Kardinali John Henry Newman katika maisha na utume wake, alishuhudia imani yake kwa Kristo na Kanisa lake, kiasi cha kuwagusa na kuwavuta watu wengi katika majadiliano ya kiekumene. Kardinali John Henry Newman katika maisha na utume wake, alishuhudia imani yake kwa Kristo na Kanisa lake, kiasi cha kuwagusa na kuwavuta watu wengi katika majadiliano ya kiekumene. 

TAHARIRI: Mchango wa Kardinali Newman katika utume wa Kanisa!

Ni kiongozi ambaye imani yake inapata chimbuko kutoka katika taalimungu kadiri ya Mapokeo ya Kanisa Anglikani, baadaye akaongoka na kuzama katika taalimungu ya Kikatoliki, kiasi hata cha kukonga nyoyo za wapinzani wake kutokana na ujuzi na weledi wa kusimamia ukweli, uhalisia wa mambo pamoja na upya wa mawazo. Shukrani kwa Kardinali Newman kwa karama na mapaji yake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Imegota miaka 40 tangu Kanisa Katoliki lilipomtangaza kwa mara ya mwisho mwamini kutoka Uingereza kuwa Mtakatifu. Tukio la Kardinali John Henry Newman kutangazwa kuwa Mtakatifu, tarehe 13 Oktoba 2019 ni sababu ya furaha na shangwe kwa familia ya Mungu ndani nje ya Uingereza, watu wanaoguswa na kuvutwa na urithi mkubwa wa amana na tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu kutoka kwa Mtakatifu Kardinali John Henry Newman. Huyu ni kiongozi ambaye ameishi katika zama ambazo utu na heshima ya binadamu vilikuwa vinasiginwa vibaya, changamoto na mwaliko wa kutafuta na kuambata utakatifu wa maisha. Ni kiongozi aliyejipambanua katika kutetea misingi ya utu na heshima ya binadamu bila ya kulaani, akathubutu kwenda kinyume cha matakwa ya wengi, lakini hakutindikiwa na heshima wala nguvu. Ni kiongozi aliyetambua na kuthamini tofauti msingi kama mahali pa watu kukutana badala ya kubaguana!

Hivi ndiyo anavyoandika Mtoto wa Mfalme Carlo wa Uingereza katika Tahariri yake iliyochapishwa kwenye Gazeti la L’Osservatore Romano katika mkesha wa kutangazwa kwa Kardinali John Henry Newman na wenzake kuwa watakatifu. Kardinali Newman ni kati ya wataalam na mabingwa wa taalimungu katika kipindi cha kwenye Karne yak umi na tisa, kiasi cha kuthubutu kutumia akili, ujuzi na maarifa yake kujibu maswali tete kuhusu uhusiano kati ya imani na zama za mashaka na mambo ya kidunia. Ni kiongozi ambaye imani yake inapata chimbuko kutoka katika taalimungu kadiri ya Mapokeo ya Kanisa Anglikani, baadaye akaongoka na kuzama zaidi katika taalimungu ya Kikatoliki, kiasi hata cha kukonga nyoyo za wapinzani wake kutokana na ujuzi na weledi wa kusimamia ukweli, uhalisia wa mambo pamoja na upya wa mawazo.

Waamini na watu wa Mataifa anasema, Mtoto wa Mfalme Carlo wa Uingereza, wanapaswa kumshukuru Kardinali Newman kwa karama na mapaji yake ambayo yamejikita katika imani Katoliki, aliyoitolea ushuhuda sanjari na kuwashirikisha watu wengi zaidi kwa njia ya wasifu wake na utunzi wake wa Ushairi uliorembeshwa kwa muziki wa Bwana Edward Elgar anayekazia utulivu unaojikita katika tofauti. Hii ndiyo dhana ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, yaani Mungu mmoja katika Nafsi Tatu. Hii ni imani ambayo Kardinali Newman ameitangaza na kuishuhudia katika maisha. Mawazo yake yameendelea kuzitajirisha Jumuiya za waamini Wakatoliki. Ni kiongozi aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Akajikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Alibahatika kuwa na karama ya kuzungumza na kuwagusa watu katika “undani wa sakafu ya nyoyo zao” “Cor ad cor”.

Tofauti za kidini, kitamaduni na kijamii zikapata chimbuko lake katika urafiki wa ndani na Mwenyezi Mungu. Imani yake ilikuwa ya Kikatoliki kweli kweli kwani ilikita mizizi yake katika uhalisia wa maisha. Alitambua kiburi na udhaifu wake wa kibinadamu kiasi cha kujiaminisha kwenye huruma ya Mungu. Ni kiongozi ambaye ameacha kumbu kumbu ya kudumu katika maisha ya watu; wengi wao wamehisi kuchangamotishwa na mawazo yake, ibada na maisha yake ya kiroho bila kuwasahau wale wote wanaotaka kusimama kidete kutetea na kulilinda Kanisa kwa kuweka uwiano mzuri zaidi kati ya imani na uwezo wa kufikiri na kutenda. Imani ni mahali muafaka pa kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu. Enzi za Kardinali Newman, ulimwengu uligubikwa na kinzani mbali mbali na wengi wakateseka kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kardinali Newman akasimama kidete kutangaza na kushuhudia imani yake, akaonesha moyo wa urafiki na upendo kwa watu mbali mbali.

Ameacha urithi mkubwa wa machapisho yake ambayo yamekusanywa katika vitabu 30, machapisho ambayo aliwatumia si tu wasomi na watu maarufu wakati ule, bali hata watu wa kawaida waliokuwa wanatafuta kuchota busara yake. Kwa hakika alikuwa ni Jaalimu “la kutupwa” huko Oxford na Dublin ambako ameonesha maana na umuhimu wa Chuo Kikuu. Kwake, elimu ilikuwa ni haki msingi ya binadamu. Amesaidia sana mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa Anglikani na kwamba, Makanisa haya mawili yanategemeana na kukamilisha. Kituo chake cha sala, michezo na masomo ni urithi mkubwa katika mchakato wa kukuza na kuendeleza karama ya elimu na huduma ya upendo ndani na nje ya Uingereza. Kardinali Newman katika hija ya maisha yake ya kiroho aliyapenda Makanisa yote mawili, akafanya tafakari ya kina kuhusu Kanisa Anglikani na Kanisa Katoliki, akathubutu kukiri kwamba, alikuwa analiacha Kanisa Anglikani kwa machozi na uzito wa moyo.

Watu wa Mungu wanamkumbuka na kumshukuru Kardinali Newman, Mwingereza “kweli kweli” asiye na hila hata kidogo ndani mwake na Mtumishi mwaminifu wa Kanisa. Ni wakati muafaka wa kumshukuru Mungu kwa urafiki uliojengeka kati ya Makanisa haya mawili, licha ya utengano ambao bado unaonekana. Lakini, majadiliano ya kiekumene yanaendelea kuimarika siku hadi siku! Kardinali Newman ameonesha uwiano bora zaidi katika mambo ya Kimungu, changamoto iwe ni kufuata imani kwa ujasiri na uelewa, ili waamini waweze kutambua tofauti zao msingi, tayari kuendeleza hija ya majadiliano ya kiekumene, ili siku moja waweze kuwa wamoja!

Kardinali Newman

 

12 October 2019, 16:08