebanon, imetangaza hali ya hatari kwa muda wa majuma mawili, huku maofisa 16 wa mji wa Beirut, wakiwa wamezuiliwa kwa kifungo cha ndani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Taarifa kutoka Beirut nchini Lebanon zinabainisha kwamba, mlipuko uliotokea kwenye eneo la bandari ya Beirut, Jumanne, tarehe 4 Agosti 2020 umekwisha kusababisha watu zaidi ya 140 kupoteza maisha na wengine 5, 000 kujeruhiwa vibaya na watu 3, 000 hawana makazi maalum baada ya nyumba zao kuharibiwa vibaya na mlipuko huo. Serikali ya Lebanon, imetangaza hali ya hatari kwa muda wa majuma mawili, huku maofisa 16 wa mji wa Beirut, wakiwa wamezuiliwa kwa kifungo cha ndani, ili kusubiri uchunguzi wa tuhuma zinazowahusu kufuatia mlipuko huo ambao umesababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao. Rais Michel Aoun alisema kwamba mlipuko huo ulisababishwa na tani 2,750 za madini ya “Amonium Nitrate” iliokuwa imehifadhiwa katika ghala moja huko Beirut. Hasara iliyojitokeza hadi wakati huu inakadiriwa kufikia bilioni 5 za dola za Kimarekani.  

Taarifa zinaonesha kwamba, madini haya “Ammonium nitrate” kwa muda wa miaka sita, yaani tangu mwaka 2013 yamekuwa yakihifadhiwa ghalani hapo baada ya Meli ya Kampuni ya Rhosus iliyokuwa inapeperusha bendera ya Moldova kuelekea nchini Msumbiji kukamatwa ikiwa na mzigo huo hatari. Madini haya hutumika kutengenezea mbolea pamoja na mabomu. Afisa mwandamizi anayeshughulikia forodha, Bwana Badri Daher amesema kwamba, shirika lake lilitoa wito kwa kemikali hiyo kuondolewa, lakini jambo hilo halikufanyika na matokeo yake ni maafa makubwa ambayo yameugeuza mji wa Beirut kuwa kama mahame ya kale! Wananchi wanasema haya ndiyo matokeo ya watu kutowajibika barabara, uongozi dhaifu, ufisadi na rushwa. Wachunguzi wa masuala ya kijeshi wanabainisha kwamba, itachukua muda mrefu kwa Beirut kuweza kurejea tena katika hali yake ya asili.

Katika hali na mazingira kama haya, Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis kwa kushirikiana na Shirika la Misaada ya Kanisa Katoliki Nchini Lebanon, Caritas Lebanon, yameanza kampeni ya kuratibu misaada kutoka kwa Wasamaria wema sehemu mbali mbali za dunia, ili iweze kuwafikia walengwa. Hospitali nyingi zimefurika na zinahitaji msaada wa dharura wa dawa na vifaa tiba. Aloysius John, Katibu mkuu wa Caritas Internationalis anakiri kwamba, janga la Virusi vya Corona, COVID-19 limeipekenya na “kuipapasa” Caritas Internaionalis, kiasi cha kuifanya kusitisha baadhi ya miradi, sera na mikakati ya shughuli zake: kiroho na kimwili. Lakini, jambo la kumshukuru Mungu ni kuona kwamba, Mashirika 162 ya Misaada ya Kanisa Katoliki katika mataifa mbali mbali yameendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa ufanisi mkubwa, huku yakijitahidi kujibu changamoto, matatizo na dharura iliyojitokeza kutokana na kuibuka kwa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Kuna mamilioni ya watu ambao kwa sasa wanaanza kuteseka kutokana na baa la njaa. Hali ya watu wa Mungu nchini Lebanon, Siria na Ukanda wa Mashariki ya Kati katika ujumla wake, inaendelea kudhohofu sana. Hii inatokana na vikwazo vya kiuchumi ambavyo vimewekwa na Jumuiya ya Kimataifa katika baadhi ya nchi zilizoko huko Mashariki ya Kati, lakini waathirika wakubwa ni maskini. Mlipuko huu umesababisha mateso makubwa kwa watu wa Mungu nchini Lebanon. Huu ni wakati muafaka kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kupitia tena sera na mikakati yake kuhusu vikwazo vya kiuchumi, ili kuweza kuboresha maisha ya wananchi wa Lebanon na Ukanda wa Mashariki ya Kati katika ujumla wake.

Caritas Lebanon
07 August 2020, 13:20