Bikira Maria alikuwa na nafasi ya pekee katika maisha na utume wa Kristo Yesu. Bikira Maria alikuwa na nafasi ya pekee katika maisha na utume wa Kristo Yesu. 

Tafakari Kipindi cha Kwaresima 2020: B.Maria Katika Maisha ya Yesu Hadharani

Padre Cantalamessa, katika tafakari yake, amefafanua kuhusu maneno ya Yesu “Mama, tuna nini mimi nawe”: Kujishuhusha kwa Mama wa Mungu”. Bikira Maria katika maisha yake alijifunza kutii kutokana na mateso yake; Bikira Maria alikuwa na nafasi ya pekee katika maisha ya hadhara ya Kristo Yesu, kiasi kwamba, akawa ni mfuasi waminifu wa Yesu hata katika ukimya wa ndani! Kujishusha

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kauli mbiu inayoongoza tafakari za Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2020 zinazotolewa kwa Baba Mtakatifu Francisko, wasaidizi wake wa karibu, yaani “Curia Romana”, wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ni: “Na penye Msalaba wake Yesu alikuwa amesimama mamaye” Rej. Yoh. 19:25). Bikira Maria katika Fumbo la Pasaka ya Kristo Yesu. Huu ni mwendelezo wa tafakari iliyotolewa na Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa wakati wa Kipindi cha Majilio kwa Mwaka 2019-2020. Padre Cantalamessa, katika tafakari yake, Ijumaa, tarehe 20 Machi 2020 amefafanua kuhusu maneno ya Kristo Yesu “Mama, tuna nini mimi nawe”: Kujishuhusha kwa Mama wa Mungu”. Bikira Maria katika maisha yake alijifunza kutii kutokana na mateso yake; Bikira Maria alikuwa na nafasi ya pekee katika maisha ya hadhara ya Kristo Yesu, kiasi kwamba, akawa ni mfuasi waminifu wa Yesu hata katika ukimya!

Tafakari ya Kipindi cha Kwaresima inaendelea kufuata nyayo za Bikira Maria, kwa kuomba ulinzi na tunza yake ya daima hasa wakati hii, binadamu wanapopambana na Virusi vya Corona, COVID-19. Maandiko Matakatifu hayazami sana kuelezea maisha ya Bikira Maria, lakini anaonekana kwa namna ya pekee katika matukio makuu ya Fumbo la Ukombozi: Katika Fumbo la Umwilisho, Pasaka na Pentekoste. Haya ni matukio ambao yamempatia Bikira Maria kipaumbele cha pekee katika historia ya kazi ya Ukombozi kwa kushiriki katika mateso ya Kristo Yesu. Tomaso, aitwaye Pacha, akawaambia wanafunzi wenziwe, “Twendeni na sisi, ili tufe pamoja naye”. Lakini kwa bahati mbaya wakati wa mateso, walitimua mbio na Bikira Maria akayaishi maneno haya pale chini ya Msalaba.

Bikira Maria alijifunza kutii kutokana na mateso yake kwani maisha yote ya Kristo Yesu, tangu kuzaliwa kwake ilikuwa ni Njia ya Msalaba kuelekea katika Fumbo la Pasaka: katika mateso, kifo na ufufuko wake. Yesu akaonesha utii wa hali ya juu na hivyo kubahatika kuwa Adamu mpya, kama alivyofanya pia Bikira Maria, Eva mpya, ambaye upanga uliingia moyoni mwake, ili yafunuliwe mawazo ya wengi. Bikira Maria akahifadhi yote moyoni mwake na kuendelea kuyatafakari katika hija ya maisha ya Yesu hadharani. Ni Mama aliyebahatika kuwa Mtakatifu na mwingi wa neema, baraka na imani. Ni mfano bora wa kuigwa ili kuweza kukabiliana kikamilifu na changamoto za maisha.

Mtakatifu Paulo Mtume anasema, Kristo Yesu, ambaye yeye mwanzo alikuwa yu namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho, bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa binadamu. (Rej. Flp. 2: 6-7). Hii ni hali ya kujimimina katika unyenyekevu, yaani “kenosis” kama anavyosema Mtakatifu Yohane Paulo II. Akiwa chini ya Msalaba, kwa njia ya imani, Bikira Maria aliungana na Kristo Yesu katika mchakato huo wa kujimimina kama kielele cha hija iliyoanza tangu mwanzo wa maisha ya Yesu hadharani. Hii ilikuwa ni hija ya imani. Matukio yote haya yanaonesha maana ya maisha ya Bikira Maria kwa Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake mintarafu ufafanuzi uliotolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Tangu mwanzo Bikira Maria alikuwa na upendeleo wa pekee kwa kukingiwa dhambi ya asili, lakini alishiriki pia mateso na changamoto mbali mbali za maisha ya nyakati zake na kwa njia hii aliweza pia kushiriki kikamilifu katika mateso ya Kristo Yesu, kielelezo cha hija ya maisha ya imani. Mwenyezi Mungu alimtaka Bikira Maria kutoa sadaka kubwa zaidi. Kristo ni mfano wa Kuhani mkuu anayeshiriki mateso na mahangaiko ya watu wake kwa njia ya utii hata kifo cha Msalaba. Bikira Maria akajifunza kuwa mtii kutokana na  mateso yake; akaonesha utii katika imani; alijaribiwa na kutikiswa, lakini akabaki na imani thabiti bila kutenda dhambi.

Bikira Maria katika maisha ya Yesu hadharani: Maneno ya Yesu kwa Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu walipomkuta pale Hekaluni yanakatisha tamaa kwani yaliweka mpaka mkubwa kati ya Mama na Mwana, kiasi cha baadhi ya watu kudhani kwamba, mahusiano yao yalikuwa hayana nguvu sana. Ombi la Bikira Maria kwa Yesu kwenye  Harusi ya Kana, liliacha maswali mengi kuliko hata majibu yaliyotolewa. Injili pacha zinasimuliwa tukio hili katika maisha ya Yesu hadharani. Bila shaka wengi wanakumbuka jinsi ambavyo Bikira Maria pamoja na ndugu zake walivyohofia afya ya Yesu kutokana na mahubiri yake, lakini hata hivyo, Bikira Maria hakupata nafasi ya kuweza kuonana na kuzungumza naye kama sehemu ya haki ya Mama kwa mtoto! Maneno ya Yesu yalikuwa ni machungu kana kwamba, yalikuwa yanamdharirisha Bikira Maria.

Bikira Maria alijitosa katika imani na kujimimina kama wanawake wengine na wala hakung’ang’ania kupewa upendeleo wa pekee na badala yake, akaacha upanga wenye makali mawili kupenya moyoni mwake. Katika maisha na utume wake, Kristo Yesu hakuwa na mahali pa kulaza kichwa chake kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria hakuwa na mahali pa kutulizia moyo wake, akawa ni shuhuda wa ufukara wa maisha ya kiroho, lakini tajiri wa matumaini. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alimfundisha Bikira Maria, jinsi ya kujisadaka na kujitoa bila ya kujibakiza, tayari kutekeleza mapenzi na mpango wa Mungu katika maisha yake.

Padre Raniero Cantalamessa, anaendelea kufafanua kwamba, Bikira Maria alijifunza kuwa mwanafunzi amini wa Kristo Yesu katika hali ya unyenyekevu. Aliendelea kumjifunza Kristo Yesu katika ukimya na imani: Akabahatika kuwa ni Mama wa Mungu na mwanafunzi msikivu wa Neno la Mungu alilolimwilisha katika vipaumbele vya maisha yake. Kristo Yesu alimpatia heshima ya hali ya juu kabisa kama Mama yake. Hii ikawa ni chemchemi ya furaha yake ya daima, hata pale ambapo hakuweza kuyafahamu kwa dhati kabisa mafumbo ya maisha ya Kristo Yesu. Kumbe, waamini wanaye Mama ambaye anafahamu fika kuhusu udhaifu na karama walizojaliwa na Mwenyezi Mungu, mwaliko ni kuendelea kumfuata Bikira Maria kama ambavyo yeye mwenyewe anavyomfuata Kristo Yesu. Katika kipindi hiki cha mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu kutokana na maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-16, Padre Raniero Cantalamessa alihitimisha mahubiri yake, kwa sala ifuatayo: Tunakimbilia ulinzi wako mzazi Mtakatifu wa Mungu usitunyime tukiomba katika shida zetu tuopoe siku zote kila tuingiapo hatarini, Ee Bikira Mtukufu na mwenye baraka. Amina.

Bikira Maria

 

 

 

20 March 2020, 15:58