Kardinali Becciu: tafakari ya Matendo makuu ya Mungu inafsishwe katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani. Kardinali Becciu: tafakari ya Matendo makuu ya Mungu inafsishwe katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani. 

Watawa: Matendo Makuu ya Mungu Yanafsishwe Katika Huduma!,

Kardinali Becciu amewataka watawa kusimama kidete na kuendelea kuwa waaminifu kwa Yesu na Kanisa lake sanjari na kuwa waaminifu kwa Karama ya Shirika ambayo kimsingi ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Uaminifu huu unafumbatwa katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Giovanni Angelo Becciu, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Mtakatifu Martha iliyoadhimishwa na Mama Kanisa tarehe 29 Julai 2020, ameongoza Ibada ya Misa Takatifu na kupokea nadhiri za daima za watawa thelathini wa Shirika la Watawa wa Martha na Maria “Suore della Congregazione di Marta y Maria”. Ibada hii ya Misa Takatifu imeadhimishwa kwenye Kanisa la Parokia ya “Sant’ Eugenio” Jimbo kuu la Roma. Hawa ni wanovisi ambao wameamua kujisadaka maisha yao yote kwa ajili ya kuyatafakari matendo makuu ya Mungu na kuyanafsisha katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani ndani ya Shirika la Mtakatifu Martha na Maria. Ni Wanovisi ambao wameitikia kwa dhati kabisa mwaliko kutoka kwa Kristo Yesu ili kujisadaka katika huduma kwa kuweka nadhiri za daima, yaani: ufukara, utii na usafi kamili.

Masista hawa kutoka: Guatemala, Hispania, Venezuela, Italia, Argentina, Honduras, Ethiopia, Cuba, Lithuania, Perù na Chile, wamemwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, tayari kujikita katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kwa neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wako tayari sasa kupambana na changamoto za utandawazi, maendeleo ya sayansi na teknolojia mintarafu mustakabali wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa! Kardinali Giovanni Angelo Becciu amewataka watawa kusimama kidete na kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake sanjari na kuwa waaminifu kwa Shirika na Karama ya Shirika ambayo kimsingi ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu, daima wakiwa tayari kusoma alama za nyakati. Muhtasari wa uaminifu huu unafumbatwa katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.

Wanaitwa kumpenda Kristo Yesu, kichwa cha Fumbo la mwili wake yaani Kanisa. Kumpenda Kristo Yesu ambaye yupo katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu yake Azizi, lakini zaidi, wanaitwa na kutumwa kuwapenda zaidi maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hawa ni maskini wa hali na mali; maskini wa maisha ya kiroho, kimaadili na kiutu, kwa kuwapenda na kuwahudumia kama walivyofanya Martha na Maria katika maisha na utume wao. Watawa hawa thelathini, mbele ya umati mkubwa wa familia ya Mungu, wameamua kusadaka maisha yao yote kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Lakini, ikumbukwe kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wote wanashiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo kama kielelezo cha upendo na majitoleo yao. Kwa njia ya nadhiri za daima, watawa hawa wanajitosa kimasomaso kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kwa njia ya Nadhiri za daima.

Tangu sasa wanapaswa kuishi kikamilifu nadhiri ya ufukara, utii na usafi kamili. Katika ulimwengu mamboleo, huu ni uamuzi mgumu na mzito unaopaswa kusindikizwa kwa sala, sadaka na majitoleo binafsi. Ni fursa ya kumshukuru Mungu kwa wingi wa miito inayoendelea kuchanua kama maua ya kondeni. Masista hawa, wataendelea kuchakarika katika maisha na utume wa Kanisa ndani ya Shirika na katika Majimbo watakapopangiwa na kutumwa. Hii ni furaha ya Kanisa zima, kwani linaendelea kushuhudia kazi ya Roho Mtakatifu anaye endelea kulizawadaia Kanisa la Kristo wingi wa neema, karama na miito ya kitawa, tayari kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Kardinali Giovanni Angelo Becciu anasema wito, maisha na utume wa Masista hawa walioweka nadhiri za daima, unaongozwa na tafakari ya kina inayonafsishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani, kama ilivyokuwa kwa Familia ya Martha na Maria, ilipomkaribisha Kristo Yesu kati yake. Waendelee kutoa nafasi kwa Kristo Yesu katika maisha yao, ili aweze kuwatembelea na kwa uwepo wake mwanana, alete mageuzi makubwa katika maisha, wito na utume wao.

Jambo la msingi ni kujenga utamaduni wa kumsikiliza Kristo Yesu katika Neno lake, Sakramenti za Kanisa, lakini zaidi kwa kuwasikiliza na kuwajibu maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Watambue kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa huruma, upendo, faraja na msamaha unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Matendo ya huruma yanayotekelezwa kwa moyo wa upendo na sadaka ya kweli ni muhimu sana katika maisha ya watawa na waamini katika ujumla wao! Kardinali Giovanni Angelo Becciu amewataka watawa kuhakikisha kwamba, wanampatia Kristo Yesu nafasi ya kwanza katika maisha na utume wao, ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo, vinginevyo wataishia kulalama, daima wakiwa na “litania za manung’uniko yasiyokuwa na mvuto wala mashiko, kiitikio ambacho kimekosa waitikiaji! Watawa wajifunze kukaa miguuni pa Kristo Yesu ili kusikiliza Neno lake, tayari kumwilisha Neno hili katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani.

Watawa wamekumbushwa kwamba, Nadhiri za daima zinagusa maisha yao yote yaani: mahusiano na mafungamano ya kijamii; akili, utashi na nguvu zao. Hii ni sadaka kubwa inayofumbatwa katika uaminifu na uhuru kamili, kwa kusaidiwa na neema pamoja na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kardinali Giovanni Angelo Becciu amehitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, Kanisa linawahitaji watawa wanaojisadaka kwa kusikiliza Neno la Mungu, kwa maisha ya sala na maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa, ili Mwenyezi Mungu aweze kupewa sifa, utukufu na heshima na mwanadamu kutakaswa na kutakatifuzwa. Kanisa linawahitaji watawa wenye ujasiri na wabunifu ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo kwa njia ya ushuhuda wa nadhiri ya ufukara, utii na usafi kamili, mambo ambayo kwa walimwengu yanaonekana kana kwamba, yamepitwa na wakati. Watu wana kiu na uchu wa mali na madaraka, lakini watawa kwa njia ya nadhiri zao, wako tayari kujisadaka kwa ajili ya Mungu na huduma kwa jirani zao; huduma inayofumbatwa katika unyenyekevu wa moyo, maisha ya kijumuiya, daima Mwenyezi Mungu na jirani wakipewa kipaumbele cha kwanza.

Itakumbukwa kwamba, Shirika la Watawa wa Martha na Maria “Suore della Congregazione di Marta y Maria” lilianzishwa tarehe 6 Januari 1979 huko Jalapa nchini Guatemala. Hizi zilikuwa ni juhudi za Askofu Miguel Ángel García y Aráuz, na Mama Ángela Eugenia Silva Sánchez. Shirika hili linatekeleza dhamana na utume wake huko Amerika ya Kusini, Afrika na katika nchi kadhaa za Ulaya. Ni Shirika ambalo linaendelea kuchanua na kushamiri kwa miito, kwani hadi mwaka 2020 lina watawa 700.

Kard. Becciu: Watawa

 

 

 

30 July 2020, 13:46