Mahubiri ya KLipindi cha Majillio kwa Mwaka 2019: Bikira Maria anapashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu! Mahubiri ya KLipindi cha Majillio kwa Mwaka 2019: Bikira Maria anapashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu! 

Mahubiri ya Kipindi cha Majilio: Bikira Maria Kupashwa Habari!

Tafakari ya kwanza imeongozwa na tema: “Malaika Gabrieli anampasha habari Maria kuwa atakuwa Mama wa Mungu”. Padre Cantalamessa amezama katika jibu la Bikira Maria: Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana: Imani kwa Mwenyezi Mungu: Umuhimu wa kufuata nyayo za Bikira Maria na kuamini kama Bikira Maria alivyo amini na kwamba, kwa hakika mwenye haki ataishi kwa imani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Padre Raniero Cantalamessa. Mhubiri wa nyumba ya Kipapa katika kipindi cha Majilio anasema, anapenda kuwaandaa waamini kuadhimisha Sherehe ya Noeli kwa mwaka 2019, wakiwa wanasindikizwa na Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa mintarafu matendo ya furaha kama yanavyotafakariwa kwenye Rozari Takatifu, muhtasari wa historia nzima ya ukombozi. “Wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye” Mt. 2:11. Hii ndiyo kauli mbiu inayoongoza tafakari za Kipindi cha Majilio kwa Mwaka huu. Ijumaa tarehe 6 Desemba 2019, tafakari yake ya kwanza imeongozwa na tema: “Malaika Gabrieli anampasha habari Maria kuwa atakuwa Mama wa Mungu”. Katika tafakari hii, Padre Cantalamessa amezama zaidi katika jibu la Bikira Maria: Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana: Imani kwa Mwenyezi Mungu: Umuhimu wa kufuata nyayo za Bikira Maria pamoja na kuamini kama Bikira Maria alivyo amini na kwamba, kwa hakika mwenye haki ataishi kwa imani.

Padre Cantalamessa amesema, Kipindi hiki cha Majilio ameamua kuwapatia upendeleo wa pekee Nabii Isaya, Yohane Mbatizaji, mtangulizi wa Masiha pamona na Bikira Maria, Mama wa Mungu. Lakini kati ya wote hawa, Bikira Maria amepewa uzito wa pekee kwani ndiye aliyeteuliwa kuwa ni Mama wa Mungu. Bikira Maria hakuadhimisha Kipindi cha Majilio, bali alikiishi kwa ukamilifu wote, lakini anaweza kuwasaidia waamini kujiandaa kwa ajili ya ujio wa Masiha anayezaliwa tena katika maisha yao. Matukio makuu katika kipindi hiki ni Bikira Maria kupashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu; Kumtembelea Elizabeti pamoja na kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Bikira Maria alipopashwa habari alijibu kwa kusema “Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana.” Malaika Gabrieli akamjuza pia matendo makuu ya Mungu aliyomtendea binamu yake Elizabeti, kiasi cha kutoka kwa haraka kwenda kumtembelea na huo ukawa ni ufunuo wa siri kubwa iliyokuwa imefichika mjini Nazareti, tukio la imani, akajiweka wazi mbele ya Mungu ili kumwezesha kuandika historia ya ukombozi kwa kukubali wito wa Mungu.

Bikira Maria akawa ni chombo cha imani kwa sababu aliamini kile alichoambiwa na Bwana. Elizabeti akamwona Bikira Maria kuwa kweli ni Mama wa Mungu, kwa sababu alikua amejaa neema “Fide plena”. Bikira Maria akawa ni Mama wa Mungu na kujiaminisha mbele ya Mungu. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa wale wote walioitwa na kupokea miito kutoka kwa Mwenyezi Mungu kama akina Nabii Yeremia na Mtakatifu Paulo Mtume. Katika muktadha huu, Bikira Maria akajikuta akizama katika upweke chanya, akatafakari kuhusu kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha yake, hali yake ya Ubikira, Sheria ya Musa na sasa ujauzito kwa njia ya Roho Mtakatifu. Hapa imani ilikuwa hatarini sana, lakini Bikira Maria akakubali kupokea yote na kujiaminisha mbele ya Mungu. Maisha yake yalikuwa hatarini kwa sababu alionekana kuwa na mimba kabla ya kufunga ndoa. Huu ni upweke ambao ungeweza kumtumbukiza katika ugonjwa wa sonona.

Bikira Maria ni shuhuda wa wale ambao hawakuona lakini, wakathubutu kuamini, tofauti kabisa na akina Thomaso, Mtume. Maandiko Mtakatifu yanamtaja Abrahamu kuwa ni mfano bora wa imani katika Agano la Kale. Lakini imani ya Bikira Maria kwa Mungu kilikuwa ni kielelezo cha haki, kwa sababu alimpenda Mungu na kujisadaka kwa furaha bila hata ya kujibakiza! Akawa amemchukua Mtoto Yesu moyoni mwake, hata kabla ya kutungwa kwake mimba. Bikira Maria alisema “Fiat” badala ya neno “Amina” yaani “na iwe hivyo”. Ikumbukwe kwamba, “Fiat” ni jibu lililokuwa linatumika katika maadhimisho ya Liturujia. “Fiat” yaani “Ndiyo” ya Bikira Maria inaonesha imani na utii kwa Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kwa Mwanaye Mpendwa Kristo Yesu katika hija ya maisha yake hapa ulimwenguni.

Padre Cantalamessa anawaalika waamini wanaounda Kanisa, kuona umuhimu wa kufuata nyayo za Bikira Maria katika imani na matumaini kama ilivyokuwa kwa Abeli, Abrahamu na Musa. Huu ni mwaliko pia kwa waamini kufufua na kuiga imani na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Bikira Maria. Kwa njia hii waamini watakuwa na uwezo wa kuzama katika Neno la Mungu, kupembua matatizo na changamoto za maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Hapa kuna haja ya kukazia umuhimu wa imani kama msingi wa matendo yote ambayo Mwenyezi Mungu anatenda kwa wale wanao mwamini Kristo Yesu katika maisha yao. Imani inamwezesha mwamini kujisadaka bila kudai malipo na kwamba, imani ndiyo inayojenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu. Kumbe kuna uhusiano wa karibu kati ya neema na imani.

Ikumbukwe kwamba, watu wanaokolewa kwa njia ya imani na kutokana na imani, Bikira Maria akapata upendeleo kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni imani ya pekee isiyokuwa na kifani na pia ni tendo la kijamii kama Mwenyezi Mungu alivyojifunua mbele yake. Anamtambua Mungu anayejifunua na kutoa ahadi kama ilivyokuwa kwa Abrahamu na kizazi chake. Hili ni fundisho kuu linaloibuliwa na Bikira Maria, Mama wa Mungu kwamba, imani inamwezesha mwamini kujiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. (Rej. Rum. 10:10). Bikira Maria aliamini kwa moyo kiasi kwamba, matendo yake yakawa ni kielelezo makini cha imani tendaji. Kumbe, imani inapaswa kumwilishwa katika maisha ya mtu binafsi pamoja na Kanisa ambamo kuna watakatifu, wafiadini na waungama imani ambao wamewatangulia watu wa Mungu mbele ya haki.

Huu ni mwaliko anasema Padre Raniero Cantalamessa kwa waamini nao kufuata mfano wa Bikira Maria katika hija ya maisha yao. Iwe ni fursa ya kupyaisha imani na kujiaminisha mbele ya Mungu kwa kukumbatia neema na uhuru kamili kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria baada ya kuambiwa kwamba, atamzaa Mwana wa Mungu. Kama ilivyokuwa kwa Maria, waamini wajifunze kusali kwa ibada na uchaji, ili waweze kuitikia wito wa Mungu bila wasi wasi wala mashaka. Ndiyo yao kama ilivyokuwa ile “Fiat” ya Bikira Maria iwe ni ushuhuda wa kiu na furaha ya Mungu nyoyoni mwao, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa upendo na amani duniani; kwa kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Padre Cantalamessa anasema, kwa hakika mwenye haki ataishi kwa imani sehemu hii inawahusu hasa wakleri, wanaopaswa kuwa ni watu wa imani, kwa sababu dhamana na utume wao si tu kwa ajili ya kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na kugawa Sakramenti pamoja na kuendelea kujisadaka kwa ajili ya kutoa huduma mbali mbali za shughuli za kichungaji, lakini kimsingi wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa imani katika matendo. Kwa njia hii wataweza kuwaongoza watu katika uhuru kumwelekea Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria. Padre anaweza kuwa ni mchungaji bora, ikiwa kama ana imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu. Vinginevyo anaweza kujikuta akiwa mtu kama “debe tupu ambalo kamwe haliachi kutika! Ushuhuda wa imani tendaji una mvuto na mashiko.

Nguvu ya mtu wa Mungu inapimwa kwa njia ya ushuhuda wa imani yake. Inasikitisha kuona kwamba, watu wanalikimbia Kanisa kutokana na ushuhuda hafifu wa baadhi ya viongozi wake, lakini cha kushanga zaidi bado watu wale wanaogelea katika dhambi na utepetevu wa moyo. Huu ni wakati wa kutangaza na kushuhudia imani kwa vitendo. Bila imani ni vigumu sana kutekeleza dhamana na nyajibu mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa. Mwishoni, Padre Raniero Cantalamessa. Mhubiri wa nyumba ya Kipapa katika kipindi cha Majilio anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumkimbilia Bikira Maria mwaminifu “Virgo fidelis” aweze kuwaombea imani, matumaini na mapendo katika kipindi hiki cha Majilio.

Cantalamessa No. 1

 

06 December 2019, 17:56