Baraza la Maaskofu Katoliki Cuba kuanzia tarehe 1-4 Agosti 2019 linaadhimisha Siku ya Vijana Kitaifa nchini Cuba. Baraza la Maaskofu Katoliki Cuba kuanzia tarehe 1-4 Agosti 2019 linaadhimisha Siku ya Vijana Kitaifa nchini Cuba. 

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya Vijana Kitaifa Cuba, 2019

Papa Francisko anapenda kuwatia shime, vijana wote kufuata nyayo na mfano wa Bikira Maria, Mtumishi mwaminifu wa Bwana, ili kuonja furaha inayobubujika baada ya kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao. Vijana wawe ni mashuhuda wa Kristo Mfufuka; kwa kumwachia nafasi ili awaletee mageuzi makubwa katika maisha yao; ili vijana wawe kwelii ni wafuasi wamisionari.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kitaifa nchini Cuba kuanzia tarehe 1 – 4 Agosti 2019 yanaongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema” Lk. 1: 38. Hili ni tukio muhimu sana, linaloacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za vijana wengi wanaohudhuria. Hili ni jukwaa lenye utajiri mkubwa wa tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii. Hiki ni kipindi cha neema na changamoto kwa vijana kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili duniani licha ya changamoto na vikwazo wanavyoendelea kupambana navyo katika maisha na wito wao. Baba Francisko katika Wosia wake Kitume “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi”, anawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya!

Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Wosia huu ni amana na utajiri unaobubujika kutoka katika mchakato mzima wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, iliyoadhimishwa mwezi Oktoba 2018, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Mang’amuzi na Miito”. Baba Mtakatifu katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Dionisio García Ibáñez wa Jimbo kuu la Santiago ya Cuba, anapenda kuwatia shime, vijana wote wanaohudhuria maadhimisho haya kufuata nyayo na mfano wa Bikira Maria, Mtumishi mwaminifu wa Bwana, ili kuonja furaha inayobubujika baada ya kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Kristo Mfufuka; kwa kumwachia nafasi ili aweze kuleta mageuzi makubwa katika maisha yao, ili kweli waweze kuwa ni wafuasi wamisionari.

Iwe ni fursa kwa vijana kugundua uwepo endelevu wa Kristo Yesu katika maisha yao; wajitahidi kusikiliza kwa makini, wito na mwaliko wake; waendelee kukua na kukomaa katika urafiki unaofumbatwa katika sala, tafakari ya Neno la Mungu, maisha ya Kisakramenti na matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha imani tendaji. Kwa njia hii, vijana wataendelea kupeta kwani maisha yao yatakuwa yamesimikwa katika uaminifu na huruma inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake! Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuchukua nafasi hii kuwakumbuka na kuwaombea vijana wote nchini Cuba pamoja na kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa upendo wa Cobre. Mama huyu mwema, awasindikize vijana wa Cuba hatua kwa hatua katika maisha yao na mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko kwa furaha kubwa anapenda kutoa baraka zake za kitume.

Wakati huo huo Askofu mkuu Dionisio García Ibáñez wa Jimbo kuu la Santiago ya Cuba, katika barua yake kwa Maaskofu wa majimbo mbali mbali ya Kanisa Katoliki nchini Cuba, anasema, maadhimisho ya Siku ya Vijana Kitaifa nchini Cuba ingekuwa ni fursa ya kukutana, kusikiliza shuhuda na hatimaye, kuadhimisha Imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, sehemu mbali mbali za Cuba, lakini mambo yamebadilika. Hii ni kutokana na kuchechemea kwa uchumi, gharama ya maisha kupanda wakati hali ya maisha ikiendelea kudidimia;  sanjari na hofu ya ulinzi na usalama wa vijana. Kumbe, maadhimisho haya kitaifa yanafanyikia kwenye eneo la Jimbo kuu la Santiago ya Cuba pamoja na maeneo ya Majimbo husika bila kwenda nje ya viunga vya Kanisa.

Askofu mkuu Dionisio García Ibáñez anasema, hii ni ndoto ambayo imefutika “ghafla bin vu”, kwani malengo ya awali yalikuwa ni kuwawezesha vijana kuadhimisha Siku ya Vijana Kitaifa katika maeneo makuu kumi na mmoja. Kwa sasa hii inakuwa pia ni changamoto katika maisha na utume wa Kanisa, inayopaswa kuvaliwa njuga kwa siku za usoni. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kitaifa nchini Cuba yanalenga kuhamasisha ari na moyo wa kimisionari miongoni mwa vijana, ili waweze kuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Serikali pia imekataza maadhimisho ya Njia ya Msalaba na hija kuelekea kwenye Madhabahu ya Bikira Maria, Mama wa upendo wa Cobre.

Vijana Cuba
02 August 2019, 12:13