Mapadre ni wahudumu wakuu wa Sakramenti za Huruma ya Mungu; wawe karibu na wale wote waliokata tamaa na kuvunjika moyo kutokana na changamoto mbali mbali za maisha! Mapadre ni wahudumu wakuu wa Sakramenti za Huruma ya Mungu; wawe karibu na wale wote waliokata tamaa na kuvunjika moyo kutokana na changamoto mbali mbali za maisha! 

Fumbo la Pasaka: Wahudumu wa Sakramenti za Huruma ya Mungu

Mapadre watekeleze utume wao, kwa kuwa karibu zaidi na watu wa Mungu wanaoteseka. Wawaonjeshe uwepo wa karibu, huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa kristo Yesu. Pale ambapo imeshindikana kabisa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa hadharani, basi Mapadre wanahamasishwa kusali zaidi na kuwafariji wale wote wanaoteseka, kwa kuwazamisha katika huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, huruma ya Mungu kwa namna ya pekee kabisa, inaadhimishwa kwenye Sakramenti ya Upatanisho, ambapo Mwenyezi Mungu anamkumbatia mdhambi na kumpatia tena neema ya kutubu na kumwongokea, tayari kuendelea na safari ya maisha ya kiroho. Huruma na upendo wa Mungu unajionesha katika maisha ya watu kwa kuwasaidia kutubu na kuongoka, ili hatimaye, kushirikiana na Mwenyezi Mungu kama vyombo na mashuhuda wake. Kwa njia ya Fumbo la Pasaka, Mwenyezi Mungu ameweza kuupatanisha ulimwengu wote pamoja naye na kwa Sakramenti ya Upatanisho, Mungu anachukua hatua ya kwanza ili kuonesha upendo kwa mdhambi, kama ilivyo kwa Mama Kanisa kuanza kwa ushupavu kuwaendea na kuwatafuta walioanguka na kutopea dhambini, waliotengwa na kuwakaribisha tena ili kuwaonjesha mang’amuzi ya huruma na upendo wa Mungu, ambayo ni matunda ya nguvu ya Baba isiyokuwa na kikomo!

Mapadre ni wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu, yaani: Ekaristi Takatifu inayowajalia waamini chakula cha njiani katika hija ya maisha yao hapa bondeni kwenye machozi pamoja na Sakramenti ya Upatanisho, inayowaonjesha waamini, huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao, tayari hata wao kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu, inayomwilishwa katika vipaumbele vya maisha yao! Mapadre waungamishaji wawe ni vyombo vya faraja kwa waamini wanaotubu na kumwongokea Mungu na kwamba, mang’amuzi ya Sakramenti ya Upatanisho yawaonjeshe watu upendo na huruma ya Mungu. Mapadre wawasaidie waamini kutambua udhaifu na dhambi zao, kwa kuwapokea na kuwakumbatia kama Baba Mwenye huruma, ili waamini hao,  waweze kukutana na Mwenyezi Mungu katika undani wa maisha yao, Mungu ambaye daima ni mwingi wa huruma na mapendo!

Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Idara ya Toba ya Kitume inayojulikana kwa lugha ya Kilatini kama "Penitenzieria Apostolica" amewaandikia mapadre na waungamishaji barua katika kipindi hiki ambacho Mama Kanisa anajiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka. Lakini kwa mwaka huu 2020, maadhimisho haya ambayo ni kiini cha imani ya Kanisa yanakabiliwa na changamoto kubwa ya maambuzi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kuna ukame mkubwa wa maisha ya kiroho kutokana na itifaki zinazopaswa kuzingatiwa ili kuzuia maambukizi ya Virus vya Corona, COVID-19. Pamoja na changamoto zote hizi, lakini huruma na upendo wa Mungu hauwezi kufungwa na wala Mwenyezi Mungu hawezi kuwaacha waja wake wanaomkilimbilia kwa machozi wakiomba huruma yake isiyokuwa ni mipaka. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kuzingatia mashari yaliyowekwa ili kudhibiti Virusi vya Corona, COVID-19, lakini maisha na utume wa Kanisa unapaswa kuendelea.

Mapadre watekeleze dhamana na utume wao, kwa kuwa karibu zaidi na watu wa Mungu wanaoteseka na kukata tamaa. Wawaonjeshe uwepo wa karibu, huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa kristo Yesu. Pale ambapo imeshindikana kabisa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa hadharani, basi Mapadre na wauangamishaji wanahamasishwa na Mama Kanisa kusali na kuwafariji wale wote wanaoteseka, kwa kuwazamisha katika huruma ya Mungu. Kardinali Mauro Piacenza anawashukuru na kuwapongeza Mapadre wote ambao wamejisadaka bila ya kujibakiza katika kipindi hiki kigumu cha maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 kiasi cha kuhatarisha na hata Mapadre wengi kupoteza maisha yao. Mapadre waendelee kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu; kwa kuonesha huduma na upendeleo wa pekee kwa maskini, wagonjwa na wale wote waliopondeka na kuvunjika moyo! Wawe karibu na wagonjwa walioko kufani, madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika sekta ya afya, ambao wanaendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu.

Mapadre wawaangalie na kuwajulia hali, wazee na watu pweke ambao wamewekwa karantini. Kuna baadhi ya watu wanapambana sana na maisha kwani hawana hata mahitaji msingi ya binadamu; wote hawa Mama Kanisa anapaswa kuwaendea kwa moyo wa huruma na ukarimu. Mapadre watambue kwamba, hata pale wanapo adhimisha Ibada ya Misa Takatifu faraghani, bado neema na huruma ya Mungu inawaendelea waja wake. Sadaka ya Yesu Msalabani ni chemchemi ya wokovu na upatanisho wa Mungu na mwanadamu. Mapadre wanahimizwa kutekeleza yale mambo msingi katika maisha na utume wao wa Kipadre, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu na kwamba, Mapadre wanayo dhamana kubwa katika utekelezaji wa utume wa Kanisa ulimwenguni! Maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa ni chemchemi ya neema na baraka, ni ushuhuda wa Injili ya upendo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu!

Kwa njia ya Sakramenti za Huruma ya Mungu, Mwenyezi Mungu anaendelea kuwaganga, kuwaponya na kuwasamehe watu wake dhambi zao. Katika kipindi hiki kigumu katika historia ya mwanadamu katika ulimwengu mamboleo, kuna haja ya kugundua tena thamani ya ukimya katika maisha; fumbo la mateso na kifo katika maisha ya mwanadamu; umuhimu wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu hata katika mazingira ya kifamilia kwa kutambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani. Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Idara ya Toba ya Kitume anawahimiza waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kumwabudu Mungu katika: ukimya, sala na huduma kwa jirani. Mama Kanisa ana amini na kufundisha kwamba, uzima wa waamini hauondolewi ila unageuzwa tu. Nayo makao ya hapa duniani yakisha bomolewa, waamini wanakirimiwa makao ya milele mbinguni. Kumbe, mauti na kifo, kamwe hakiwezi kubomoa mahusiano na mafungamano ya waamini, bali yanaimarishwa zaidi katika muungano na watakatifu!

Kardinali: Fumbo la Pasaka
09 April 2020, 15:04