Mama Kanisa katika kipindi cha Mwaka 2019 anatarajia kupata Wenyeheri 9 na Watumishi wa Mungu 5 Mama Kanisa katika kipindi cha Mwaka 2019 anatarajia kupata Wenyeheri 9 na Watumishi wa Mungu 5 

Mama Kanisa kupata Wenyeheri wapya 9 na Watumishi wa Mungu 5

Tarehe 19 Machi 2019, Papa Francisko ameridhia kwamba, zichapwe Hati zitakazoliwezesha Kanisa kupata Wenyeheri wapya 9 na Watumishi wa Mungu 5, baada ya kutambua fadhila za kishujaa walizoonesha wakati wa uhai wao. Kati yao kuna Maaskofu 7 Mashahidi wa imani, waliouwawa wakati wa utawala wa Kikomunisti nchini Romania pamoja na Padre Alfredo Cremonesi wa Italia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko baada ya kukutana na kuzungumza na Kardinali Giovanni Angelo Becciu, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, tarehe 19 Machi 2019 ameridhia kwamba, zichapwe Hati zitakazoliwezesha Kanisa kupata Wenyeheri wapya 9 na Watumishi wa Mungu 5, baada ya Mama Kanisa kutambua fadhila za kishujaa walizoonesha wakati wa uhai wao. Kati yao kuna Maaskofu 7 Mashahidi wa imani, waliouwawa wakati wa utawala wa Kikomunisti nchini Romania pamoja na Padre Pime Alfredo Cremonesi, mmisionari kutoka Italia aliyeuwawa kikatili nchini Myanmar kutokana na chuki dhidi ya imani.

Kanisa linatambua muujiza uliotendwa kwa maombezi ya Sr. Maria Emilia Riguelme wa Zayas, Mwanzilishi wa Shirika la Masista Wamisionari wa Sakramenti kuu na wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Alizaliwa tarehe 5 Agosti 1847 huko Granada, nchini Hispania na kufariki dunia tarehe 10 Mwezi Desemba 1940. Kanisa linatambua na kuthamini kifodini cha Maaskofu 7 kutoka Romania waliouwawa kati ya mwaka 1950-1970. Hawa ni Askofu Valeriu Traian Frenţiu,  Askofu Vasile Aftenie, Askofu Ioan Suciu, Askofu Tit Liviu Chinezu, Askofu Ioan Bălan, Askofu Alessandru Rusu pamoja na Askofu Iuliu Hossu. Kanisa linatambua ushuhuda uliotolewa na Padre Alfredo Cremonesi aliyeuwawa kutokana na chuki za kidini huko Myanmar. Padre Cremonesi alizaliwa tarehe 7 Februari 1953.

Kanisa limetambua fadhila za kishujaa zilizoshuhudiwa na Watumishi wa Mungu Padre Francesco Maria Di Francia, Padre wa Jimbo na muasisi wa Shirika la Masista Wakapuchin wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, aliyezaliwa tarehe 19 Februari 1853 huko Messina, Italia na kufariki dunia tarehe 22 Desemba 1913. Sr. Maria Hueber, muasisi wa Shirika la Masista wa Utawa wa tatu wa Mtakatifu Francisko, aliyezaliwa tarehe 22 Mei 1653 huko Bressanone, Italia na kufariki dunia tarehe 31 Julai 1705. Sr. Maria Teresa Camera, Muasisi wa Shirika la Mabinti wa Mama Yetu wa Huruma. Alizaliwa tarehe 8 Oktoba 1818 huko Ovada, Italia na kufariki dunia tarehe 24 Machi 1894.

Watumishi wa Mungu waliomo kwenye orodha hii ni pamoja na Sr. Maria Teresa Gabrieli, Muasisi mwenza wa Shirika ya Watawa wanawake maskini, Alizaliwa tarehe 13 Septemba 1837 huko Bergamo, Italia na kufariki dunia tarehe 6 Februari 1908. Mwishoni ni Sr. Giovanna Francesca wa Roho Mtakatifu, Mwanzilishi wa Shirika la Masista Wafranciskani Wamisionari wa Neno wa Mungu, aliyezaliwa tarehe 14 Septemba 1888 huko Emilia, Italia na kuaga dunia tarehe 21 Desemba 1984.

Wenyeheri Wapya

 

21 March 2019, 09:59