Vatican News
Tangu baada ya Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Kanisa limeendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu. Tangu baada ya Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Kanisa limeendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu.  (AFP or licensors)

Mchango wa Mababa wa Kanisa Katika Majadiliano ya Kidini! Amani

Mtakatifu Yohane XXIII na Mtakatifu Paulo VI walisimami utekelezaji wa maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Mt. Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa XVI pamoja na Papa Francisko ni viongozi wa Kanisa waliojipambanua katika mchakato wa majadiliano ya kidini ili kudumisha utu, heshima, haki msingi za binadamu, amani, urafiki na udugu wa kibinadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tangu Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipozindua mchakato wa majadiliano ya kidini katika Tamko lao la “Nostra aetate” yaani “Nyakati Zetu”, kumekuwepo na mafanikio makubwa yanayofumbata amana na utajiri wa maisha ya kiroho; uelewa na udugu wa kibinadamu unaopania kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kati ya waamini wa dini mbali mbali duniani. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kanisa Katoliki halikatai yoyote yaliyo kweli na matakatifu katika dini mbali mbali zisizo za kikristo. Lenyewe laheshimu kwa sifa timamu namna zile za kutenda na kuishi, sheria zile na mafundisho yale ambayo, ingawa mara nyingi yanatofautiana na yale ambayo lenyewe laamini na kufundisha, hata hivyo, mara nyingine, yanarudisha nuru ya mshale wa ule Ukweli wenye kumwangazia kila mtu. Kanisa linaendelea kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, njia, ukweli na uzima. Rej. Yn. 14:6. Ndani ya Kristo Yesu kuna utimilifu wa utauwa, na ambamo Mwenyezi Mungu alivipatanisha vitu vyote na nafasi yake. 

Kanisa pia linawatazama kwa heshima waamini wa dini ya Kiislam, wanaomwabudu Mungu aliye mmoja, mwenye uhai na mwenye kuwepo, rahimu na Mwenyezi, Muumba wa mbingu na dunia, aliyenena na wanadamu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, huwasihi waamini wote ili haki jamii, tunu za kimaadili, amani na uhuru kwa ajili ya watu wote vihifadhiwe na kuhamasishwa kwa juhudi za pamoja. Kuhusiano na Wayahudi, Mama Kanisa anatambua dhamana na wajibu aliokuwa nao Ibrahimu, Baba wa imani. Kanisa linakiri kuwa wokovu wa Kanisa umeaguliwa kifumbo katika “kutoka” kwa taifa teule walipohama toka nchi ya utumwa. Ndiyo maana Kanisa linakumbuka kwamba, limepokea ufunuo wa Agano la Kale kwa njia ya watu wale ambao Mungu katika huruma yake isiyoelezeka, alipenda kufunga agano nao. Kanisa linaamini kwamba, kwa njia ya Fumbo la Msalaba, Kristo Yesu aliwapataanisha Wayahudi na watu wa Mataifa, kuwa wamoja katika nafsi yake.

Kutokana na utajiri mkubwa uliomo kwenye dini ya Wayahudi, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanahimiza umuhimu wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na Wayahudi, ili kufahamiana na kuheshimiana mintarafu Biblia na Taalimungu, ili kudumisha majadiliano ya udugu wa kibinadamu. Kanisa linalaani na kushutumu vikali: chuki, udhalimu na ukatili dhidi ya Wayahudi. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kujizatiti katika majadiliano ya kidini, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, utu, heshima, maridhiano na udugu wa kibinadamu! Ni katika muktadha huu, Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika makala yake kuhusu mchango wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, mintarafu majadiliano ya kidini, anapembua mahusiano kati ya Wakristo, Wayahudi na Waislam. Huu ni mchango mkubwa kutoka kwa Mtakatifu Yohane XXIII na Mtakatifu Paulo VI waliosimamia utekelezaji wa maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Mtakatifu Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa XVI pamoja na Papa Francisko kwa hakika ni viongozi wa Kanisa waliojipambanua kikamilifu katika mchakato wa kumwilisha majadiliano ya kidini katika maisha na utume wa Kanisa. Huu ni mchakato unaopania pamoja na mambo mengine kujenga na kudumisha utu, heshima, haki msingi za binadamu, amani, urafiki na udugu wa kibinadamu. Mtakatifu Paulo VI alipotembelea Uganda kunako mwezi Julai 1969, alikazia kwa namna ya pekee, umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa watu wa Mungu nchini Uganda. Akiwa nchini Uganda, alipata nafasi ya kukutana na kusalimiana na wawakilishi wa dini ya Kiislam. Aliwataka waamini wote kuwa kweli ni vyombo vya haki, amani, msamaha, umoja na upatanisho wa kitaifa. Haya ni mambo msingi yanayohimizwa na Vitabu Vitakatifu. Mtakatifu Yohane Paulo II, daima emeendelea kukazia umuhimu wa majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam, kwa kutambua kwamba, Ibrahimu ni Baba wa imani kwa wote. Majadiliano ya kidini ni kielelezo makini cha uaminifu wa waamini kwa Mwenyezi Mungu.

Ni katika hali na mazingira ya kukuza na kudumisha amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 27 Oktoba 1986 akaitisha mkutano wa sala uliowajumuisha viongozi mbali mbali wa kidini kwa ajili ya sala, kama kielelezo cha umoja na mshikamano na Mwenyezi Mungu. Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya tukio hili la kimataifa, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alionya kwamba, misimamo mikali ya kidini na kiimani; chuki na uhasama pamoja na kufuru ya kutumia jina la Mungu kuchochea vurugu ni mambo yanayohatarisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Vitendo vya kigaidi na mauaji ya kimbari ni kielelezo cha watu kukengeuka na kutopea katika mmong’onyoko wa kanuni maadili na utu wema. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, kwa kukuza na kudumisha utu, umoja na udugu wa kibinadamu, hapo ndipo waamini wa dini zote wanaweza kusema kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Baba wa wote, kwa sababu wote wameumbwa kwa sura na mfano wake. Ukabila, ubaguzi wa rangi na dini ni mambo yanayopingana sana na mapenzi ya Kristo.

Waamini wanahamasishwa kuwa na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, kama yamkini, kwa upande wao, wakae katika amani na watu wote, ili wapate kuwa kweli ni wana wa Baba aliye mbinguni. Kwa hakika mtu asiyejua kupenda, huyo hawezi kumfahamu Mungu kwa sababu Mungu ni upendo. Hati ya Udugu wa Kibinadamu, ilitiwa mkwaju kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Huu ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Hati ya Udugu wa Kibinadamu inapata chimbuko lake katika mikutano elekezi iliyowasaidia waamini wa dini hizi mbili kushirikishana: furaha, majonzi, matamanio yao halali pamoja na changamoto mamboleo zinazoendelea kumwandama mwanadamu! Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika makala yake kuhusu mchango wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, mintarafu majadiliano ya kidini, anahitimisha kwa kusema, mchakato wa kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu ni hatua muhimu sana ya ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa na ni kikolezo kikubwa cha maendeleo fungamani ya binadamu!

Nyakati Zetu
15 August 2020, 08:09