Baraza la Maaskofu Katoliki Mexico linaandaa mbinu mkakati wa kupambana na nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya jamii! Baraza la Maaskofu Katoliki Mexico linaandaa mbinu mkakati wa kupambana na nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya jamii! 

Maaskofu Katoliki Mexico: Mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia!

Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa limekubali mwaliko wa Maaskofu Katoliki Mexico, ili kuwasaidia katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa kwa kumtuma Askofu mkuu Charles J. Scicluna nchini humo kuanzia tarehe 20-27 Machi 2020. Lengo ni kulisaidia Kanisa nchini Mexico kupambana na nyanyaso hizi ambazo zimekita mizizi yake katika jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake Binafsi ya kichungaji, “Kama Mama mpendelevu” iliyochapishwa Juni, 2016, anasema nyanyaso za kijinsia ni kati ya makosa makubwa ambayo yamebainishwa barabara kwenye Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa. Baba Mtakatifu anapenda kuwahimiza viongozi wa Kanisa kuwa macho dhidi ya nyanyaso za kijinsia wanazoweza kufanyiwa watoto wadogo; anaonesha hatua zitakazochukuliwa ili kutekeleza vifungu vya Sheria ambavyo viko tayari kwenye Sheria za Kanisa Namba 193§ 1 na Sheria za Kanisa la Mashariki Namba 975§1. Mkazo hapa ni wajibu wa viongozi wa Kanisa katika kutekeleza dhamana na utume wao! Malezi na majiundo endelevu kwa Maaskofu ni mambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa.

Maaskofu wanakumbushwa kwamba, wanayo dhamana na wajibu kwa Wakleri na watawa wanaoishi na kufanya utume katika maeneo yao, kwa kuangalia utakatifu wa maisha na utume wao! Kumbe, uchaguzi wa vijana wanaotaka kuingia katika wito na maisha ya kipadre na kitawa ni muhimu sana! Maaskofu wanapaswa kufuatilia malezi na majiundo yao katika hatua mbali mbali na kwamba, Askofu anapaswa kuwa karibu zaidi na mapadre pamoja na watawa wake ili kujenga na kudumisha majadiliano katika udugu, ili aweze kuwasindikiza katika shida na mahangaiko yao, katika furaha na matarajio yao. Askofu mkuu Charles Jude Scicluna wa Jimbo kuu la Malta, ambaye pia ni Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, katika hotuba yake elekezi kwenye mkutano wa Kanisa kuhusu Ulinzi wa Watoto wadogo ndani ya Kanisa, tarehe 21 Februari 2019 aligusia kuhusu dhamana na wajibu katika mchakato wa kesi za nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuzuia vitendo hivi katika maisha na utume wa Kanisa!

Ni katika muktadha huu, Kardinali Luis Francisco Ladaria Ferrer, S.J., Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa amekubali mwaliko wa Baraza la Maaskofu Katoliki Mexico, ili kuwasaidia katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa kwa kumtuma Askofu mkuu Charles Jude Scicluna nchini humo kuanzia tarehe 20-27 Machi 2020. Lengo ni kulisaidia Kanisa nchini Mexico kupambana na nyanyaso hizi ambazo zimekita mizizi yake katika jamii, kwa kuanzia ndani ya familia, shule, michezo na maeneo ya kazi kwa kuzingatia ukweli, uwazi, uwajibikaji pamoja na kuondokana na utamaduni wa kulindana ambao kwa sasa umepitwa na wakati! Ubalozi wa Vatican nchini Mexico utatumika kwa ajili ya kukutana na watu na makundi mbali mbali yanayohitaji kupata msaada wa kitaalam ili kupambana na kashfa hii ambayo imechafua maisha na utume wa Kanisa. Haya yatakuwa ni mazungumzo ya faragha. Hivi karibuni, Baba Mtakatifu ameunda Kikosi Kazi cha kushughulikia nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Lengo kuu la Kikosi Kazi ni kuwasaidia Maaskofu na Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa.

Barua binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko “Motu proprio” ijulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia.  Katika barua hii, Baba Mtakatifu anabainisha sheria, kanuni na taratibu mpya zinazopaswa kutekelezwa pale kunapojitokeza shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Maaskofu mahalia pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume wanapaswa kuwajibika barabara. Sheria hizi zinawalazimisha wakleri na watawa kutoa taarifa pale kunapokuwepo na shutuma kama hizi. Kila Jimbo linapaswa kuwa na mfumo maalum utakaoiwezesha jamii kutoa taarifa za shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa.

Maaskofu Katoliki Mexico
03 March 2020, 14:13