Vatican News
Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi kwa Watoto Wadogo: Dhamana na Wajibu wa Askofu Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi kwa Watoto Wadogo: Dhamana na Wajibu wa Askofu  (ANSA)

Mkutano wa kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto: Wajibu wa Askofu

Maaskofu na Wakuu wa Mashirika wanao wajibu wa kuwasikiliza kwa makini waathirika, ili haki iweze kutendeka; kwa kujikita pia katika: huruma na upendo. Maaskofu wanaposhindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu, Sheria za nchi zinaingilia kati kutokana na ukweli kwamba, wakleri na watawa wameshindwa kuishi kadiri ya wito na utume wao ndani ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Rubén Salazar Gómez, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bogotá nchini Colombia, katika hotuba yake kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo, Alhamisi, tarehe 21 Februari 2019 amekazia kuhusu dhamana na wajibu wa Askofu katika kudhibiti kashfa ya nyanyaso za kijinsia kwa kutenda kwa ushupavu mkuu! Kwanza kabisa, Askofu anapaswa kutekeleza wajibu wake kama Mchungaji mkuu; anatakiwa kutenda kwa kushirikiana katika urika wa Maaskofu chini ya uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Pili, Askofu anawajibika kwa Mapadre na Watawa wanaofanya kazi katika eneo lake! Maaskofu watambue kwamba, wanawajibika pia kwa watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, kashfa ya nyanyaso za kijinsia ambayo imechafua maisha na utume wa Kanisa ni matokeo ya uchu wa mali na madaraka; sanjari na matumizi mabaya ya madaraka ndani ya Kanisa. Ili kupambana na changamoto hii, kuna haja ya kufanya toba na wongofu wa ndani; kwa kutenda zaidi kuliko maneno, kwani maneno matupu kamwe hayawezi kuvunja mifupa! Viongozi wa Kanisa watambue kwamba, wanawajibika mbele ya Mungu na Kanisa na kwamba, wao ni wachungaji wakuu.

Askofu anayo dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, dhamana anayoitekeleza kwa kujenga na kudumisha umoja na ushirikiano katika urika wa Maaskofu chini ya Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kumbe, wanao wajibu wa kuwasikiliza kwa makini waathirika, ili haki iweze kutendeka; kwa kujikita pia katika: huruma na upendo. Maaskofu wanaposhindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu, Sheria za nchi zinaingilia kati kutokana na ukweli kwamba, wakleri na watawa wameshindwa kuishi kadiri ya wito na utume wao ndani ya Kanisa.

Ni ukweli usiofumbiwa macho kwamba, kashfa ya nyanyazo za kijinsia imeenea sana hata katika jamii, lakini hiki si kibali kwa kashfa kama hizi kutendeka ndani ya Kanisa, kwani lengo la Kanisa ni wokovu wa roho za watu na maisha ya uzima wa milele. Vyombo vya mawasiliano pamoja na mitandao ya kijamii, imesaidia sana kubainisha kashfa hii katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza waandishi wa habari ambao wamekuwa wa kweli kwa kubainisha kashfa hizi ndani ya Kanisa na kwamba, watu wawe na ujasiri wa kufichua makossa kama haya.

Kardinali Rubén Salazar Gómez, anaendelea kufafanua kwamba, Kanisa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, limepambana sana na kashfa za nyanyaso za kijinsia, lakini halina budi kusimama kidete, ili kashfa kama hizi zisijitokeze tena na wahusika wapewe adhabu inayowapasa! Askofu mahalia anatenda kazi kwa kushirikiana na Maaskofu katika urika wa Maaskofu chini ya Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa” ili kuliwezesha Kanisa kufanya maamuzi kwa kushikamana. Sekretarieti kuu ya Vatican iliwahi kutoa “Mwongozo wa Kanuni za Maisha ya Kipadre.

Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake Binafsi ya kichungaji, “Kama Mama mpendelevu” iliyochapishwa Juni, 2016, anasema nyanyaso za kijinsia ni kati ya makosa makubwa ambayo yamebainishwa barabara kwenye Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa. Baba Mtakatifu anapenda kuwahimiza viongozi wa Kanisa kuwa macho dhidi ya nyanyaso za kijinsia wanazoweza kufanyiwa watoto wadogo; anaonesha hatua zitakazochukuliwa ili kutekeleza vifungu vya Sheria ambavyo viko tayari kwenye Sheria za Kanisa Namba 193§ 1 na Sheria za Kanisa la Mashariki Namba 975§1. Mkazo hapa ni wajibu wa viongozi wa Kanisa katika kutekeleza dhamana na utume wao! Malezi na majiundo endelevu kwa Maaskofu ni mambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa.

Maaskofu wanakumbushwa kwamba, wanayo dhamana na wajibu kwa Wakleri na watawa wanaoishi na kufanya utume katika maeneo yao, kwa kuangalia utakatifu wa maisha na utume wao! Kumbe, uchaguzi wa vijana wanaotaka kuingia katika wito na maisha ya kipadre na kitawa ni muhimu sana! Maaskofu wanapaswa kufuatilia malezi na majiundo yao katika hatua mbali mbali na kwamba, Askofu anapaswa kuwa karibu zaidi na mapadre pamoja na watawa wake ili kujenga na kudumisha majadiliano katika udugu, ili aweze kuwasindikiza katika shida na mahangaiko yao, katika furaha na matarajio yao.

Shutuma za nyanyaso za kijinsia dhidi ya mapadre na watawa zinapaswa kushughulikiwa kadiri ya Sheria za Kanisa na Sheria za nchi husika. Watuhumiwa wasaidiwe kutambua hali yao! Haki za pande zote zinazohusika zinapaswa kudumishwa, lakini waathirika wa nyanyaso za kijinsia wanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, hali ambayo itamlazimisha Askofu mahalia kumsimamisha Padre wake kutoa huduma ya hadhara. Kwa hakika kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa imesababisha madhara makubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, wajibu wa kwanza ni kuwasikiliza waathirika wa nyanyaso za kijinsia.

Kuna wakati waathirika wa nyanyaso za kijinsia walikuwa wanasukumwa zaidi kupata fidia, bila kuzingatia madhara waliyokuwa wanasababisha katika maisha na utume wa Padre husika. Ni kutokana na kishawishi cha kutaka kuwalinda mapadre na watawa dhidi ya shutuma za nyanyaso za kijinsia, kukaibuka rushwa ili kuzima kilio cha watu waliokuwa wanataka haki itendeke. Kamwe fedha haitaweza kuwa ni kipimo cha haki, lakini kuna baadhi ya waathirika wameathirika kiasi kwamba, wanahitaji ruzuku ili kusonga mbele.

Kumbe, katika mazingira na hali kama hizi Kanisa halina budi kuwapatia waathirika msaada wa: kiroho, kisaikolojia, kiakili na kiutu. Changamoto kubwa mbele ya Kanisa ni kwa wakleri na watawa kujibidisha zaidi katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kuambata neema na utakatifu wa maisha. Kanisa linawahitaji mapadre na watawa wema na watkatifu watakaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Umoja na mshikamano ni muhimu sana katika kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa.

Kardinali Gomez
21 February 2019, 16:01