Serikali ya Hungaria inaadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 30 tangu ilipoanzisha uhusiano wa Kidiplomasia na Vatican: 1990-2020. Serikali ya Hungaria inaadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 30 tangu ilipoanzisha uhusiano wa Kidiplomasia na Vatican: 1990-2020. 

Miaka 30 ya Uhusiano wa Kiplomasia: Hungaria na Vatican

Serikali ya Hungaria imetoa msaada wa barakoa 45, 000 kwa ajili ya kusaidia wafanyakazi wa Vatican kujikinga na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Msaada huu umetolewa kama sehemu ya kumbukizi la miaka 30 tangu Hungaria na Vatican walipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia. Kumekuwepo na mafanikio makubwa kwa pande zote mbili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Kanisa liko karibu pamoja na wale wote wanaoteseka kutokana na  athari za maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Mama Kanisa anapenda kuwapatia watu wa Mungu ulinzi na tunza yake ya kimama wagonjwa na wale wote ambao wameathirika kutokana na ugonjwa huu ambao haubagui wala hauchagui. Katika kipindi hiki cha shida na mahangaiko ya ndani, watu wengi wanaonekana kutaharuki, kuchanganyikiwa pamoja na kuingiwa na hofu juu ya hatima ya maisha yao kwa siku za usoni.

Inaonekana kwamba, watu wengi wamesongwa na pingu za magonjwa na kifo kiko malangoni pao! Hawana tena mahali pa kuwaombolezea ndugu, jamaa na rafiki zao, Corona, COVID-19 imesababisha maafa makubwa duniani. Sera na mikakati ya kupambana na Virusi vya Corona, COVID-19 inapaswa kuratibiwa na Shirika la Afya Duniani, WHO, ili hatimaye, dunia iweze kuondokana na Virusi vya Corona, COVID-19. Kuna haja ya kuangalia jinsi ya kuboresha usafirishaji wa dawa na vifaa tiba kwa ajili ya kupambana na Virusi vya Corona, COVID-19. Jikinge na uwakinge na wengine ndiyo kauli mbiu ya Kimataifa inayoongoza mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Hivi karibuni, Serikali ya Hungaria imetoa msaada wa barakoa 45, 000 kwa ajili ya kusaidia wafanyakazi wa Vatican kujikinga na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Ubalozi wa Hungaria mjini Vatican ulimkabidhi msaada huo Fra Binish Thomas Mulackal, Mkurugenzi mkuu wa Duka la Dawa Mjini Vatican. Huu ni msaada kidogo ikilinganishwa na mahitaji makubwa ya vifaa vya kinga kwa ajili ya wafanyakazi wa Vatican, lakini ulikuwa na umuhimu wa pekee sana kwani ilikuwa ni sehemu ya kumbukizi ya Miaka 30 tangu Hungaria ilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican, kunako mwaka 1990. Serikali ya Hungaria imesema, itaendeleza umoja na mshikamano na Vatican katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Barokoa nyingine zimetolewa kwa ajili ya mahitaji ya Kanisa ndani na nje ya Vatican.

Hungaria Miaka 30 ya Diplomasia na Vatican
11 May 2020, 13:54