Mwenyeheri Mariano Mullerat y Soldevila: Mwamini mlei, Baba wa familia, mwanasiasa, mwandishi wa habari lakini zaidi daktari wa maskini! Mwenyeheri Mariano Mullerat y Soldevila: Mwamini mlei, Baba wa familia, mwanasiasa, mwandishi wa habari lakini zaidi daktari wa maskini! 

Mwenyeheri Mariano: Mwanasiasa, Daktari na Mwandishi wa habari!

Mwenyeheri Mariano Mullerat Soldevila, alizaliwa tarehe 24 Machi 1897. Kunako mwaka 1922 akafunga ndoa na Bi Dolores Sans Bovè na kubahatika kupata watoto watano. Nyumba yao, daima ilikuwa wazi kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa na maskini! Alisimama kidete kutetea tunu msingi za maisha ya Kiinjili kama: daktari wa maskini, mwanasiasa na mwandishi wa habari.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Giovanni Angelo Becciu, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, tarehe 23 Machi 2019, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, amemtangaza Mtumishi wa Mungu Mariano Mullerat Soldevila kuwa Mwenyeheri, katika Ibada iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Tarragona, nchini Hispania. Mwenyeheri Mariano Mullerat Soldevila, alikuwa ni mwamini mlei, baba wa familia na daktari aliyeuwawa kikatili kutokana na chuki dhidi ya imani “In odium fidei”. Ni daktari aliyetoa kipaumbele cha kwanza kwa wagonjwa maskini bila kudai chchote kutoka kwao.

Mwenyeheri Mariano Mullerat Soldevila, alizaliwa tarehe 24 Machi 1897. Kunako mwaka 1922 akafunga ndoa na Bi Dolores Sans Bovè na kubahatika kupata watoto watano. Nyumba yao, daima ilikuwa wazi kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa na maskini! Alisimama kidete kutetea tunu msingi za maisha ya Kiinjili kama: daktari, mwanasiasa na mwandishi wa habari. Kunako mwaka 1936 wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Hispania, Mariano Mullerat Soldevila alikamatwa na kutiwa nguvuni kutokana na ushuhuda wake wa imani kwa Kristo na Kanisa lake! Mwamini mlei ambaye kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, ameweza kushiriki kikamilifu: Unabii, Ufalme na Ukuhani wa Kristo Yesu, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake, kwa ajili ya upendo kwa maskini, akiwakumbusha wanasiasa kwamba, siasa ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huduma ya upendo kwa jirani! Kabla ya kuuwawa kikatili, aliandika orodha ya majina ya wagonjwa wake na kumwomba Askari Magereza kumkabidhi daktari mwingine, ili aendelee kuwahudumia hata baada ya kifo chake!

Ni mwamini mlei aliyerutubisha maisha na utume wake kwa njia ya tafakari ya Neno la Mungu; alijitahidi kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Ibada ya Misa, humo akajichotea neema na baraka ya kuwa ni Ekaristi kwa ajili ya wagonjwa na maskini. Alitenga muda wa ziada kwa ajili ya kuabudu Ekaristi Takatifu, ili kumsikiliza Kristo Yesu aliyekuwa anazungumza naye kutoka katika undani wa maisha yake. Ibada hii, ikawa ni chemchemi ya upendo na ukarimu kwa jirani zake, kiasi hata cha kuwa tayari kumwaga damu yake kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.

Mwenyeheri Mariano Mullerat Soldevila aliuwawa pamoja na wenzake watano, lakini ni yeye peke yake, ambaye Mama Kanisa ameamua kumtangaza kuwa ni Mwenyeheri anasema Kardinali Giovanni Angelo Becciu katika mahojiano maalum na Vatican News! Hii inatokana na ukweli kwamba, katika maisha yake, alijitahidi kuzama kabisa katika tunu msingi za maisha ya Kikristo, kiasi cha kuwasamehe hata watesi wake, wakati alipokuwa anakaribia kuiga dunia! Wakati akisali, mtesi wake, akampiga na jembe mdomoni, ili kumshikisha adabu! Mbele ya mashuhuda wa imani, waamini wanajisikia wadogo sana kuliko hata mbegu ya haladali!

Huu ni mwaliko kwa waamini kusimama kidete kutangaza na kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ushuhuda wa imani tendaji! Kardinali Giovanni Angelo Becciu katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu amekazia umuhimu wa waamini kujikita katika upendo wa Kristo na wala hakuna kitu chochote kile kinachoweza kuwatenga na upendo huo. Upendo huo unawajalia nguvu ya kuhimili mateso, dhuluma na nyanyaso, kiasi cha kuwakirimia utakatifu wa maisha kwa njia ya huduma.

Mwenyeheri Mariano
23 March 2019, 16:22