Siku ya Wanawake Duniani 2020: Dhamana na wajibu wa wanawake katika kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu! Siku ya Wanawake Duniani 2020: Dhamana na wajibu wa wanawake katika kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu! 

Siku ya Wanawake Duniani 2020: Wanawake wajenzi wa udugu wa kibinadamu!

Wanawake walioshiriki katika mkutano wa maandalizi ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Mwaka 2020 wanasema, Hati hii ya Kimama inawafumbata na kuwaambata watu wote duniani kama chanzo cha hija ya pamoja. Hati hii inakazia pia haki msingi za wanawake, vijana na watoto. Ni hati inayotambua na kuthamini umoja, utofauti na utajiri unaojionesha kati ya watu wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Mwaka 2020 inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Machi, kwa kuongozwa na Kauli mbiu “Wanawake katika mshikamano tutaendeleza mapambano”, Jumanne, tarehe 3 Machi 2020 limefanya mkutano wa kiekumene na kidini mjini Roma. Mkutano umeratibiwa na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini pamoja na wawakilishi wa nchi mbali mbali mjini Vatican. Umehudhuriwa na wanawake kutoka katika dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo, kwa lengo la kujadili kwa kina na mapana “Dhamana na wajibu wa wanawake katika kudumisha udugu wa kibinadamu”.

Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Maisha ya Pamoja, iliyotiwa mkwaju kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari  2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu, ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini na madhehebu mbali mbali, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Maisha ya Pamoja inapata chimbuko lake katika mikutano elekezi iliyowasaidia waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo kushirikishana: furaha, majonzi, matamanio yao halali pamoja na changamoto mamboleo zinazoendelea kumwandama mwanadamu!Wanawake walioshiriki katika mkutano wa maandalizi ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Mwaka 2020 wanasema, Hati hii ya Kimama inawafumbata na kuwaambata watu wote duniani kama chanzo cha hija ya pamoja. Hati hii inakazia pia haki msingi za wanawake, vijana na watoto. Ni hati inayotambua na kuthamini umoja na utofauti unaojionesha kati ya watu wa Mungu mintarafu dini, rangi, jinsia, tabaka na lugha zao kama sehemu ya mapenzi ya Mungu kwa binadamu, walioumbwa kwa sura, mfano na hekima yake. Wanawake hawa wanakubaliana kimsingi kuendeleza tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii ambazo zimebainishwa katika “Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Maisha ya Pamoja”.

Wanawake wanapania kusimama kidete kupambana na uchoyo na ubinafsi, kwa kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Mwenyezi Mungu anayewakirimia zawadi ya maisha inayopaswa kulindwa na kudumishwa; kwa kuwasaidia maskini, watu waliokata tamaa; watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na wale wote wanaojisadaka katika ujenzi wa utamaduni wa kiutu! Wanawake hawa wanataka kusimama kidete kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; kwa kushirikiana kwa karibu zaidi na wanasiasa, vyombo vya mawasiliano ya jamii, wachumi, wadau wa elimu, sayansi na sanaa sanjari na vijana wa kizazi kipya ili kuhakikisha kwamba, dini zinakuwa ni chombo cha ujenzi wa amani duniani, na kamwe dini zisitumike kuchochea chuki, uhasama na vita; na badala yake, waamini wa dini mbali mbali waheshimiane na kuthaminiana.

Wanawake wanataka pamoja na mambo mengine kujielekeza zaidi katika kukuza fadhila ya upendo wenye huruma na ujasiri katika imani ili kujiimarisha pamoja na kukuza kipaji cha ubunifu, ili kupambana kufa na kupona kama sehemu ya harakati za kung’oa mifumo yote ya utumwa mamboleo inayodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hawa ni watu wanaoathirika kutokana na umaskini na baa la njaa; kwa kutaka kilio cha watu hawa kiweze kusikika katika Jumuiya ya Kimataifa. Wanawake wamedhamiria kuboresha uwezo wao wa kulinda na kutetea uhai; kwa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Wanawataka kuwa ni madaraja yanayowakutanisha watu kutoka katika tamaduni na staarabu mbali mbali za dunia, ili kila mtu aweze kutajirishwa na tamaduni za wengine, kwa kushirikishana na kujadiliana katika ukweli na uwazi.

Wanawake wa imani wanakubaliana kimsingi juu ya tofauti zao za kidini; wanataka kujielimisha zaidi kwa kushirikiana na wanawake wenzao ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu. Ni katika muktadha huu, wanawake wa imani wanawaalika watu wote wenye mapenzi mema na wale wanaotaka kuishi katika misingi ya haki na amani, kuwaunga mkono katika makubaliano haya, kama kielelezo cha urafiki wa kijamii unaofumbatwa katika misingi ya kuheshimiana! Wakati huo huo, Kauli mbiu ya Kitaifa ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa mwaka 2020 nchini Tanzania inasema: “Kizazi cha Usawa kwa Maendeleo ya Tanzania ya Sasa na Baadae”. Kwa mwaka huu, Maadhimisho yataendelea kufanyika katika ngazi ya Mkoa ili kutoa wigo mpana kwa wanawake, wadau mbalimbali na kila Mtanzania kutathmini hatua tulizofikia kama Taifa katika masuala ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake na wasichana.

Siku ya Wanawake Ulimwenguni 2020

 

 

04 March 2020, 11:51