Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko baada ya kumteuwa mwezeshaji mkuu, makatibu maalum, sasa amewateua wajumbe watakaoshiriki katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Baba Mtakatifu Francisko baada ya kumteuwa mwezeshaji mkuu, makatibu maalum, sasa amewateua wajumbe watakaoshiriki katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia.  (Vatican Media)

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Wajumbe wa Sinodi

Bara la Afrika katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, itawakilishwa na: Kardinali mteule Fridolin BESUNGU; Askofu mkuu Marcel MADILA BASANGUKA, wa Jimbo kuu la Kananga. Wengine ni Padre Martín LASARTE TOPOLANSKI, S.D.B. kutoka Angola; Sr. Mary Agnes Njeri MWANGI wa Shirika la Masista wa Consolata pamoja na Padre Rigobert MINANI, S.I. Wajumbe!

Na Padre Richard A.  Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia yatafanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 6-27 Oktoba 2019 kwa kuongozwa na kauli mbiu "Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani". Tangu mwanzo, Mababa wa Sinodi wamekazia umuhimu wa: kuona, kung'amua na kutenda! Ni Sinodi itakayopembua tema mbali mbali:kuhusu: haki jamii, malezi awali na endelevu, katekesi, liturujia na utambulisho wa Kanisa katika Ukanda wa Amazonia unaoziunganisha nchi tisa ambazo ni: Bolivia, Brazil, Colombia, Equador, Perù, Venezuela, Suriname na Guyana. Hatua zote za maandalizi tayari zimekwisha kutekelezwa. Baba Mtakatifu Francisko ndiye mhusika mkuu katika maadhimisho haya akisaidiwa kwa karibu sana na Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu. Ili kufaninikisha maadhimisho haya, Baba Mtakatifu amemteua: Kardinali Claudio Hummes kuwa Mwezeshaji mkuu wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia pamoja na Askofu David M. De Aguirre Guinea Kardinali mteule Michael Czerny, kuwa Makatibu maalum wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia.

Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko amewateuwa: Kardinali Baltazar Enrique Porras Cardozo, Askofu Mkuu wa  Jimbo Kuu la Mérida (Venezuela); Kardinali Pedro Ricardo Barreto Jimeno, Askofu mkuu Jimbo kuu la Huancayo (Perù) Kardinali João Braz de Aviz, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kuwa Marais wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Baba Mtakatifu amekamilisha Orodha ya wajumbe wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia itakayokuwa na wajumbe 185. Wajumbe ni kutoka Tume ya Mawasiliano, Tume ya Utata, REPAM, Wawakilishi wa Majimbo Makuu ya Nchi za Ukanda wa Amazonia, Viongozi wakuu wa Mabaraza ya Kipapa. Katika orodha hii, kuna wajumbe walioteuliwa moja kwa moja na Baba Mtakatifu. Kuna wawakilishi kutoka Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume. Kuna wajumbe walioteuliwa kwa ajili ya maandalizi ya Sinodi; washiriki maalum, yaani wataalam.

Baba Mtakatifu pia amewateua baadhi ya wakleri, watawa na waamini walei kuwa ni wasikilizaji. Kuna Makatibu wakuu wa Sinodi za Maaskofu, Wajumbe wa dini na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo pamoja na wageni maalum na kati yao kuna Dr. Ban Moon, Katibu mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa. Bara la Afrika katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, itawakilishwa na: Kardinali mteule Fridolin AMBONGO BESUNGU wa Jimbo kuu la Kinshasa, DRC; Askofu mkuu Marcel MADILA BASANGUKA, wa Jimbo kuu la Kananga, nchini Congo Brazzaville  na ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika ya Kati, A.C.E.A.C. Wengine ni Padre Martín LASARTE TOPOLANSKI, S.D.B. kutoka Angola; Sr. Mary Agnes Njeri MWANGI wa Shirika la Masista wa Consolata pamoja na Padre Rigobert MINANI, S.I., kutoka DRC., Mratibu wa “Réseu Ecclesial du Bassin du Congo” [REBAC].

Hati ya Kutendea Kazi: “Instrumentum Laboris” imepitishwa hivi karibuni na Wajumbe Washauri wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Hati hii imegawanyika katika Sehemu Kuu III, kwa kuwa na utangulizi pamoja na hitimisho lake. Sehemu ya kwanza inapembua kuhusu Sauti kutoka Amazonia kwa kujikita katika: Maisha, Ukanda wa Amazonia, Nyakati na Majadiliano. Sehemu ya Pili ni kuhusu Ekolojia fungamani:Kilio cha Dunia Mama na Kilio cha maskini. Hapa wanaangaliwa watu mahalia waliojitenga, wahamiaji, ukuaji wa miji; familia na jumuiya za watu, rushwa na ufisadi; afya fungamani, elimu makini na wongofu wa kiekolojia. Sehemu ya Tatu: Kanisa Sauti ya Kinabii Ukanda wa Amazonia: Changamoto na matumaini. Sura ya Kanisa na Umisionari Ukanda wa Amazonia; changamoto za utamadunisho; maadhimisho ya fumbo la imani na liturujia iliyotamadunishwa. Muundo wa jumuiya; Uinjilishaji mijini; Majadiliano ya kidini na kiekumene pamoja na utume wa vyombo vya mawasiliano ya jamii. Utume wa kinabii wa Kanisa pamoja na mkakati wa maendeleo fungamani ya binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume huko Amerika ya Kusini hivi karibuni alisikitika kusema kwamba, ukoloni mamboleo unaojikita katika nguvu ya kiuchumi: kwa uchimbaji wa mafuta na gesi asilia; kilimo cha mashamba makubwa ili kukidhi mahitaji ya mali ghafi ya viwanda; ni mambo yanayotishia usalama, maisha, ustawi na maendeleo ya Ukanda wa Amazonia. Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kuwa karibu zaidi na wakleri wao; kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya Kiinjili ili kupambana na saratani ya rushwa, ufisadi na kumong'onyoka kwa haki msingi, utu na heshima ya binadamu na kwamba, Maaskofu wathamini majadiliano katika ukweli na uwazi.

Sinodi Amazonia

 

21 September 2019, 15:44