Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi la Askofu Josè Càmnate na Bissign wa Jimbo Katoliki Bissau la kung'atuka kutoka madarakani. Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi la Askofu Josè Càmnate na Bissign wa Jimbo Katoliki Bissau la kung'atuka kutoka madarakani. 

Askofu Josè Càmnate na Bissign Ang'atuka Kutoka Madarakani!

Askofu mstaafu José Câmnate na Bissign alizaliwa mwaka 1953 huko Guinea Bissau. Akiwa na umri wa miaka 29 alipewa Daraja Takatifu ya Upadre mwaka 1982. Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 15 Oktoba 1999 akamteuwa kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Bissau na kuwekwa wakfu, 2000. Tarehe 11 Julai 2020, Papa Francisko ameridhia ombi lake la kutaka kung’atuka kutoka madarakani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowakilishwa kwake na Askofu José Câmnate na Bissign wa Jimbo Katoliki Bissau, Guinea-Bissau la kutaka kung’atuka kutoka madarakani. Historia inaonesha kwamba, Askofu mstaafu José Câmnate na Bissign, alikuwa ni Padre mzalendo wa kwanza kuteuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu kunako tarehe 15 oktoba 1999 na kuwekwa wakfu tarehe 12 Februari 2000 wakati wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2000 ya Ukristo. Ni Askofu aliyejizatiti kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki Bissau kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2020. Itakumbukwa kwamba, Askofu mstaafu José Câmnate na Bissign alizaliwa tarehe 28 Mei 1953 huko Mansôa, Guinea Bissau.

Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akiwa na umri wa miaka 29 alipewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 31 Desemba 1982. Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 15 Oktoba 1999 akamteuwa kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Bissau na hatimaye, kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 12 Februari 2000. Tarehe 11 Julai 2020, Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lake la kutaka kung’atuka kutoka madarakani. Askofu mstaafu José Câmnate na Bissign, anakumbukwa sana katika maisha na historia ya watu wa Mungu nchini Guinea Bissau kwa kujisadaka bila ya kujibakiza katika mchakato wa majadiliano kiekumene, kidini na kisiasa nchini mwake.

Alijipambanua kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu wakati alipokuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani, Baraza la Maaskofu Katoliki Guinea Bissau. Waswahili wanasema, “mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni”. Yamekuwa ni mapokeo ya miaka mingi, kuandika mambo machache sana kwa Maaskofu wanapong’atuka kutoka madarakani. Lakini, hawa ni viongozi ambao wamejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika majimbo mahalia, Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Askofu mstaafu José Câmnate na Bissign ni mfano bora wa kuigwa!

Jimbo Katoliki la Bissau
13 July 2020, 07:03