Vatican News
Dini mbali mbali duniani zina mchango mkubwa katika utekelezaji wa Malengo ya Mendeleo Endelevu ya Binadamu ifikapo 2030 Dini mbali mbali duniani zina mchango mkubwa katika utekelezaji wa Malengo ya Mendeleo Endelevu ya Binadamu ifikapo 2030  (ANSA)

Dini na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030

Kardinali Turkson, katika hotuba yake amekazia mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu; umuhimu wa kusikiliza na kujibu kilio dunia na kilio cha maskini duniani! Dini zinapaswa kuwa ni kikolezo cha mageuzi katika mchakato mzima wa maendeleo fungamani ya binadamu na kwamba, majadiliano katika ukweli na uwazi, yaendelezwe.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030 ni mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inajizatiti katika kutokomeza umaskini, baa la njaa na magonjwa duniani. Watu wanapaswa kupatiwa elimu bora, kwa kuhakikisha usawa wa kijinsia pamoja na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote. Jumuiya ya Kimataifa inataka kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na upatikanaji wa maji safi na salama; nishati mbadala kwa gharama nafuu pamoja na uwepo wa mipango bora ya miji na makazi ya watu, ili kudumisha usalama na upatikanaji wa maendeleo fungamani ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe kulinda mazingira pamoja na kudumisha amani duniani!

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu kwa kushirikiana na Sr. Sheila Kinsey, FCJM, Katibu mkuu mwenza wa Tume ya Haki na Amani, Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Jumanne, tarehe 5 Machi 2019, wamewasilisha kwa vyombo vya mawasiliano ya jamii, mkutano wa kimataifa unaoongozwa na kauli mbiu “Dini na Malengo Endelevu ya Binadamu”. Mkutano unaanza tarehe 7-9 Machi 2019 hapa mjini Vatican.

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, katika hotuba yake amekazia mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu; umuhimu wa kusikiliza na kujibu kilio dunia na kilio cha maskini duniani! Dini zinapaswa kuwa ni kikolezo cha mageuzi katika mchakato mzima wa maendeleo fungamani ya binadamu na kwamba, majadiliano katika ukweli na uwazi, yanapaswa kuendelezwa, ili kutekeleza malengo haya kwa haraka zaidi! Malengo ya Maendeleo Endelevu yalipaswa kugharimiwa na Taasisi mbali mbali za fedha pamoja na kufuta madeni makubwa yaliyokuwa yanakwamisha mchakato wa maendeleo kwa Nchi changa zaidi duniani!

Changamoto hii, ikaonekana kukwama na mwaka 2015 ukagota pasi na kufikiwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu! Mkutano huu unaowajumuisha viongozi wa dini mbali mbali unapania pamoja na mambo mengine kusaidia kuhamasisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu, kwa kufanya kazi kwa pamoja! Changamoto kubwa iliyoko mbele ya Jumuiya ya Kimataifa ni kilio cha Dunia Mama kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira pamoja na kusikiliza kilio cha maskini duniani, ambao kimsingi ndiyo waathirika wakuu wa mabadiliko ya tabianchi. Amana na utajiri kutoka kwa watu mbali mbali duniani, visaidie kukoleza maisha: kiroho na kimwili. Waamini wa dini mbali mbali duniani, wanaweza kushiriki kikamilifu katika kujibu kilio cha maskini duniani; watu wanaohitaji chakula bora, maji safi na salama, huduma makini ya afya na elimu pamoja na makazi bora zaidi.

Dini mbali mbali ni viungo muhimu sana katika kukoleza mchakato wa maendeleo endelevu na fungaman ya binadamu. Dini ni mdau mkubwa wa elimu, afya, ustawi na maendeleo ya watu kwa asilimia 50% kwenye maeneo yaliyoko chini ya Jangwa la Sahara na kwamba, zinachangia zaidi ya asilimia 12% ya rasilimali fedha katika sekta ya afya. Kumbe, dini zinaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko katika mtindo wa maisha, uzalishaji, biashara, ulaji pamoja na utunzaji wa taka. Dini zinataka kuchangia kuhusu maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu kwa siku za usoni.

Umoja wa Mataifa uwasaidie wananchi sehemu mbali mbali za dunia kudumisha ekolojia, kwa kujikita katika wongofu wa kiekolojia, ili kuleta mabadiliko yanayokusudiwa kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Huu ni wajibu fungamani kwani madhara yake yanawaathiri watu wote bila ubaguzi. Uchafuzi mkubwa wa mazingira unaendelea kuhatarisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi duniani. Malengo ya Maendeleo Endelevu yanapaswa kuvaliwa njuga kwa kusikiliza kilio cha Dunia Mama pamoja na kujibu kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kwa upande wake, Sr. Sheila Kinsey, FCJM, Katibu mkuu mwenza wa Tume ya Haki na Amani, Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume amekazia mchango uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Laudato si” na kama alivyokazia kwenye hotuba yake, wakati alipokuwa analihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Mwezi Septemba 2015. Alisema, kuna ajenda za Kimataifa ambazo kamwe haziwezi kuahirishwa kutokana na unyeti pamoja na athari zake katika maisha, ustawi na maendeleo ya watu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujikita katika kukuza na kudumisha ustawi wa watu; amani na mshikamano wa dhati unaosimamiwa na kanuni auni!

Sr. Sheila Kinsey anaendelea kufafanua kwamba, muda unazidi kuyoyoma kwa kasi, kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kutekeleza kwa haraka Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu. Umoja na mshikamano wa dhati ni mambo msingi katika utekelezaji wa Malengo haya kwa vitendo. Watu kutoka katika makundi na medani mbali mbali za maisha wanapaswa kushirikishwa katika utekelezaji wake.

Malengo Maendeleo

 

 

06 March 2019, 16:31