Kumbukumbu ya Mashujaa Askari Walinzi wa Papa Clement VII waliofariki dunia tarehe 6 Mei 1527. Ibada ya Misa Takatifu pamoja na kula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kumbukumbu ya Mashujaa Askari Walinzi wa Papa Clement VII waliofariki dunia tarehe 6 Mei 1527. Ibada ya Misa Takatifu pamoja na kula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. 

Kumbukumbu ya Walinzi wa Papa Kutoka Uswiss, 6 Mei 1527

Jumatano tarehe 6 Mei 2020 Wanajeshi wa Kikosi cha Ulinzi wa Papa kutoka Uswiss, watafanya kumbu kumbu ya askari 147 kutoka Uswiss walioyamimina maisha yao mjini Roma kwa ajili ya kumtetea Papa Clemente VII kunako mwaka 1527. Kutokana na maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 hakuwa na shamra shamra kubwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kikosi cha Walinzi wa Papa kutoka Uswiss, maarufu kama “Swiss Guards” kina dhamana na utume unaojikita katika wito, uaminifu, umakini na sadaka inayotekelezwa kwa moyo wa unyenyekevu pasi na makuu. Jumatano tarehe 6 Mei 2020 Wanajeshi wa Kikosi cha Ulinzi wa Papa kutoka Uswiss, wanafanya kumbu kumbu ya askari 147 kutoka Uswiss walioyamimina maisha yao mjini Roma kwa ajili ya kumtetea Papa Clement VII kunako mwaka 1527. Kutokana na maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 maadhimisho haya yatatangazwa moja kwa moja na vyombo vya mawasiliano na mitandao ya jamii inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican kwa kuzingatia protokali inayodhibiti maambukizi ya Corona, COVID-19. Monsinyo Luigi Roberto Cona ataongoza Ibada ya Misa Takatifu kuanzia saa 11: 00 za jioni kwa Saa za Ulaya. Mashuhuda hawa watakumbukwa kwa kuwekewa shada la maua kwenye mnara wa mashahidi ulioko kwenye Uwanja wa “Promartiri Romani” saa 12:00 jioni kwa Saa za Ulaya. Askofu mkuu Edgar Peña Parra, Katibu mkuu Msaidizi wa Vatican ndiye mgeni rasmi katika sherehe hizi ambazo zitawawezesha wawakilishi wa wanajeshi hawa kula kiapo kwa niaba ya wenzao! Ukipenda unaweza kufuatilia matukio haya kwa njia ya anuani ifuato: http://www.guardiasvizzera.ch/

Katika tukio kama hili mwaka 2019 Baba Mtakatifu Francisko, alikutana na kuzungumza na wanajeshi hawa waliokuwa wameandamana na wanafamilia wao kutoka Uswiss. Baba Mtakatifu aliwashukuru kwa ukarimu na sadaka yao kwa ajili ya ulinzi na usalama kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na Kanisa. Kila siku, anaonja majitoleo yao, weledi na upendo unaobubujika kutoka katika shughuli zao! Baba Mtakatifu anawapongeza wana familia wa wanajeshi hawa ambao wameridhia uamuzi wao wa kujisadaka kwa ajili ya Vatican na kuendelea kuwasindikiza kwa upendo na sala zao. Baba Mtakatifu aliwakumbusha kwamba, mwaka huo, wanajeshi hawa wanakula kiapo cha utii wakati ambapo Mama Kanisa anaendelea kushangilia Fumbo la Pasaka, changamoto na mwaliko hata kwa wao kuwa ni mashuhuda wa Kristo Mfufuka, kwa kutangaza furaha ya Pasaka; kwa kueneza utamaduni wa Ufufuko wa wafu dhidi ya utamaduni wa kifo, unao onekana kutaka kuwameza watu wengi.

Katika maisha na utume, hata wao wamewahi kukutana na watu ambao “wanaelemewa na makaburi”; watu wasiokuwa na dira wala mwelekeo wa maisha; watu wenye shida na mahangaiko makubwa. Hawa ni wale wanaotarajia kuona mwanga utakaopyaisha maisha na hatimaye, kuzaliwa upya! Baba Mtakatifu aliwasihi wanajeshi hawa wapya kuwaendea watu wote hawa kwa maneno ya faraja; kukutana nao katika alama ya udugu, ili kwa pamoja waweze kuwa kweli ni mashuhuda hai wa Kristo Mfufuka; Alfa na Omega, nyakati zote ni zake! Hii ndiyo njia muafaka ya kuishi kikamilifu wito wao wa Kikristo unaopata chimbuko lake kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, chemchemi ya imani! Wakati wote watakapokuwa hapa Roma, wanahimizwa kushuhudia imani yao kwa furaha, ili mahujaji na wageni wanaotembelea mjini Vatican waweze kuonja na kuguswa na ari pamoja na sadaka ya maisha yao inayofumbatwa na upendo wa Mungu kwa kila binadamu. Huu ndio wito wa kwanza kabisa kwa kila mwamini!

Baba Mtakatifu aliwataka wanajeshi wapya kuwa jasiri, huku wakiendelea kuimarishwa na imani kutoka kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Wawe ni mashuhuda na mitume wa upyaisho wa maisha binafsi na yale ya kijumuiya, kama kielelezo cha utakatifu wa maisha unaobubujika kutoka katika huduma na maisha ya kijumuiya. Watu wanataka kuona utakatifu wa maisha kutoka kwa wafanyakazi wa Vatican! Kambi ya Jeshi iwe ni mahali pa kujifunza kanuni maadili na tunu msingi za maisha ya kiroho, ili kukuza na kudumisha majadiliano, ukweli wa maisha, mahusiano mema pamoja na kuelewana. Katika hali na mazingira kama haya, kutakuwepo na nyakati za furaha pamoja na nyakati za majonzi. Kipindi hiki, kiwe ni fursa ya kujenga urafiki mwema, kwa kuheshimu na kuthamini mawazo yanayotolewa na wengine; kwa kuendelea kujifunza kuona kwa mwingine yule ndugu na jirani ambaye ni mwadani wa safari ya pamoja.

Tabia hii itawawezesha kuishi katika Jamii wakiwa na mwelekeo sahihi wa maisha, kwa kutambua tofauti za kitamaduni, kidini na kijamii kama amana na utajiri na wala si tishio la maisha. Hii ni changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo kutokana na uwepo wa makundi makubwa ya watu wanaotafuta usalama na maisha bora zaidi. Mwishoni, mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu aliwashukuru wanajeshi hawa wapya kwa sadaka na majitoleo yao na kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Padri Thomas Widermer, Padri mshauri wa kiroho wa Kikosi cha Ulinzi wa Papa kutoka Uswiss anasema, wanajeshi hawa ambao wengi wao ni vijana, wenye matumaini makubwa mbele yao, wanaunda Parokia ya pekee na kumbe, kazi ya Padri mshauri ni kuhakikisha kwamba, anawasaidia katika majiundo na ukomavu wa maisha ya kiroho na kimwili. Wanatambua kwamba, hapa Roma ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu, kumbe, hata wao wanapaswa kuwa na mtazamo na mwelekeo kama huu wanapotekeleza dhamana na utume wao kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Padri Widermer katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano anasema, kuna sababu mbali mbali ambazo zinaweza kuwasukuma vijana kutaka kujiunga na Kikosi cha Ulinzi wa Papa. Mosi ni kwamba, vijana wanataka kupata uzoefu, mang’amuzi na weledi kuhusiana na wito pamoja na taaluma ya kijeshi. Wengi wao, hii ni nafasi ya kukua na kukomaa katika imani, matumaini na mapendo, kwa kufanya utume wao karibu sana na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Wanatambua kwamba, ufahamu wa mazingira ya mji wa Vatican na lugha ya Kiitalia ni utajiri mkubwa ambao unaacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo zao wakati wote! Padri mwongozi wa maisha ya kiroho amepewa dhamana ya kuhakikisha kwamba, anawasaidia vijana hawa wanaojiandaa kwa utume maalum, kukua na kukomaa katika maisha ya kiroho na kiutu. Kwa mfano, wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, walijifunzaa kwa umakini mkubwa kuhusu dhana ya huruma ya Mungu kama inavyofafanuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume, Uso wa huruma, “Misericordiae vultus”.

Katika majiundo yao, wanapata katekesi ya kina na endelevu kuhusu: uaminifu, maana ya sadaka na zawadi ya maisha; ulinzi na usalama; dhamana na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika Kanisa la Kristo. Hiki pia ni kipindi kinachowawezesha askari hawa kupata utajiri wa kitamaduni kwa kufanya hija katika maeneo muhimu ya kihistoria. Wanajeshi hawa wanajifunza kwa kina na mapana matendo ya huruma kiroho na kimwili, kwani ni sehemu ya vinasaba vya utume wao. Mara nyingi hawa ndio wanaomsindikiza mtunza sadaka mkuu wa Papa katika kuwasaidia maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii katika mitaa ya Roma nyakati za usiku, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Swiss Guards
05 May 2020, 13:26