Papa Francisko ameunda Jimbo Jipya la Ekwulobia, Nchini Nigeria na kumteua Askofu mstaafu Peter Ebere Okpaleke kuwa Askofu wake wa kwanza! Papa Francisko ameunda Jimbo Jipya la Ekwulobia, Nchini Nigeria na kumteua Askofu mstaafu Peter Ebere Okpaleke kuwa Askofu wake wa kwanza! 

Jimbo Jipya la Ekwulobia, kuongozwa na Askofu mstaafu Peter Ebere Okpaleke

Askofu mstaafu Peter Ebere Okpaleke wa Jimbo Katoliki Ahiara, lililoko nchini Nigeria kuwa Askofu wake wa kwanza. Jimbo Katoliki la Ekwulobia limeundwa baada ya Baba Mtakatifu kulimega Jimbo Katoliki la Awka na hivyo kuwa ni sehemu ya Jimbo kuu la Onitsha, Nigeria. Parokia ya “St. Joseph’s Catholic Church”, ndilo litakalokuwa Kanisa kuu la Kiaskofu, huko Anambra, Nigeria!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ameunda Jimbo Jipya la Ekwulobia nchini Nigeria na kumteua Askofu mstaafu Peter Ebere Okpaleke wa Jimbo Katoliki Ahiara, lililoko nchini Nigeria kuwa Askofu wake wa kwanza. Jimbo Katoliki la Ekwulobia limeundwa baada ya Baba Mtakatifu kulimega Jimbo Katoliki la Awka na hivyo kuwa ni sehemu ya Jimbo kuu la Onitsha, Nigeria. Makao makuu ya Jimbo Katoliki la Ekwulobia yatakuwa huko Anambra, Kusini Mashariki mwa Nigeria na Parokia ya “St. Joseph’s Catholic Church”, ndilo litakalokuwa Kanisa kuu la Kiaskofu. Jimbo jipya linaundwa na Parokia 82 zitakazohudumiwa na Mapadre wa Jimbo 240 wakisaidiana na Mapadre wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume 12. Kuna watawa wa kiume 14 na watawa wa kike 22. Waseminari walioko Seminari kuu ni 58 na walioko kwenye Seminari ndogo ni 276. Jimbo jipya lina Seminari ndogo moja. Limebahatika kuwa na shule za msingi 35 na shule za sekondari ni 14. Taasisi za ustawi na maendeleo ya jamii ni 3.

Itakumbukwa kwamba, Askofu Peter Ebere Okpaleke aliteuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2012, lakini hakufanikiwa kuingia na kuongoza, kufundisha wala kuwatakatifuza waamini wa Jimbo Katoliki Ahiara kutokana na mgomo baridi ulioitishwa na baadhi ya wakleri kwa madai kwamba, Kanisa lilitaka kuwakandamiza wananchi wa Ahiara. Hizi ni tuhuma ambazo hazikuwa na mashiko wala mvuto kwa ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu Jimboni humo. Baada ya kutafakari kwa kina kuhusu sakata hili, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 8 Juni 2017 akawaandikia wakleri barua ya kitume akiwataka kuonesha utii na kumkubali Askofu Peter Ebere Okpaleke wa Jimbo Katoliki Ahiara kwa maandishi katika kipindi cha siku 30 vinginevyo, wangefungiwa huduma ya kichungaji!

Wakleri wakatekeleza amri hii lakini wakaonesha kwamba, ilikuwa ni kinyume kabisa cha utashi wao! Kanisa linaheshimu na kuthamini utashi wa mtu kama mahali patakatifu sana ambapo Mwenyezi Mungu anaongea na mwanadamu kutoka katika undani wa maisha yake! Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 19 Februari 2018 akaridhia kung’atuka kutoka madarakani kwa Askofu Peter Ebere Okpaleke wa Jimbo Katoliki Ahiara. Tarehe 5 Machi 2020 Baba Mtakatifu Francisko ameunda Jimbo Jipya la Ekwulobia nchini Nigeria na kumteua Askofu mstaafu Peter Ebere Okpaleke wa Jimbo Katoliki Ahiara, lililoko nchini Nigeria kuwa Askofu wake wa kwanza! Matendo makuu ya Mungu!

Jimbio Jipya Nigeria

 

05 March 2020, 14:49