Vatican News
Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye Makao yake Makuu mjini Roma, Ijumaa, tarehe 5 Juni 2020 imeadhimisha mkesha kwa ajili ya kuombea amani na utulivu nchini Marekani baada ya machafuko ya ubaguzi wa rangi. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye Makao yake Makuu mjini Roma, Ijumaa, tarehe 5 Juni 2020 imeadhimisha mkesha kwa ajili ya kuombea amani na utulivu nchini Marekani baada ya machafuko ya ubaguzi wa rangi.  (ANSA)

Mkesha kwa ajili ya kuombea amani na utulivu nchini Marekani

Binadamu wote ni sawa kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Amani na haki jamii; umoja, utulivu na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ni mambo msingi katika maisha ya jamii yoyote ile. Marekani ni nchi ambayo imeonja na kuguswa na saratani ya ubaguzi wa rangi kati ya miaka ya 1960 hadi mwaka 1970. Mateso haya hayakupatiwa ufumbuzi wa kudumu hadi leo hii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye Makao yake Makuu mjini Roma, Ijumaa tarehe 5 Juni 2020 imeadhimisha mkesha wa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea umoja, amani na utulivu nchini Marekani, baada ya kukumbwa na vurugu za kijamii kutokana na mauaji ya kikatiliki ya Bwana George Floyd. Mauaji haya yamesababisha hasira kubwa, majonzi, huzuni na wasi wasi mkubwa kutokana na vitendo vya chuki na ubaguzi wa rangi pamoja na maamuzi mbele. Binadamu wote ni sawa kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Amani na haki jamii; umoja, utulivu na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ni mambo msingi katika maisha ya jamii yoyote ile. Marekani ni nchi ambayo imeonja na kuguswa na saratani ya ubaguzi wa rangi kati ya miaka ya 1960 hadi mwaka 1970. Ni mateso ambayo yameacha madonda makubwa katika dhamiri za watu, lakini kwa bahati mbaya, hayakupata ufumbuzi wa kudumu ndiyo maana hata wakati huu yanaendelea kujitokeza na kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Utu, heshima, haki msingi za binadamu; umoja na udugu wa kibinadamu ni tunu msingi zinazopaswa kurithishwa kutoka kizazi hadi kizazi na kuendelea kupyaishwa, ili tunu hizi msingi zisichafuliwe na dhambi, kiasi cha kusababisha ukosefu wa haki msingi, vurugu na ghasia pamoja na ukandamizaji wa utu na heshima ya binadamu! Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha katika mkesha wa kuombea umoja, amani na utulivu nchini Marekani, uliofanyika kwenye Kanisa kuu la “S. Maria in Trastevere” lililoko mjini Roma. Ni wajibu wa waamini kutangaza na kushuhudia upya wa Injili unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Waamini watambue kwamba, wao ni Mahekalu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Amani ni zawadi ya Kristo Mfufuka inayopaswa kuendelezwa na kudumishwa na wote kwa njia ya ushuhuda makini wa maisha.

Waamini wawe na ujasiri wa kuwatambua na kuwathamini jirani zao walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Waheshimu na kuthamini umoja na tofauti zao msingi kwani huu ni utajiri na amana kubwa ya kazi ya uumbaji. Amani ya Kristo inayoishi ndani mwao, iwawezeshe kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Waamini wawe ni mashuhuda wa Injili ya huruma, upendo na upatanisho wa kweli, ili kujenga udugu wa kibinadamu. Marekani ni nchi ambayo imeasisiwa kutokana na vurugu na kinzani mbali mbali za maisha, lakini, ikafanikiwa kujipatia uhuru wa kweli na kuanza kujielekeza katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika usawa, wakiwa wana uhuru na haki ya kuishi; kwa kuvumiliana hata katika tofauti zao, ili kila mtu aweze kujipatia ustawi na maendeleo kwa ajili yake binafsi na jamii katika ujumla wake. Hivi ni vinasaba vya maisha ya wananchi wa Marekani anasema, Kardinali Kevin Joseph Farrell.

Mafundisho Jamii ya Kanisa yawe ni kielelezo na mwongozo wa Wakristo katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yao katika jamii. Watu wajenge upendo na mshikamano; kwa kusaidiana na kushikamana; huku wakiendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Upendo wenye huruma na wokovu wa Mungu uwaambate na kuwakumbatia watu wote pasi na ubaguzi. Ubaguzi ni dhambi kubwa na hatari katika mafungamano ya kijamii. Injili ya Kristo Yesu iwe ni silaha madhubuti ya kuchochea ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na hivyo kuondokana na ubaguzi unaoweza kufanywa kwa misingi ya kiitikadi, kitaifa au kikabila. Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu, kwa kuendelea kujikita katika ujenzi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu! Huu ni wakati wa kujenga utamaduni wa watu kukutana katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana na kuthaminiana.

Chuki, vita, vurugu na ghasia ni hatari sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Waamini wajielekeze zaidi katika kudumisha misingi ya haki, usawa pamoja na kuendelea kujikita katika utawala wa sheria. Ubaguzi ni dhambi ambayo kamwe haiwezi kufumbiwa macho kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Waamini wawe waaminifu kwa Injili ya Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake! Wasimame kidete kulinda na kudumisha utu, heshima, haki msingi, ustawi na maendeleo ya wote sanjari na ujenzi wa udugu wa kibinadamu!

Vurugu Marekani
06 June 2020, 14:27