Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina laanza hija ya kitume kwa kukutana na Baba Mtakatifu Francisko, 2 Mei 2019. Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina laanza hija ya kitume kwa kukutana na Baba Mtakatifu Francisko, 2 Mei 2019. 

Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina laanza hija ya kitume!

Kundi la kwanza la Maaskofu kutoka Argentina limekutana na Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 2 Mei 2019, Kundi la Pili, itakuwa ni tarehe 10 Mei na Kundi la tatu ni hapo tarehe 16 Mei 2019. Kardinali Mario Aurelio Poli ndiye Rais wa Baraza.Itakumbukwa kwamba, Kanisa Katoliki nchini Argentina linaundwa na Majimbo makuu 14 yaliyogawanyika katika Majimbo 48. Majimbo mawili ni ya kijeshi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina limeanza hija ya kitume inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na waandamizi wake kuu. Kundi la kwanza la Maaskofu kutoka Argentina limekutana na Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 2 Mei 2019, Kundi la Pili, itakuwa ni tarehe 10 Mei na Kundi la tatu ni hapo tarehe 16 Mei 2019. Kardinali Mario Aurelio Poli ndiye Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina. Itakumbukwa kwamba, Kanisa Katoliki nchini Argentina linaundwa na Majimbo makuu 14 yaliyogawanyika katika Majimbo 48. Kuna Majimbo mawili ya kijeshi nchini Argentina.

Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina, linafanya hija ya kitume mjini Vatican, baada ya Kanisa kuwatangaza: Askofu Enrique Angel Angelelli, Mtawa Carlos de Dios Murias, Padre Gabriel Longueville pamoja na Wenceslao Pedernera, Katekista na Baba wa familia, kuwa Wenyeheri. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hawa ni mashuhuda wa imani, walioteseka kwa sababu ya haki na upendo wa Kiinjili. Mfano na sala zao, ziwatie shime wale wote wanaoendelea kujisadaka, ili kweli dunia iweze kusimikwa katika misingi ya haki na mshikamano.

Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina, tangu mwaka 1983 demokrasia iliporejea tena nchini humo, limeendelea kusimama kidete kulinda, kutangaza na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Mafundisho Jamii ya Kanisa yamekuwa ni dira na mwongozo katika mapambano dhidi ya umaskini, hali mbaya ya uchumi; biashara ya binadamu na viungo vya vyake, mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo, kazi za suluba kwenye migodi na mashamba makubwa makubwa! Daima Maaskofu wamekazia: utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Maaskofu wameendelea kuhakikisha kwamba, Kanisa linaunda mazingira salama kwa malezi na makuzi ya watoto kwa kupambana kufa na kupona na vitendo vya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina limeandaa Mwongozo unaopaswa kufuatwa ikiwa kama kutajitokeza kashfa ya nyanyaso za kijinsia nchini humo. Umoja na upatanisho wa kitaifa; haki msingi za binadamu; Usawa; majadiliano ya kisiasa na kitamaduni; ukweli, haki, amani, huruma na upendo ni kati ya mada ambazo zimekuwa zikijadiliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina, ili kuimarisha imani, matumaini na mapendo ya familia ya Mungu nchini humo.

Maaskofu wameendelea kukazia umuhimu wa familia ya Mungu nchini Argentina kujikita katika kanuni maadili na utu wema, kwa kukataa kishawishi cha kutumbukizwa katika biashara haramu, matumizi na usambazaji wa dawa za kulevya. Wamekuwa pia wakitoa dir ana mwongozo wa kufuata katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI; Umuhimu wa kukuza na kudumisha maisha ya ndoa na familia, kadiri ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu! Yote haya ni mambo msingi yanayofumbatwa katika imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kumbe, changamoto ya uinjilishaji mpya inayofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko ni kati ya vipaumbele vinavyofanyiwa kazi nchini Argentina.

Mambo mengine ni Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo na kwamba, huruma, upendo na furaha ya Injili ni kati mambo msingi yaliyobainishwa kwenye Sera na Mikakati ya shughuli za kichungaji nchini Argentina kati ya Mwaka 2015- 2017. Mwongozo wa Mwaka 2017- 2021 ni kutangaza na kushuhudia Injili, maisha ndani ya Kanisa pamoja na kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote.

Papa: Argentina
02 May 2019, 15:33