Vatican News
UNESCO: Kanisa kuu la Notre Dame, Jimbo kuu la Paris, Ufaransa ni amana, utajiri na urithi wa maisha ya kiroho na kitamaduni; uzuri na utambulisho wake viendelezwe! UNESCO: Kanisa kuu la Notre Dame, Jimbo kuu la Paris, Ufaransa ni amana, utajiri na urithi wa maisha ya kiroho na kitamaduni; uzuri na utambulisho wake viendelezwe!  (AFP or licensors)

Kanisa kuu la Notre Dame: Utajiri na amana: Kiroho na kitamaduni

UNESCO katika mkutano wake 43 uliofanyika mjini Baku, umekazia: umuhimu wa kuendeleza uzuri na utambulisho wa Kanisa kuu la Notre Dame, Jimbo kuu la Paris, nchini Ufaransa, kama sehemu ya urithi wa asili na utamaduni. Kanisa hili ni utambulisho wa kitamaduni, unaowaunganisha watu mbali mbali katika imani, kama kielelezo cha uwepo wa Mwenyezi Mungu kati ya watu wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Askofu mkuu Michel Aupetit wa Jimbo kuu la Paris Ufaransa wakati Kanisa kuu la Notre Dame lilipoteketea kwa moto alisema kwamba,  anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake. Kanisa kuu la Notre Dame ni kielelezo na utambulisho wa wananchi wa Ufaransa katika umoja na utofauti wao! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, baada ya ukarabati, Kanisa kuu la Notre Dame litaendelea kuwa nyumba ya wote, alama ya imani, amana na utajiri wa kihistoria na maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu alisema, huu ni utajiri wa familia ya Mungu nchini Ufaransa, lakini pia ni kito cha thamani na amana kwa ajili ya binadamu wote! Janga hili la moto limesababisha uharibifu mkubwa katika Kanisa hili la kihistoria!

Moto umetikisa alama na utambulisho wa wananchi wa Ufaransa unaofumbatwa katika umoja na tofauti zao. Kanisa kuu la Notre Dame, ni kito cha thamani, mahali pa watu kukutana katika matukio mbali mbali. Kanisa hili limekuwa ni ushuhuda wa imani na mahali pa sala kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Paris, Ufaransa. Maneno yanayotia shime na matumaini mapya kwa familia ya Mungu nchini Ufaransa, hivi karibuni yamerudiwa tena na Monsinyo Francesco Follo, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO katika mkutano wake 43 uliofanyika huko mjini Baku, Azerbaigian. Katika hotuba yake amekazia umuhimu wa kuendeleza uzuri na utambulisho wa Kanisa kuu la Notre Dame, Jimbo kuu la Paris, nchini Ufaransa, kama sehemu ya urithi wa asili na utamaduni.

Kanisa hili ni utambulisho wa kitamaduni, unaowaunganisha watu mbali mbali katika imani, kama kielelezo cha uwepo wa Mwenyezi Mungu kati ya watu wake. Kumbe, juhudi zote za kukarabati Kanisa kuu la Notre Dame, hazina budi kuzingatia uzuri wake wa asili na utambulisho wake unaochota amana na utajiri katika maisha ya kiroho. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, waamini wanapata mahali pa kuabudu na kuadhimisha Mafumbo Matakatifu, yaani mahali ambapo Liturujia inaadhimishwa. Mama Kanisa anatamani sana kuona kwamba,  waamini wote wanaongozwa kwenye kuyashiriki maadhimisho ya Liturujia kwa utimilifu, kwa ufahamu na utendaji! Hii ndiyo tabia ya Liturujia na kwa sababu ya Sakramenti ya Ubatizo, ni haki na wajibu wa waamini ambao kimsingi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki wa Mungu.

Liturujia ni chemchemi ya roho ya kweli ya kikristo. Liturujia inaimarisha nguvu za waamini kumtangaza  na kumshuhudia Kristo. Lengo ni umoja na mshikamano wa watoto wa Kanisa. Liturujia ni muhimu kwa ajili ya kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa kwa njia ya Kristo Yesu. Liturujia ni utekelezaji wa kazi ya Kikuhani ya Kristo Yesu. Hii ni changamoto pevu katika utekelezaji wa mradi wa ukarabati wa Kanisa kuu la Notre Dame, Jimbo kuu la Paris, nchini Ufaransa.Waamini wanataka kurejea tena na kuendelea na maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa ndani ya Kanisa kuu la Notre Dame. Hili ni Kanisa ambalo ni amana na utajiri mkubwa wa kitamaduni, lakini pia ni kielelezo na ushuhuda wa imani kwa wale waliolijenga. Ni matumaini ya Vatican kwamba, ukarabati wa Kanisa kuu la Notre Dame, utafanywa kwa ufundi mkubwa, ili hatimaye, amana na utajiri huu, uweze kurejeshwa tena mikononi mwa waamini na hata kwa wale wasioamini. Ni utajiri wa kitamaduni, lakini unabeba uzito mkubwa kama alama na ushuhuda wa imani ya Kanisa kwa Kristo na Kanisa lake!

UNESCO: Notre Dame
10 July 2019, 16:06