Vatican News
Ijumaa Kuu 2019: tafakari ya Njia ya Msalaba: Sr. Eugenia Bonetti: Biashara ya binadamu na mifumo ya utumwa mamboleo! Ijumaa Kuu 2019: tafakari ya Njia ya Msalaba: Sr. Eugenia Bonetti: Biashara ya binadamu na mifumo ya utumwa mamboleo!  (Vatican Media)

Ijumaa kuu 2019: Tafakari ya Njia ya Msalaba: Colosseo Roma

Kauli mbiu ya tafakari hii ni “Pamoja na Kristo na Wanawake kwenye Njia ya Msalaba". Ni tafakari inayogusa waathirika wa biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Ni wanawake wanaotumbukizwa katika biashara na utalii wa ngono; wanaolazimishwa kuzihama na kuzikimbia nchi zao kwa ahadi hewa! Muhimu: Utu, heshima ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

IJUMAA KUU, 19 Aprili 2019 ni kumbu kumbu ya mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Baba Mtakatifu Francisko, anatarajiwa kuanzia saa 11:00 jioni majira ya saa za Ulaya kuongoza Ibada ya Liturujia ya Neno la Mungu, Kuabudu Msalaba pamoja na Ibada ya Komunio Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

NJIA YA MSALABA: Kuanzia saa 3:15 Usiku kwa saa za Ulaya, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Njia ya Msalaba, mwishoni atatoa neno na kuwapatia waamini baraka zake za kitume. Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo yaliyoko mjini Roma, Ijumaa kuu, Kanisa linapofanya kumbukumbu ya mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani, kwa mwaka 2019, imeandaliwa na Sr. Eugenia Bonetti wa Shirika la Consolata ambaye pia ni Rais wa Chama cha Kiraia “Slaves No More”. Kiini cha tafakari hii ni mateso, nyanyaso na dhuluma zinazojitokeza katika biashara ya binadamu na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo.

Sr. Eugenia Bonetti anasema, kauli mbiu ya tafakari hii ni “Pamoja na Kristo na Wanawake kwenye Njia ya Msalaba” yenye Vituo 14 kadiri ya Mapokeo ya Kanisa Katoliki. Ni tafakari inayogusa waathirika wa biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Hawa ni wanawake wanaotumbukizwa katika biashara na utalii wa ngono; wanaolazimishwa kuzihama na kuzikimbia nchi zao kwa ahadi hewa! Yote hii ni Misalaba inayopaswa kuamsha tena dhamiri za watu ili kusimama kidete kupambana na biashara ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo inayodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu! Haya ni matokeo ya uchoyo, ubinafsi, uchu wa mali, madaraka na tamaa ya kupata utajiri wa haraka haraka hata kama ni kwa njia mateso na mahangaiko ya watu wengine. Zote hizi ni dalili za utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Kituo cha kwanza, kinawagusa viongozi wenye dhamana na wajibu katika jamii, kuhakikisha kwamba, wanasikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kama ilivyokuwa kwa Pilato, hawa ni watu ambao wamehukumiwa adhabu ya kifo kutokana na sera na mikakati isiyojali wala kuguswa na utu, heshima na haki msingi za binadamu! Hawa ni watu ambao hawana fursa za ajira, kiasi cha kukosa matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Hawa ni wakimbizi na wahamiaji wanaolazimika kuzikimbia na kuzihama nchi zao. Matokeo yake ni watu wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, kiasi cha kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Kuna watoto wanaoteseka na kunyanyasika kwa sababu ya rangi na mahali wanapotoka. Licha ya changamoto zote hizi, Kristo Yesu anaendelea kutoa mfano bora wa kufuatwa kwa njia ya huduma makini ya upendo, msamaha, sadaka na mahangaiko ya watu, kwa njia ya ushuhuda wa upendo unaomwilishwa katika upendo kwa jirani, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Imekuwa ni vigumu sana kuwasaidia wenye shida! Sr. Eugenia Bonetti anafafanua kwamba Kristo Yesu katika Njia ya Msalaba anakutana na wanawake katika mazingira mbali mbali. Yesu kwa kukutana na Mama yake Bikira Maria inawakumbusha wanawake wengi ambao wameachana na watoto wao ambao “wamezamia Barani Ulaya” kwa matumaini ya kuweza kupata uwezo wa kiuchumi ili, waweze kurejea nyumbani kwao na kuzisaidia familia zao zinazoogelea katika umaskini! Kwa bahati mbaya njiani, wanakabiliwa na hali ngumu na tete ya maisha! Wananyanyasika na kudhulumiwa, kiasi hata cha kukabiliana na kifo machoni pao!

Yesu anapoanguka mara ya kwanza, anawakumbusha watu kuhusu udhaifu wa mwili, unaopaswa kuwakumbusha watu katika ulimwengu mamboleo, kuanza kujivika fadhila za Msamaria mwema, kwa kuwahudumia kwa huruma na mapendo, ili kuganga na kufunga majeraha yao ya kimwili, kimaadili na kiutu; upweke hasi pamoja na watu kuwageuzia kisogo! Kutokana na changamoto mbali mbali za maisha, imekuwa ni vigumu leo hii kutambua ni nani anayehitaji msaada wa kweli. Matokeo yake ni kuona watu wanasimama kidete kudai haki zao msingi; kulinda na kutetea masilahi yao binafsi, kiasi hata cha kuwasahau maskini na wahitaji zaidi. Huu ni wakati muafaka wa kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwasaidia waamini kupenda, kusikiliza na kujibu kilio cha mahangaiko ya maskini!

Watoto wadogo, waathirika wa biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo ya utumwa mamboleo, wote wanaandamana na Kristo Yesu katika Njia yake ya Msalaba kuelekea Kalvari! Kuna umati mkubwa wa watoto wadogo ambao hawana fursa ya kwenda shule. Hawa ndio wale wanaotumikishwa kazi za suluba kwenye machimbo ya migodi, mashamba makubwa makubwa, sekta ya uvuvi na wakati mwingine wanauzwa na kununuliwa kama bidhaa madukani. Ni watoto wanaonyofolewa viungo vyao na kuuzwa “sokoni”. Kimsingi watoto hawa wanayanyaswa hata na Wakristo pasi na huruma hata kidogo.Watoto hawa wamepokwa haki zao msingi na hawana tena fursa ya kuendelea na masomo na wakati mwingine, wanatumiwa kwa ajili ya kuridhisha tamaa za watu wazima kwa kutumbukizwa kwenye utalii wa ngono sehemu mbali mbali za dunia!

Sr. Eugenia Bonetti, kati kati kabisa mwa Njia ya Msalaba anagusia kashfa ya biashara ya binadamu na viungo vyake na kati ya waathirika wakuu ni wakimbizi na wahamiaji. Watu watambue kwamba, wote wanahusika na kuwajibika katika mapambano dhidi ya biashara hii haramu na mifumo yote ya utumwa mamboleo! Watu wanapaswa kusimama kidete kupambana na matukio haya yanayoendelea kudhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu! Kituo cha Nane cha Njia ya Msalaba, Yesu anakutana na wanawake wanaomlilia! Wanawake wanapaswa kujenga ujasiri wa kukabiliana na changamoto za maisha, ili kufikiri na kutenda; ujasiri wa kukutana na maskini, watu wenye tofauti msingi na kuwaangalia kwa jicho la huruma na upendo na wala si kama adui wanaopaswa kufyekelewa mbali kutoka katika uso wa dunia. Wageni na wahamiaji waangaliwe kwa jicho la huruma na upendo; kama ndugu, wanaopaswa kupokelewa na kusaidiwa katika maisha.

Dhuluma na nyanyaso kwa Kristo Yesu kwa njia ya wanawake wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; wanaonyanyasika na kudhulumiwa ni matokeo ya utandawazi usiojali shida na mahangaiko ya jirani. Kituo cha Tisa, Yesu anaanguka mara ya tatu kutokana na uregevu wa mwili kutokana na mateso makali. Kuna makundi makubwa ya wanawake na wasichna ambayo yametumbukizwa kwenye biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Miili yao imekuwa ni mahali pa kuzima vionjo, tamaa na anasa za kibinadamu! Hata leo hii Mungu anaendelea kuuliza, Je, dada yako yuko wapi? Hawa ni watu wanaopaswa kusaidiwa ili hatimaye kukombolewa na biashara pamoja na utumwa mamboleo. Uchu wa mali, fedha, utajiri wa haraka haraka na madaraka ni kati ya mambo ambayo leo hii yamegeuka kuwa ni miungu mamboleo.

Kituo cha Kumi, Yesu anavuliwa nguo iliyogandamana na madonda yake na hivyo kumsababishia maumivu makali. Pamoja na mwelekeo tenge kuhusu wahamiaji na wakimbizi, lakini bado kuna watu wanaothubutu kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya kuwaokoa wakimbizi na wahamiaji kwenye Bahari ya Mediterrania ambayo imegeuka kuwa kaburi lisilo na alama. Kuna watu na familia ambazo zimekuwa ni kielelezo cha Msamaria mwema; kiasi cha kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji, yote haya wanayafanya ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu! Kituo cha Kumi na Nne, Yesu anazikwa kaburini! Matumaini katika ufufuko na maisha mapya!

Leo hii anasema Sr. Eugenia Bonetti kuna makaburi mapya ambayo ni: Jangwa la Sahara na Bahari ya Mediterrania, huko ndiko wahamiaji na wakimbizi wanakohifadhiwa pasi na alama yoyote ile. Hawa ni watu ambao, Jamii imeshindwa kuwapatia hifadhi ya maisha, au kuwaokoa walipokuwa wanakabiliwa na kiu, njaa na utupu jangwani au walipokuwa wanasukwa sukwa na mawimbi mazito ya Bahari ya Mediterrania. Yote haya yanatendeka wakati ambapo viongozi wa Serikali na wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa wanaendelea kujadiliana na kulumbana pasi na muafaka. Matokeo yake, leo hii Jangwa la Sahara limesheheni mifupa ya wakimbizi na wahamiaji, waliofariki dunia kwa kiu na njaa kali. Bahari ya Mediterrania imegeuka kuwa kaburi lisilo na mlinzi!

Mateso na Kifo cha Kristo Msalabani, iwe ni changamoto kwa viongozi wakuu wa Serikali na Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, uwe ni mwanga wa matumaini, furaha, maisha mapya, udugu, ukarimu, umoja na mshikamano kati ya watu, mataifa na sheria mbali mbali duniani!

Via Crucis 2019
18 April 2019, 17:27