Vatican inafuatilia kwa makini sana kuhusu suala  la haki ya kisiasa -jamii nchini Nicaragua.Vile vile Maaskofu wanaomba waamini wasali kwa ajili ya amani. Vatican inafuatilia kwa makini sana kuhusu suala la haki ya kisiasa -jamii nchini Nicaragua.Vile vile Maaskofu wanaomba waamini wasali kwa ajili ya amani. 

Askofu Mkuu Jurkovic:Suluhisho la haki nchini Nicaragua lipatikane haraka!

Katika Kikao cha 42 cha Baraza la Haki za kibinadamu,kilichofanyika mjini Geneva tarehe 10 Septemba 2019 kuhusu mada ya hali ya Nicaragua,Askofu Mkuu Jurkovic Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika ofisi za Umoja wa Mataifa iliyoko Geneva,amesisitizia juu ya kupata suluhisho la haki na amani kwa haraka kwa kuzingatia misingi daima ya haki za kibinadamu na haki za nchi mahalia.

Na Padre Angelo Shikombe – Vatican

Askofu mkuu Ivan Jurkovic  mwakilishi wa kudumu wa Vatican katika ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva nchini Uswis  ameungana na sauti ya pamoja ya Umoja wa Mataifa wakiomba majadiliano  ya  haki nchini Nicaragua. Akimwelekeza Rais Michelle Bachelet, Rais wa Tume ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Haki za binadamu katika hotuba yake, Jumanne tarehe 10 Septemba 2019 kwa kuongozwa na mada ya Haki ya Nicaragua kwenye Mkutano wa 42 wa Baraza la Haki msingi za kibinadamu. Askofu Mkuu amesema, Vatican inafuatilia kuhusu suala la haki  msingi za binadamu na kwa maana hiyo kuhusu migogoro ambayo haikuweza kupata suluhisho hadi sasa, lazima itatuliwe kwa haraka hasa kwa kuzingatia kuheshimu misingi daima ya haki za kibinadamu na misingi iliyo kubaliwa na Katiba ya Nchi. Ni lazima  kushughulikia migogoro na vurugu zinazoendelea katika Nchi ya Niacagua ambazo zinahatarisha ustawi wa maisha ya watu wake. Aidha katika hotuba yake Askofu Mkuu Jurkovik ameonesha mtazamo wake kuwa amani ya nchi ya Nicaragua itapatikana katika majadiliano na maridhiano kati ya pande zinazokinzana.

Askofu Mkuu Jurkovic amesema machafuko na vurugu zinazoendelea Nchini Nikaragua zinafahamika, hivyo hali hiyo yenye kuhatarisha maisha ya wengi inahitaji suluhu ndani muda mfupi ili kuokoa uhai wa watu nchini humo. Katika kuimarisha umoja wananchi kunahitajika kuzingatia  haki za binadamu  pamoja na kusimamia katiba ya nchi yao.  Ili waweze kufikia umoja huo, nchi inahitaji kujengewa msingi imara wa kikatiba kwa ajili ya kulinda haki za watu na kuwapatia watu fursa ya kujiandalia maisha yao ya badaye.  Mwakilishi huyo wa Baba Mtakatifu amesema, Mamlaka za Kitume za Baba Mtakaifu zingependekeza kuondoa tofauti zilizopo kati ya Serikali na wadau wake ili kuweza kuhuisha roho ya uwajibikaji na upatanisho. Katika hali kama hiyo ukweli unapaswa kuheshimiwa ili kuweza kuweka misingi ya haki na amani kwa ajili ya manufaa ya wote.

Akiendelea kufafanua hoja yake, Askofu Ivan Jurkovic amesema, Taasisi za Kanisa  zinasadiki kabisa kuwa mifarakano katika jamii kamwe haitaweza kutatuliwa kwa njia za mabavu, bali inaweza kutatuliwa kwa njia za majadiliano na maridhiano yanayofikiwa na pande zote mbili zinazokinzana. Hivyo, majadilianao yaliyokwisha fanyika na makubaliano yaliyofikiwa mnamo Machi 2018 yanatoa mwelekeo wa kuingia katika kipindi cha uchaguzi kwa njia ya amani na uwazi mkubwa. Aidha maboresho katika taratibu za uchaguzi lazima yawezeshe uchaguzi kuwa huru na wazi hata kwa watazamaji kutoka Jumuiya ya kimataifa.  

Ikumbukwe nchi ya  Nicaragua ni taifa la Amerika ya kati, lililopakana na bahari ya Karibia na bahari ya Pasifiki kati ya Costa Rica na Honduras.  Nchi ya Nicaragua ina idadi ya watu takriban milioni 5.4. Tangu uchaguzi wa kidemokrasia uliofanyika mnamo mwaka 1990, Nicaragua imepitia mageuzi ya uchumi wa soko ikafanikiwa  kufanya uchaguzi wa wazi na wa haki, na ilifanya kazi katika kujenga taasisi za demokrasia, japokuwa kadiri ya miaka ilivyokwenda mbele kumekuwapo na mabadiliko mengi sana ya kisiasa na kijamii .

Hata hivyo hivi karibuni Maaskofu wametangaza  kuanza wiki ya kuombea haki na amani nchini mwao kuanzia tarehe 8-15 Septemba 2019. Baraza la Maaskofu katoliki nchini humo limewaomba waamini wake kuombea haki na amani kufuatia na matarajio ya maadhimisho ya siku ya uhuru itakayofikia kilele chake siku ya Dominika tarehe 15 Septemba 2019. Kwa hakika nchi ya Nicaragua inaishi kipeo kikubwa cha kisiasa na kijamii ambapo ni jukumu la wote kuombea, ili  hiyo haki na amani iweze kutawala. Soma zaidi: https://www.vaticannews.va/sw/church/news/2019-09/nicaragua-maaskofu-kutangaza-wiki-ya-maombi-ya-amani-na-haki.html

NICARAGUA
11 September 2019, 16:03