Vatican News
Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI: Unasaidia tafiti, ufadhili wa masomo pamoja na kuendeleza taalimungu ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa XVI, Jaalimu na shuhuda wa imani! Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI: Unasaidia tafiti, ufadhili wa masomo pamoja na kuendeleza taalimungu ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa XVI, Jaalimu na shuhuda wa imani!  (ANSA)

Mfuko wa Joseph Ratzinger katika kukuza tafiti za kitaalimungu

Mfuko wa Joseph Ratzinger, unapania kuibua na kukuza taalimungu ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwa njia ya tafiti makini za kisayansi, mikutano, warsha na makongamano ya kitaifa na kimataifa. Ni mfuko unaosaidia watafiti mbali mbali kuchapisha kazi zao pamoja na kutoa udhamini kwa wanafunzi wanaotaka kujizatiti zaidi katika taalimungu ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Padre Federico Lombardi, SJ., Rais wa Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI, ulioanzishwa rasmi tarehe 1 Machi 2010 na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anasema, Mfuko huu unapania pamoja na mambo mengine kuibua na kukuza taalimungu ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwa njia ya tafiti makini za kisayansi, mikutano, warsha na makongamano ya kitaifa na kimataifa. Ni mfuko unaosaidia watafiti mbali mbali kuchapisha kazi zao pamoja na kutoa udhamini kwa wanafunzi wanaotaka kujizatiti zaidi katika taalimungu ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, ambaye katika maisha na utume wake wote ameendelea kujipambanua kuwa ni shuhuda wa imani thabiti ya Kanisa Katoliki. Kila mwaka, Mfuko huu unatoa tuzo kwa washindi katika nyanja mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa.

Padre Lombardi anasema, kati ya tarehe 8-9 Oktoba 2019 wa Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI, uliadhimisha Kongamano la Kimataifa huko Budapest, nchini Hungaria kwa kushirikiana na Kitivo cha Taalimungu cha Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Pazmany Peter  pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Hungaria. Kongamano hili limewashirikisha viongozi wa Kanisa, Serikali ya Hungaria, Wasomi na Wanazuoni kutoka ndani na nje ya Hungaria. Washiriki wa Kongamano hili pamoja na mambo mengine wamepembua kuhusu: Kuporomoka kwa Ukomonisti, mabadiliko ya kisiasa Ulaya ya Kati; Dhamana na wajibu wa Kanisa; Mwelekeo mpya wa uchumi kimataifa. Utaifishaji wa mali za Kanisa, Rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma; wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; pamoja na matamanio halali ya vijana wa Ulaya

Kardinali Peter Erdo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Esztergorm-Budapest katika hotuba yake elekezi, amepembua kuhusu: kuporomoka kwa Ukomunisti Barani Ulaya, mabadiliko ya kisiasa Ulaya ya Kati na dhamana na utume wa Kanisa kati ya mwaka 1989 hadi mwaka 2019 katika muktadha huu. Kumekuwepo na uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu tangu kuanguka kwa Ukomunisti. Demokrasia imekuwa na kupanuka kwa wananchi kuwa na wawakilishi wao Bungeni. Mabadiliko ya kisiasa yamefanyika kwa amani na utulivu, hata kama hapa na pale kumekuwepo na baadhi ya watu kutaka kulipiza kisasi kutokana na dhuluma walizokumbana nazo wakati wa utawala wa Kikomunisti.

Chaguzi mbali mbali za kisiasa zimefanyika kwa kujikita katika haki, ukweli na uwazi. Lakini kwa bahati mbaya, rushwa, wizi na ubadhirifu wa mali ya umma, umepekea kuongezeka kwa deni kubwa la ndani na nje kwa mataifa mwengi ya Ulaya ya Kati; ukosefu wa fursa za ajira pamoja na kusua sua kwa ukuaji wa uchumi fungamani. Kumekuwepo na ongezeko kubwa la uhalifu wa kimataifa, biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na kukomaa kwa utumwa mamboleo. Kanisa kwa upande wake limeendelea kuwekeza katika maisha ya kiroho na kimwili, kwa kukazia uhuru wa kuabudu; ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu. Dhamana na utume wa Kanisa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii.

Nchini Hungaria mali iliyotaifishwa na Serikali ya Kikomunisti, bado haijareshwa kwa Kanisa, ingawa Mkataba uliotiwa saini kati ya Hungaria na Vatican wa Mwaka 1997 unaonesha kwamba, nusu ya mali ya Kanisa inapaswa kurejeshwa lakini utekelezaji wake bado unasua sua sana. Kwa sasa Kanisa linataka kuangalia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini kwa kukuza na kudumisha umoja na mshikamano wa watu wa Mungu; kwa kuendelea kujikita katika upatanisho wa kitaifa; majadiliano ya kidini na kiekumene katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu ndani na nje ya Hungaria. Umoja na mshikamano wa dhati ni mambo yanayofanyiwa kazi kwa sasa Wajumbe wamegusia kwa namna ya pekee kabisa mchakato wa mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiroho katika kipindi cha miaka thelathini iliyopita.

Kuyumba kwa demokrasia pamoja na “kuchanganyikiwa” kwa Wakatoliki katika masuala ya kisiasa sehemu mbali mbali za dunia. Imekuwa ni fursa ya kuangalia mwenendo wa uchumi katika nchi za Ulaya ya Kati kuanzia mwaka 1989 hadi mwaka 2019. Kuporomoka kwa Ukuta wa Berlin nchini Ujerumani na mwingiliano wa watu Barani Ulaya na jinsi ambavyo ndoto ya matumaini kwa wananchi wengi wa Ulaya ilivyoyeyuka kama “ndoto ya mchana”. Baraza la Maaskofu Katoliki Hungaria limejadili hali ya kisiasa nchini Hungaria mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumeibuka dhana ya utaifa usiokuwa na mashiko wala mvuto kwa baadhi ya wanasiasa kutafuta umaarufu, hali ambayo imezua kinzani kubwa katika Umoja wa Ulaya, changamoto inayowataka watu wa Mungu kuwajibika barabara katika kuandika historia na mustakabali wao.

Wajumbe wamezipembua changamoto hizi katika mwanga wa Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa kukazia utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, huku haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza. Wajumbe walipata nafasi pia ya kujadiliana katika makundi, ili kuwawezesha watu wengi zaidi kuchangia hoja msingi. Itakumbukwa kwamba, Mfuko wa Joseph Ratzinger/Benedikto XVI, kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha LUMSA kilichoko mjini Roma, kuanzia tarehe 15-16 Novemba 2018 waliadhimisha Kongamano la Kimataifa lililojadili kuhusu: Uhuru wa kidini, haki asilia, mabadiliko katika uhuru na utamaduni wa haki msingi za binadamu pamoja na upotoshaji wa dhana hizi katika Jumuiya ya Kimataifa!

Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI ulihitimisha shughuli zake kwa mwaka 2017 kwa kuadhimisha Kongamano la VII ambalo liliandaliwa kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Costa Rica, kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama unavyochambuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Laudato si” yaani “Sifa kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Huu ni mradi ulioachambua kwa kina na mapana changamoto ya utunzaji bora wa mazingira na maendeleo yake katika medani mbali mbali za kimataifa!

Mfuko wa Ratzinger
10 October 2019, 14:54