Mtakatifu Maria Faustina Kowalska: Kumbu kumbu ya Miaka 20 tangu kutangazwa kwake kuwa Mtakatifu, Jumapili ya Huruma ya Mungu, tarehe 30 Aprili 2000. Mtakatifu Maria Faustina Kowalska: Kumbu kumbu ya Miaka 20 tangu kutangazwa kwake kuwa Mtakatifu, Jumapili ya Huruma ya Mungu, tarehe 30 Aprili 2000. 

Mtakatifu Maria Faustina Kowalska wa Huruma ya Mungu

Mtakatifu Faustina Kowalska alizaliwa tarehe 25 Agosti 1905. Mwaka 1925 akajaribu kuanza maisha ya kitawa ndani ya Shirika la Masista wa Mama wa Mungu wa huruma. Tarehe 3 Aprili 1927 anatokewa na muujiza, Mwaka 1931 akaanza utume wake katika tasaufi ya huruma ya Mungu. Mwaka 1993 akaweka nadhiri za daima. Mwaka 1938 akafariki dunia. Mwaka 1993 Mwenyeheri!

Na Padre Wojciech Adam Koscielniak, Hekalu la Huruma ya Mungu, -Musoma.

AGOSTI 25, 1905 Helena anazaliwa kama mtoto wa tatu wa wazazi wake Marianna na Stanislaus Kowalski katika kijiji cha Glogowiec, Wilaya ya Turek, Mkoa wa Łódź, Poland (kwa mujibu wa kumbukumbu za Parokia yake) AGOST 27, 1905 akabatizwa katika kanisa la Mt. Kasimiri, Kijiji cha Świnice Warckie, Wilaya ya Turek, na Padre Joseph Chodyński. Alipewa jina la Ubatizo - Helena. Wazazi wake wa Ubatizo walikuwa Konstanty Bednarek na Marianna Szewczyk (Szczepaniak). 1912 Katika umri wa miaka 7, wakati wa Masifu ya Jioni parokiani kwake, Helena akaonja Upendo wa Mungu na kusikia sauti rohoni mwake ya kuitwa kwa maisha ya ukamilifu. 1914 Anapokea Komunyo Takatifu ya Kwanza kutoka kwa Padre Roman Pawłowski, paroko wa Parokia ya Świnice Warckie. 1917 Helena Kowalska naanza elimu ya msingi katika shule ya msingi Świnice Warckie. 1921 Katika umri wa miaka 16, Helena anaanza kufanya kazi za ndani katika familia ya Kazimierz na Leokadia Bryszewski, katika mji wa Aleksandrów Łódzki. OKTOBA 30, 1921 akapewa Sakramenti ya Kipaimara katika Parokia ya Aleksandrów Łódzki kutoka kwa Mhashamu Baba Askofu Wincent Tymiennicki 1922 Baada ya kufanya kazi za ndani mwaka mmoja katika nyumba ya familia ya Bryszewski, alirudi nyumbani kutanganza nia yake ya kujiunga na Shirika la Kitawa. Wazazi wake wakataa kata kata nia yake hiyo. VULI 1922 Helena akaenda jiji la Łódź kutafuta kazi nyingine. Anafikia kwenye nyumba ya mjomba wake Michał Rapacki katika Mtaa wa Krośnieńska. Huko Akafanya kazi kwa Watawa wa Kifranciskani wa Utawa wa Tatu.

FEBRUARI 2, 1923 Anaanza kufanya kazi kwa Marcjanna Sadowska, mmiliki wa duka katika Mtaa wa Ambramowski 29 katika jiji la Łódź. JULAI 1924. Helena alikwenda mji mkuu wa Poland - Warsaw - kujaribu kujiunga na Shirika la Kitawa. Anafanya kazi kwa Aldona Lipszycowa katika mji wa Ostrówek, kata ya Klembów. Anaomba kujiunga na Shirika la Masista wa Mama wa Mungu wa Huruma katika Mtaa wa Żytnia 2/3 katika Mji Mkuu wa Warsaw. Mama Mkuu Michaela Moraczewska anampa kibali cha awali cha kumpokea Shirikani. AGOSTI 1, 1925 Helena Kowalska anapokelewa rasmi katika Shirika la Masista wa Mama wa Mungu wa Huruma katika Mtaa wa Żytnia 2/3 jijini Warsaw. AGOSTI 1925 Mpostulanti Helena Kowalska anapelekwa nyumba ya mapumziko katika mji wa Skolimów karibu na Warsaw kwa lengo la kuimarisha afya yake iliyokuwa dhaifu. Mwaka 1925 Upostulanti wa Helena Kowalska unaanza katika nyumba ya kitawa jijini Warsaw chini ya malezi ya Mama Janina Bartkiewicz. JANUARI, 23 1926 Helena Kowalska anasafiri kutoka jiji la Warsaw kwenda jiji la Kraków kwa ajili ya kuhitimisha kipindi cha Upostulanti wake na kuingia katika kipindi cha miaka miwili ya malezi ya Kinovisi chini ya Mama Małgorzata Gimbutt na Mama Maria Josepha Brzoza. APRILI 30, 1926 Helena Kowalska akavishwa vazi la kitawa na kupewa jina la kitawa Sr. Maria Faustina.

APRILI 3, 1927 Sista Faustina anatokewa na muujiza wa usiku wa giza. Jaribu hili linadumu karibu kipindi chote cha unovisi. Mama Mkuu, Mary Joseph Brozoza anamtia moyo, anampumzisha katika taratibu za kila siku za kiimani, na kumsihi kuzidi kuwa mwaminifu mbele za Mungu. (Hafidhi, 1:80. APRILI 20, 1928 Sista Maria Faustina anaanza mafungo kabla ya nadhiri za kwanza. APRILI 30, 1928 Sista Maria Faustina anaweka nadhiri zake za kwanza (usafi kamili wa moyo, utii na ufukara) kwa kipindi cha mwaka mmoja. Itakumbukwa kwamba, nadhiri za kwanza hurudiwa kila mwaka hadi hatua ya kuweka nadhiri za maisha. OKTOBA 31, 1928 Sista Faustina anarudi jiji la Warsaw na kupewa kazi ya upishi katika nyumba ya kitawa ya Shirika lake. FEBRUARI 21, 1929 Sista Maria Faustina anasafiri hadi mji wa Vilnius kuchukua nafasi ya Sista Petronela Basiura aliyeondoka kwenda katika hatua ya Jaribio la Tatu katika malezi yake. JUNI 11, 1929 Sista Maria Faustina anarudi jiji la Warsaw na kuendelea kuishi na kufanya kazi katika nyumba ya kitawa ya Shirika lake iliyoko Mtaa wa Żytnia. JUNI 1929 Sista Maria Faustina anahamia katika nyumba mpya ya Shirika lake iliyoko Mtaa wa Hetmańska, kata ya Grochów, jiji la Warsaw. JULAI 7, 1929 Sista Maria Faustina anatumwa kwenye nyumba ya Shirika katika mji wa Kiekrz, karibu na Poznań, kukaimu nafasi ya mpishi ya sista Modesta Rzeczkowska aliyekuwa anaumwa.

OKTOBA 1929 Sista Maria Faustina anaendelea kuishi katika Makao Makuu ya Shirika katika Mtaa wa Żytnia, jiji la Warsaw. MEI - JUNI 1930. Sista Maria Faustina anawasili mji wa Płock na kufanya kazi katika duka la kiwanda cha mikate. • Sista Faustina anaishi katika konventi iliyoko Biała, kilometa 10 kutoka mji wa Płock. FEBRUARI 22, 1931 Mwanzo wa utume katika maisha ya Sista Faustina. Maono ya kwanza ya Yesu wa Huruma na agizo la Bwana la kuchora Picha Takatifu (Płock). FEBRUARI 1931 Agizo la Bwana Yesu la kuweka Sikukuu ya Huruma ya Mungu siku ya Dominika ya Pili ya Pasaka (Jumapili inayofuata Dominika ya Sherehe ya Pasaka). 1930-1932 Makazi ya muda mfupi na muda mrefu katika konventi ya Biała, jirani na mji wa Płock. NOVEMBA 1932 Mafungo katika Walendów. Maungamo ya Sista Faustina kwa Padre Edmund Elter SJ na uthibitisho wa kwanza wa uhalisia wa maono aliyokuwa anayapata Sista Faustina. DESEMBA 1, 1932 Sista Maria Faustina anaanza Jaribio la Tatu katika mchakato wa malezi yake chini ya Mama Małgorzata Gimbutt. MACHI 1933 Wanda, mdogo wake Sista Faustina anamtembelea katika Makao Makuu ya Shirika katika Mtaa wa Żytnia, jijini Warsaw. APRILI 18, 1933 Sista Maria Faustina anawasili jijini Kraków.

APRILI 21, 1933 Mwanzo wa mafungo ya siku nane kabla ya kuweka nadhiri za maisha. Mafungo yaliongozwa na Padre Antoni Bronisław Wojnar SJ. Maungamo kwa Padre Józef Andrasz SJ. MEI 1,1933 Sista Faustina anaweka nadhiri za maisha mbele ya Mhashamu Baba Askofu Stanisław Rospond. MEI 25, 1933 Anaondoka kwenda Vilnius kupitia mji wa Częstochowa. Huko Vilnius anapewa jukumu la kutunza bustani. JUNI 1933 Sista Maria Faustina anakutana kwa mara ya kwanza na Padre Michał Sopoćko, mwungamishaji wake na baba yake wa kiroho huko Vilnius, aliyeteuliwa na Mungu kuwa msaidizi wake katika kutimiza utume aliopewa na Mungu. JANUARI 2, 1934 Sista Faustina kwa mara ya kwanza anakwenda kwa msanii Eugeniusz Kazimirowski. Anasindikizwa na Mama mkuu wa nyumba, Mama Irena Krzyżanowska. MACHI 29, 1934 Sista Faustina anaweka hati ya majitoleo kamili ya maisha yake yote kwa ajili ya wokosefu, hasa kwa roho zilizopoteza matumaini yao kwa Huruma ya Mungu. JUNI 1934 Uchoraji wa picha ya Yesu wa Huruma, uliofanywa na msanii Kazimirowski chini ya uangalizi wa Sista Faustina, umekamilika. Sista Faustina anaangua kilio baada ya kuona picha na kulalamika kwamba Yesu katika picha hii si mzuri kama alivyomwona katika maono. JULAI 26, 1934 Sista Faustina ni mgonjwa - ameugua mafua. AGOSTI 12, 1934 Sista Maria Faustina anazidiwa katika ugonjwa wake. Padre Michał Sopoćko anampatia Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa. AGOSTI 13, 1934 Sista Faustina anapata nafuu katika ugonjwa wake.

MACHI 4, 1935 Sista Petronela na Sista Faustina wanakwenda na gari la mizigo katika mnada “na Kazika” uliokuwa unafanyika siku ya Sikukuu ya Mt. Kasimiri kila mwaka kwa ajili ya manunuzi ya vyombo na vitendea kazi kwa ajili ya nyumba yao ya kitawa. APRILI 26-28, 1935 Picha ya Yesu wa Huruma huonyeshwa hadharani kwa mara ya kwanza katika Ostra Brama mjini Vilnius. MEI 1935 Sista Faustina anapata maono ya kwanza yahusuyo wazo la kuanzisha Shirika jipya. SEPTEMBA 13-14, 1935 Sista Maria Faustina anapata maono yahusuyo Rozari ya Huruma ya Mungu. SEPTEMBA 29, 1935 Sista Fautina pamoja na Watawa wenzake anashiriki katika Ibada ya Masaa 40 katika Kanisa la Mt. Michaeli. OKTOBA 19, 1935 Sista Faustina anaelekea jiji la Kraków kwa ajili ya mafungo ya siku nane. NOVEMBA 4, 1935 Sista Faustina anarudi Vilnius kupitia Częstochowa baada ya kuhitimisha mafungo ya siku nane. JANUARI 8, 1936 Sista Maria Faustina anamtembelea Mhashamu Baba Askofu Romuald Jałbrzykowski na kushirikisha dai la Yesu la kuanzisha Shirika jipya la kitawa. MACHI 17, 1936 Sista Borgia Tichy, Kiongozi wa Makao – Vilnius anapata habari kutoka kwa Mama Mkuu juu ya kuhamishwa kituo Sista Faustina kutoka Volnius kwenda Walendow. (Vil. Chron. Uk. 337).

MACHI 21, 1936 Sista Faustina anaondoka mji wa Vilnius na kurejea jiji la Warsaw. MACHI 25, 1936 Sista Faustina anawasili mji wa Walendów, kisha anaelekea Derdy. MEI 11, 1936 Akisindikizwa na Sista Edmunda Sękul, Sista Maria Faustina anaondoka Derdy na kwenda jiji la Kraków kuishi huko hadi mwisho wa maisha yake. MEI 12, 1936 Sista Faustina anawasili jiji la Kraków. JUNI 19, 1936 Akiwa na Watawa wengine, Sista Faustina anashiriki katika maandamano ya Moyo Mtakatifu wa Yesu katika basilika la Shirika la Wajesuiti katika Mtaa wa Kopernik jijini Kraków. SEPTEMBA 14, 1936 Mhashamu Baba Askofu Mkuu Romuald Jałbrzykowski anatembelea Makao Makuu ya Shirika jijini Kraków na kuzungumza na Sista Faustina. SEPTEMBA 19, 1936 Sista Faustina anafanyiwa uchunguzi wa kiafya katika hospitali ya Prądnik jijini Kraków. OKTOBA 20, 1936 Akiwa katika jiji la Kraków, anashiriki mafungo ya siku nane. DESEMBA 9, 1936 Kwa sababu za kiafya, Sista Faustina anapelekwa hospitali ya Prądnik. DESEMBA 24, 1936 Kwa ruhusa ya daktari, Sista Maria Faustina anarejea nyumbani Shirikani apate kushiriki Sherehe ya Noeli na Watawa wenzake.

DESEMBA 27, 1936 Anarudi tena hospitali ya Prądnik kwa ajili ya matibabu zaidi. MACHI 27, 1937 Anarejea konventini Łagiewniki kutoka hospitalini, afya yake ikiwa imeimarika. APRILI 13, 1937 Hali ya Afya ya Sista Faustina inarudi kuwa mbaya. APRILI 14, 1937 Muujiza wa uponyaji wa Sista Faustina. Yesu anamwambia - “Enenda, ukamwambie Mamea kwamba u mzima”. APRILI 23, 1937 Sista Faustina anafanya mafungo ya siku tatu. MEI 4, 1937 Sista Faustina anapata ruhusa kutoka kwa Mama Mkuu Michaela Moraczewska kuondoka Shirikani lakini kwa sababu ya giza nene la kiroho hatumii ruhusa hiyo akitambua kwamba katika uamuzi huo hakuna Mapenzi ya Mungu. MEI 20, 1937 Sista Faustina anarejea hali yake ya kiafya aliyokuwa nayo kabla ya uponyaji wa kimuujiza akiamua kumtumikia Yesu katika hali inayompendeza Bwana zaidi. JULAI 29, 1937 Sista Faustina anaondoka Kraków kulelekea mji wa Rabka kwa matibabu zaidi. AGOSTI 10, 1937 Sr. Faustina anarudi Krakow. AGOSTI 12, 1937 Padre Michał Sopoćko anakutana na Sista Faustina katika konventi ya Kraków-Łagiewniki. AGOSTI 25, 1937 Padre Sopoćko hubakia Kraków kwa siku kadhaa na anaendelea kupata fursa ya kukutana na kuzungumza na Sista Faustina katika konventi ya Łagiewniki.

SEPTEMBA 6, 1937 Kutokana na kuendelea kudhoofika kiafya, Sista Faustina anabadilishiwa majukumu Shirikani - anaondolewa katika kazi ya mtunza bustani na kupewa jukumu la kuwa mlinzi wa mlangoni. SEPTEMBA 19, 1937 Kaka yake Stanisław anamtembelea Sista Faustina konventini. SEPTEMBA 27, 1937 Sista Faustina akisindikizwa na Mamea Mama Irena Krzyżanowska, anakwenda kampun ya uchapishaji kwa ajili ya kuagiza uchapishaji wa picha takatifu za Yesu wa Huruma. Anapata fursa ya kusali katika Basilika ya Bikira Maria jijini Kraków. OKTOBA 1937 Akiwa katika konventi ya Kraków-Łagiewniki, Sista Faustina anapewa maono yahusuyo Saa Kuu ya Huruma ya Mungu. APRILI 21, 1938 Afya ya Sista Faustina inadhoofika zaidi, viongozi wanaamua kumpeleka tena hospitali ya Prądnik tena. JULY1938 Mama Mkuu Michaela Moraczewska anamtembelea Sista Faustina akiwa hospitalini Prądnik. AGOSTI 1938 Mama Mkuu Moraczewska anamtembelea katika hospitali. (Kumb. za Mama Michael Uk. 10; Kumb. Sista Felicia). AGOSTI 24, 1938 Mamea Mama Irena Krzyżanowska anakesha usiku kucha pembeni mwa kitanda cha Sista Faustina hospitalini Prądnik. AGOSTI 25, 1938 Padre Teodor Czaputa, baba wa kiroho wa konventi ya Kraków-Łagiewniki anampatia Sista Faustina Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa akiwa hospitalini Prądnik. AGOSTI 28, 1938 Padre Michał Sopoćko anawasili Kraków na kumtembelea Sista Faustina mara kadhaa hospitalini Prądnik.

SEPTEMBA 17, 1938 Sista Faustina anarudi konventini Łagiewniki. SEPTEMBA 22, 1938 Akiwa anazidi dhoofika zaidi, kwa mujibu wa desturi ya Shirika anaomba radhi Watawa wenzake kwa makosa yoyote yale ambayo aliyatenda pasipo kukusudia. SEPTEMBA 26, 1938 Padre Michał Sopoćko anakutana na Sista Faustina kwa mara ya mwisho. Sista Faustina anamwambia kwamba “amejikita katika muungano kamili na Baba wa mbinguni”. OKTOBA 5, 1938 • Saa 10.00 jioni - Padre Józef Andrasz anamuungamisha Sr. Faustina kwa mara ya mwisho, • Baba wa kiroho wa konventi ya Kraków-Łagiewniki - Padre Teodor Czaputa akiwa na Watawa wenzake wa Sista Faustina wanadumu katika sala za kumwombea. Saa 4.45 usiku, Sr. Faustina akaaga dunia. Sista Amelia Socha na Sista Eufemia Traczyńska ni mashuhuda wa kifo chake. OKTOBA 7, 1938 Mazishi ya Sista Maria Faustina Kowalska yakafanyika siku ya Ijumaa ya kwanza ya mwezi. Ilikuwa ni Sikukuu ya Bikira Maria Malkia wa Rozari Takatifu. Padre Władysław Wojtoń SJ aliadhimisha Misa ya Mazishi katika Altare kuu ya Kanisa la Shirika na Padre Tadeusz Chabrowski SJ aliadhimisha Misa ya kumwombea Sista Faustina katika Altare ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Hakuna ndugu yeyote wa Sista Faustina aliyeshiriki Mazishi yake mwa sababu Sista Faustina hakutaka nduguze waingie gharama kubwa ya safari. Sista Faustina alizikwa katika makaburi ya Shirika katika bustani ya konventi ya Łagiewniki.

MACHI 6, 1959 Vatican ikaondoa hati ya pingamizi dhidi ya Ibada ya Huruma ya Mungu na kuwakataza waamini kueneza Ujumbe na Ibada ya Huruma ya Mungu kama ulivyofafanuliwa na Kristo Yesu kupitia kwa Sr. Faustina (Acta Apostolicae Sedis, uk. 271). OKTOBA 21, 1965 Mwadhama Karol Kardinali Wojtyła, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kraków, anaanzisha mchakato wa kumtangaza Sr. Faustina kuwa Mwenye heri na hatimaye Mtakatifu. Kikao cha kwanza cha mchakato kinasimamiwa na Mhashamu Baba Askofu Julian Groblicki, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Kraków. NOVEMBA 25, 1966 Mwili wa Sista Faustina unahamishiwa Kanisa la Shirika Kraków-Łagiewniki kutoka makaburini na kuzikwa upya chini ya sakafu ya kanisa hilo. SEPTEMBA 20, 1967 Mwadhama Kardinali Karol Wojtyła, anafunga mchakato wa utafiti wa maisha na fadhila za Sr. Faustina katika Jimbo Kuu la Kraków. Nyaraka zote zikapelekwa kwenye Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu.  APRILI 15, 1978 Hati ya pingamizi ya Kiti cha Kitume inafutwa (tangazo lilitolewa tarehe 30/6/1978 katika Acta Apostolicae Sedis, uk. 350). 1981 Chapisho la kwanza la SHAJARA ya Sr. Maria Faustina Kowalska inatolewa. APRILI 18, 1993. Baba Mtakatifu Yohane Paulo II anamtangaza Sr. Maria Faustina Kowalska kuwa Mwenye Heri. Tamko hili linatolewa wakati wa Misa Takatifu Kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kunafanyika uzinduzi rasmi wa Masalia Matakatifu ya Mwenye Heri Sista Faustina katika Altare ya Picha ya Yesu wa Huruma katika kanisa la konventi ya Shirika lililoko Kraków-Łagiewniki.

JUNI 7, 1997 Hija ya Mtakatifu Yohane Paulo II katika Kituo cha Hija cha Huruma ya Mungu - Kraków-Łagiewniki. Sala mbele ya Picha ya Yesu wa Huruma na mbele ya Masalia Matakatifu ya Mwenye Heri Sr. Faustina. APRILI 30, 2000 Mwenye Heri Sr Maria Faustina Kowalska anatangazwa kuwa Mtakatifu na Papa Yohane Paulo II kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican,  Dominika ya Pili ya Pasaka. Kupitia kwenye matangazo mubashara ya luninga waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wakiwemo na mahujaji katika Kituo cha Hija Kraków-Łagiewniki, waliweza kushiriki kikamilifu. Baba Mtakatifu Yohane Paulo II anatangaza kwamba Dominika ya Pili ya Pasaka, itakuwa ni Sikukuu ya Huruma ya Mungu kwa Kanisa zima la ulimwengu. AGOSTI 17, 2002 Hija ya pili ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo II katika Kituo cha Hija cha Kraków-Łagiewniki . Ibada ya kutabaruku Kanisa kuu la Huruma ya Mungu na Sala ya majitoleo kamili ya ulimwengu mzima (kutakatifuza ulimwengu mzima) kwa Huruma ya Mungu. 2005 Chapisho la kwanza la BARUA za Sr. Faustina hutolewa. MEI 27, 2006 Baba Mtakatifu Benedikto XVI anasali mbele ya Picha ya Yesu wa Huruma na mbele ya Masalia Matakatifu ya Mt. Sista Faustina katika Kituo cha Hija cha Kraków-Łagiewniki. JULAI 30, 2016 Hija ya Baba Mtakatifu Francisko (wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani - Krakow, Poland kuanzia tarehe 26-31/7/2016) katika Kituo cha Hija cha Kraków-Łagiewniki na sala yake binafsi mbele ya Picha ya Yesu wa Huruma na mbele ya Masalia ya Mtakatifu Faustina.

Mtakatifu Faustina
20 April 2020, 13:44