Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma amekumbwa na maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 amelazwa Hospitali ya Agostino Gemelli, Roma. Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma amekumbwa na maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 amelazwa Hospitali ya Agostino Gemelli, Roma. 

Kardinali Angelo De Donatis akumbwa na Virusi vya Corona!

Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu Jimbo Kuu la Roma ameshambuliwa na ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona na kwa sasa amelazwa kwenye Hospitali ya Agostino Gemelli, IRCCS, Roma. Hadi kufikia tarehe 31 Machi 2020, zaidi ya Mapadre 80 na Askofu mmoja wamekwisha fariki dunia kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu, Virusi vya Corona.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwaresima ni wakati uliokubalika wa kumwilisha huruma na upendo wa Mungu kama ushuhuda wa mshikamano, kielelezo makini cha imani tendaji kwa kujiweza chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma, baada ya kufanyiwa uchunguzi wa afya yake, Jumatatu tarehe 30 Machi 2020 amegundulika kuwa ameambukizwa homa ya ugonjwa wa mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kwa sasa amelazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Mfuko wa Agostino Gemelli, IRCCS, Roma. Kardinali Angelo De Donatis anakuwa ni Kardinali wa kwanza kushambuliwa na Virusi vya Corona, COVID. Taarifa kutoka Hospitalini humo zinaonesha kwamba, kwa sasa anaendelea vyema. Wasaidizi wake wa karibu wamejiwekea karantini binafsi kama njia ya kuzuia maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID yasisambae zaidi.

Kardinali Angelo De Donatis, katika ujumbe wake kwa watu wa Mungu Jimbo Kuu la Roma anasema kwamba, hata yeye binafsi anashiriki kikamilifu katika kipindi hiki cha majaribu makubwa kwa imani na matumaini. Anapenda kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu pamoja na kuendelea kutegemea sala za watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma. Anasema, anapenda kutumia fursa hii ya kulazwa kwake Hospitalini kama njia ya kushiriki mateso na mahangaiko ya watu wengi na kwamba, anapenda kutolea sala na mahangaiko yake kwa ajili ya watu wa Mungu wanaoishi Jimbo kuu la Roma. Takwimu zinaonesha kwamba, hadi kufikia tarehe 31 Machi 2020, zaidi ya Mapadre 80 wamekwisha kufariki dunia nchini Italia. Askofu Angelo Moreshi, anasadikiwa kuwa ni Askofu wa kwanza kufariki kwa ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Wakati huo huo, Askofu Antonio Napolioni wa Jimbo Katoliki la Cremona, Italia, ambaye hivi karibuni alilazwa hospitalini kwa muda wa siku 10 kutokana na Virusi vya Corona, amepona na kurejea tena Jimboni mwake, kuendelea na shughuli za kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Anasema, katika kipindi chote alichokuwa amelazwa hospitalini, ameonja: utu, weledi, sadaka na majitoleo ya madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika sekta ya afya walivyokuwa wanachakarika usiku na mchana ili kuokoa maisha ya wagonjwa wao!

Katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, Mama Kanisa anatumia silaha zifuatazo: Kufunga na kusali; Ibada ya Misa Takatifu kwa nia mbali mbali; Tafakari ya Neno la Mungu; Matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na Ibada ya Rozari Takatifu, ili kuwajengea watu imani, matumaini na mapendo katika kipindi hiki kigumu cha historia ya mwanadamu sanjari na kukimbilia: huruma, upendo, faraja na wokovu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Jumuiya ya Kimataifa imeingia katika Vita kuu ya Dunia isiyokuwa na mshindi, kwani kila mtu ameguswa na kutikiswa kwa namna yake. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, Ijumaa tarehe 27 Machi 2020 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican alijikita zaidi katika Injili kama ilivyoandikwa na Marko: 4:35 jinsi ambavyo Kristo Yesu alivyotuliza dhoruba kali, lakini wanafunzi wake walidhani kwamba alikuwa amelala na wala hakujali kwamba, walikuwa wanaangamia. Lakini Yesu akawakemea kwa sababu walikuwa na imani “haba kama kiatu cha raba”.

Baba Mtakatifu anasema, hata katika hali na dhoruba ya maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kuna watu wanadhani kwamba, Yesu amelala na wala hajishughulishi hata kidogo na kusahau kwamba, daima anawajali na kuwasumbukia waja wake; anawaokoa na kuwarejeshea tena imani na matumaini ya kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Hii ni changamoto ya kurejea tena kwenye mambo msingi ya imani na maisha kwa kuondokana na uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka, vita na kinzani pamoja na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Ni muda muafaka wa kufanya toba na wongofu wa ndani, kwa kuzingatia na kuambata mambo msingi katika maisha. Baba Mtakatifu anasema, ni wakati wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki zao msingi. Huu ni wakati wa kuwashukuru madaktari, wauguzi, wafanyakazi katika sekta ya afya, vikosi vya ulinzi na usalama, watu wa kujitolea, mapadre na watawa wanaoendelea kusadaka maisha yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni wakati wa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa watu wa Mungu!

Corona Roma

 

31 March 2020, 14:55