Askofu mkuu Bernardito Auza: Palipo na haki na majadiliano ya dhati, hapo amani huchanua na kustawi kama mtende wa Lebanon Askofu mkuu Bernardito Auza: Palipo na haki na majadiliano ya dhati, hapo amani huchanua na kustawi kama mtende wa Lebanon 

Wasanii ni wajenzi wa utamaduni wa majadiliano & amani duniani!

Askofu mkuu Bernardito Auza, amekiri kuwa siyo waamini wote wanaishi vizuri hata hivyo, wito wake kila mmoja anapaswa kuwa mjenzi wa amani. Amani, utamadunisho na majadiliano ya kiekumene yana uhusiano wa karibu sana kwani yana mzizi mmoja na yanakua kwa pamoja. Palipo na haki pamoja na majadiliano ya dhati daima amani hustawi kwa ajili ya mafao ya wengi.

Na Padre Angelo Shikombe, - Vatican.

Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, hivi karibuni amewaomba wasanii kutumia kipaji chao cha usanii kwa ajili ya kuleta amani na kuimarisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Askofu mkuu Bernardito Auza ameyasema hayo katika mkutano wa majadiliano ya kijamii juu ya utamaduni wa amani uliofanyika hivi karibuni huko New York, Marekani. Akitoa hoja yake katika mjadala huo Askofu mkuu Auza amesema, wasanii wana nafasi muhimu katika jamii ya kuweza kuleta tofauti ya fikra katika kuboresha utamaduni wa amani ndani ya jamii wanamoishi. Akifafanua hoja yake Askofu mkuu Auza amesema, wasanii wamejaliwa karama ya kujenga amani kutokana na kazi zao zinazopokelewa na jamii kwa moyo wote. Neno amani yaani “shalom” kutoka kwa lugha ya Kiebrania au neno “salaam” kutoka kwa lugha ya kiarabu linatumika katika salaam ya kila siku likimaanisha kuwepo kwa muafaka kamili, maendeleo na utulivu wa kweli.

Kwa hiyo kutokana na kazi zao wanalazimika kujibidiisha na ujenzi wa amani. Askofu mkuu amewakumbusha kuwa katika maisha yao wanapaswa kukuza utamaduni wa majadiliano na mahusiano chanya katika jamii zao ili kuweza kuinusuru hali ya amani inayosongwa na vurugu za aina mbalimbali. Ili waweze kutekeleza hayo, wanatakiwa kuachana na udhalimu pamoja na mifumo yake yote ya unyanyasaji, ukandamizaji na ubaguzi. Sanaa zao zijenge mtazamo wa kumwona kila mtu kuwa ni ndugu na siyo adui. Kwa mtazamo huo jamii moja haitajiona kuwa bora kuliko jamii nyingine. Udugu ndicho kiunganishi cha jamii kiasi kwamba, kinapokosekana amani inatoweka. Wasanii wanaojua kazi yao vizuri ni kioo cha jamii na hivyo wasisite kuwashirikisha wengine upendo, uzoefu, na furaha yao. Watambue kwamba, kazi hiyo ya usanii inafungamana na ukuzaji wa mchakato wa majadiliano. Katika ulimwengu unaotishwa kwa hofu ya vitendo vya  kigaidi, mifarakano na nyanyaso; amani hutupwa mbali, na watu hukosa matumaini ya kupata furaha tena. Wasanii wa dini mbali mbali wanaalikwa kuendelea kutetea amani ulimwenguni kwa  mafao ya wengi.

Zaidi ya hayo Askofu mkuu Auza amekazia kuwa matendo ndiyo lugha iliyo na nguvu zaidi kuliko maneno. Askofu mkuu amekiri kuwa siyo watu wote wanaoipokea dini wameishi vizuri hata hivyo kwa wito wake kila mmoja anapaswa kuwa mjenzi wa amani. Amani, utamadunisho na majadiliano ya kiekumene yana uhusiano wa karibu sana kwani yana mzizi mmoja na yanakua kwa pamoja. Palipo na haki pamoja na majadiliano ya dhati daima amani hustawi. Kama Baba Mtakatifu Francisko na Hati ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa sahihi kati yake na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini Misri wakieneza utamaduni wa kuheshimiana na kuchukuliana ili kupambana na matatizo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, vivyo hivyo na jamii ya wasanii inavyoweza kuleta mabadiliko makubwa katika jamii. Kama kila mmoja akichukua hatua ya kujenga amani katika jamii anayoishi huenda ulimwengu wote ukafurahia matunda ya amani.

Askofu mkuu Auza

 

16 September 2019, 13:53