Tafakari ya Mafungo Kipindi cha Kwaresima: "Msiogope"! Safari ya Jangwani ni mada ambazo zimechambuliwa na Padre Pietro Bovati, SJ., Jumatano tarehe 4 Machi 2020, huko Ariccia. Tafakari ya Mafungo Kipindi cha Kwaresima: "Msiogope"! Safari ya Jangwani ni mada ambazo zimechambuliwa na Padre Pietro Bovati, SJ., Jumatano tarehe 4 Machi 2020, huko Ariccia. 

Mafungo ya Kiroho: Msiogope! Safari ya Jangwani! Uasi, huruma na upendo wa Mungu!

“Msiogope na Safari ya Jangwani” ndiyo mada kuu mbili zilizoongoza tafakari ambayo Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuifuatilia akiwa kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha, mjini Vatican. Katika ulimwengu mamboleo watu wamegubikwa na woga na wasiwasi kwa sababu wanajihisi kuwa kama mavumbi. Watu wamegubikwa na hofu kwa sababu wanajihisi kuwa kama mavumbi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwenyezi Mungu alimteua na kumtuma Musa kwenda kwa Farao, ili apate kuwaokoa watu wake, hao wana wa Israeli katika Misri. Haki msingi za Waisraeli waliokuwa ugenini, wakinyanyaswa na kunyonywa, zinapewa kipaumbele katika wito, maisha na utume wa Musa. Hii ndiyo changamoto mamboleo inayopaswa kudumishwa kwa ajili ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Tafakari wakati wa mafungo maisha ya kiroho Kipindi cha Kwaresima kwa wasaidizi wa karibu wa Baba Mtakatifu, “Curia Romana” kuanzia tarehe 1 Machi hadi 6 Machi, 2020 huko Ariccia nje kidogo ya mji wa Roma, inaongozwa na Padre Pietro Enrico Bovati, SJ, Katibu mkuu wa Tume ya Kipapa ya Biblia na Mtaalam wa Sayansi ya Maandiko Mtakatifu. Kauli mbiu ya mafungo haya ni “Kile kijiti kiliwaka moto: mkutano kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu mintarafu mwanga wa Kitabu cha Kutoka, Injili ya Mathayo na Sala ya Zaburi”.

Padre Pietro Enrico Bovati, SJ, katika tafakari yake, Jumatano, tarehe 4 Machi 2020: “Msiogope” na “Safari ya Jangwani” ndizo mada kuu mbili zilizoongoza tafakari ambayo Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuifuatilia akiwa kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha, mjini Vatican. Katika ulimwengu mamboleo watu wamegubikwa na woga na wasiwasi kwa sababu wanajihisi kuwa kama mavumbi. Neno la Mungu linawatia shime kupambana kufa na kupona hasa pale binadamu anapokabiliana na changamoto pamoja na magumu ya maisha. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Waisraeli katika Agano la Kale walipokuwa wanajiandaa kuvuka kwenye Bahari ya Shamu (Rej. Kut. 14:1-31). Katika Agano Jipya, Yesu alipowaendea wafuasi wake huku akitembea juu ya bahari wakafadhaika na kushikwa na hofu (Rej. Mt. 14:22-32). Lakini Kristo Yesu akawatuliza na kuwaambia “Jipeni moyo, ni mimi, msiogope”.

Kuna wakati hata viongozi wa Kanisa wanashikwa na hofu, woga na wasi wasi, lakini wanapaswa kuiga mfano wa Musa, Mtumishi wa Mungu, aliyekuwa mwaminifu, mtiifu na jasiri aliyetumiwa na Mwenyezi Mungu kama chombo cha kuwatia matumaini Waisraeli ili waweze kuvuka Bahari ya Shamu. Hata ikiwa ni usiku wa manane, kwa kutaabika na mawimbi na upepo mkali kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wa Yesu, bado hii inakuwa ni fursa ya kushuhudia ufunuo wa utukufu wa Mungu. Hata katika mazingira kama haya, Mwenyezi Mungu anawatengenezea njia waja wake, ili kuwashirikisha Fumbo la Pasaka. Katika mateso na kifo, Kristo Yesu, alionja usaliti, upweke na hata kukataliwa na watu aliojisadaka kuwahudumia kiroho na kimwili. Katika mazingira kama haya hakuna njia ya mkato katika maisha ya kiroho.

Huu ni ushuhuda ulioneshwa hata na Musa akiwa Jangwani. Watu wengi wana hofu, woga na wasi wasi kwa sababu wanajihisi kuwa “si mali kitu; wanajifananisha na mavumbi au maua ya kondeni, kiasi hata cha kujikatia tamaa hata katika maisha ya kiroho na hivyo kusahau ahadi ya Mungu kwa waja wake na kuanza kukumbuka “Masufuria ya nyama na vikapu vya vitunguu saumu”. Watu wa Mungu wakashindwa kuona thamani yao kama watu huru na kuanza kumshutumu Musa kwa mambo mengi. Katika muktadha huu, Musa akaibuka kidedea kwa kuwapatia maneno ya imani, matumaini na faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu, tofauti kabisa na tunu msingi za kibinadamu. Musa, Mtumishi wa Mungu akawatia shime na kuwaimarisha katika imani ya uwepo endelevu wa Mungu kati yao. Huu ni ushuhuda wa nguvu ya kinabii kwa ajili ya ukombozi wa watu wa Mungu unaofumbatwa katika huruma na upendo.

Padre Pietro Enrico Bovati anaendelea kufafanua kwamba, hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa wanafunzi wa Yesu, walipomwona Yesu akitembea juu ya Bahari, wakati chombo chao kina taabika sana na mawimbi. Hapa wanafunzi wanagubikwa na “jinamizi la usiku wa manane, wanaonja hatari kubwa mbele yao; wanaonja upweke kwa kutokuwa na Yesu kati yao”. Yesu anapowatokea, giza la usiku wa manane, hofu na woga wa kifo vinatoweka kwa Yesu mwenyewe kuwatia shime “Jipeni moyo, ni mimi, msiogope”. Hii ni changamoto kwa viongozi wa Kanisa kuwashirikisha huruma na upendo wa Mungu wale wote waliokata tamaa na kuanza kutembea katika uvuli wa mauti. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa faraja kama wao wenyewe walivyofarijiwa na Mwenyezi Mungu. Wakleri watambue kwamba, wao ni vyombo vya huruma ya Mungu, hija inayowaongoza watu wa Mungu katika upya wa maisha kwa sababu uwepo wa Mungu kati yao ni chemchemi ya faraja.

Kristo Yesu katika maisha na utume wake amewahurumia na kuwasamehe watu dhambi zao; akawaganga na kuwaponya magonjwa yao; akawalisha na kuwanywesha katika kisima cha upendo, haki na amani. Ni kwa njia hii, waamini wanaweza kumkiri Kristo Yesu kuwa kweli ni Mwana wa Mungu aliye hai. Ushuhuda huu unapaswa kumwilishwa katika upendo wa kitume unaoonesha uwepo endelevu wa Mungu anayeokoa! Padre Pietro Enrico Bovati katika tafakari yake ya jioni amegusia kuhusu Safari ya Jangwani Sinai; Mwenyezi Mungu alifanya Agano na Israeli na kuwapatia Amri 10, taratibu na maagizo ambayo walipaswa kuyafuata. Jangwani, Waisraeli wanaonesha uasi, wanatenda dhambi na kumwabudu ndama ya dhahabu. Dhambi hii inaweza kufafanuliwa kuwa ni ukosefu wa imani kwa Mwenyezi Mungu, kiasi cha kuvunja ile Amri ya Kwanza: Usiabudu miungu wengine. Huu ni upofu wa imani unaozungumziwa na Kristo Yesu katika Agano Jipya! Dhambi itaendelea kubaki katika nyoyo za waamini ikiwa kama watashindwa kutambua, kuitubu na kuomba msamaha.

Kristo Yesu anatoa “Ole kwa Mafarisayo” kwa sababu wao wanasema, lakini wanashindwa kutenda, kumbe si mfano bora wa kuigwa. Waamini wanapaswa kumpatia Mwenyezi Mungu utukufu na kamwe wasimwabudu mwanadamu. Waamini wajitahidi katika safari ya maisha yao ya kiroho kutambua; ukweli na haki; huruma, upendo na msamaha; uaminifu pamoja na kujikita kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi; mambo yanayopaswa kumwilishwa katika matendo, ili kuondokana na unafiki katika maisha ya kiroho kama ilivyokuwa kwa Mafarisayo! Waisraeli waliabudu ndama ya dhahabu, kielelezo cha upofu wa imani kwa kushindwa kutambua uwepo endelevu wa Mungu katika maisha yao, kwa kuvunja Sheria na Amri za Mungu.

Hiki ni chanzo kikuu cha dhambi na utepetevu wa maisha ya kiroho na kiutu. Mtakatifu Paulo Mtume katika Waraka wake kwa Warumi, anawataka waamini kumtambua Mwenyezi Mungu na Kristo Yesu mteule wake, ambaye amekuwa ni chemchemi ya neema na utume, changamoto na mwaliko wa kusikiliza kwa makini sauti ya Mungu asiyeonekana, Kamwe waamini wasichanganye kiri yao ya imani na ufahamu wa mambo ya Mungu. Kwa kuamini, watu wanajaliwa kuufahamu ukweli wanaopaswa kuutafuta kwa unyenyekevu. Waamini wawe makini kufahamu kile wanaochofuata bila kutumbukia katika mtindo wa kuiga bila kufahamu kile wanachoiga. Liturujia na Ibada mbali mbali zinazoadhimishwa na Mama Kanisa ziwe ni ushuhuda wa sala na tafakari ya Neno la Mungu linaloleta mabadiliko katika maisha ya watu. Vishawishi vya Yesu Jangwani ni changamoto endelevu katika maisha na utume wa Kanisa. Watu wa Mungu wataweza kuvishinda vishawishi hivi kwa njia ya Neno la Mungu, Sala na Kufunga. Hakuna sababu ya kuogopa kwani Kristo Yesu ameushinda ulimwengu!

Mafungo ya Kiroho: Msiogope
05 March 2020, 14:24