Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi kwa Watoto Wadogo: Ibada ya Misa ya Kufunga Mkutano. Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi kwa Watoto Wadogo: Ibada ya Misa ya Kufunga Mkutano. 

Mkutano Kuhusu Ulinzi wa Watoto: Sasa ni mwanzo mpya wa Kanisa!

Viongozi wa Kanisa wamepewa mamlaka ya kuwahudumia watu wa Mungu, ili wapate kuwajenga na wala si kuwaangusha. Kuna hatari kwamba, mamlaka yakatumiwa vibaya na hivyo kuharibu maisha ya watu, ikiwa kama mamlaka haya yanakwenda kinyume cha huduma na upendo. Mbaya zaidi, mamlaka haya yanaweza hata kuua kama ilivyo katika kashfa ya nyanyaso za kijinsia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatiacn.

Wajumbe wa Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo, Jumapili, tarehe 24 Februari 2019 wameshiriki Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye “Sala Regia” na mahubiri kutolewa na Askofu mkuu Mark Benedict Coleridge wa Jimbo kuu la Brisbane, Australia ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Australia. Katika mahubiri yake, amewaalika wajumbe kusikiliza kwa makini sauti ya Kristo Yesu, anayezungumza kwa mamlaka, kama hata michoro mbali mbali inayopamba “Sala Regia” inavyoshuhudia. Hii ni michoro ya mapambano na vita ya kidini; mauaji na dhuluma mbali mbali; ni mapambano kati ya Wafalme wa dunia na viongozi wa Kanisa.

Liturujia ya Neno la Mungu inawaalika wajumbe kutafakari mamlaka, dhana ambayo imechambuliwa kwa kina na mapana wakati wa mkutano wao. Somo la kwanza linamwonesha Daudi jinsi alivyosukumwa na busara na kuweza kutumia madaraka yake kuokoa maisha ya Mfalme Saul, Mpakwa wa Bwana! Viongozi wa Kanisa wamepewa mamlaka ya kuwahudumia watu wa Mungu, ili wapate kuwajenga na wala si kuwaangusha. Kuna hatari kwamba, mamlaka yakatumiwa vibaya na hivyo kuharibu maisha ya watu, ikiwa kama mamlaka haya yanakwenda kinyume cha huduma na upendo. Mbaya zaidi, mamlaka haya yanaweza hata kuua kama ilivyo katika kashfa ya nyanyaso za kijinsia.

Wahusika wa nyanyaso za kijinsia wamedhirika kuwa ni watu ambao wamemezwa sana na malimwengu! Lakini katika Injili ya leo, Kristo Yesu anawataka wafuasi wake, kuwapenda adui zao. Adui wa Kanisa katika muktadha huu ni wale wote walioshiriki kutenda na kunyamazia uhalifu huu; waathirika ambao wamelisababishia uchungu Kanisa kwa kufunua ukweli wa madonda ya maisha yao kwa ujasiri mkuu. Lakini, kwa bahati mbaya, Kanisa liliwaona waathirika wa nyanyaso hizi kuwa kama adui, kiasi hata cha kushindwa kuwapenda, kuwathamini na kuwabariki, kiasi kwamba, Kanisa likageuka kuwa ni adui mkubwa wa waathirika wa nyanyaso za kijinsia.

Kristo Yesu anawataka wafuasi wake kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni alivyo na huruma! Lakini, Kanisa limeshindwa kuwa ni chombo cha huruma ya Baba wa mbinguni! Matokeo yake, likawageuzia waathirika kisogo, ili kulinda na kutunza heshima ya Kanisa na viongozi wake! Ni kutokana na mwelekeo huu, lazima viongozi wa Kanisa wapate adhabu inayowastahili kama ilivyokuwa kwa Mfalme Saul, ili kutoa nafasi kwa utakatifu wa maisha na utume wa Kanisa kuchanua tena. Lakini, ni kwa njia ya toba na wongofu wa ndani utakaoliwezesha Kanisa kuona na kugusa madonda ya waathirika wa nyanyaso za kijinsia na kutambua kwamba, wao kamwe si adui wa Kanisa.

Toba na Wongofu wa ndani ni mageuzi makubwa kwa kutambua kwamba, waathirika wa nyanyaso za kijinsia ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani, Kanisa. Kumbe, huu ni mwaliko wa kuwaangalia, kuwasikiliza kwa makini, ili kuanza mapambazuno mapya ya maisha na utume wa Kanisa kwa kutambua kwamba, nyanyaso ambazo wamewafanyia watoto wadogo ni sawa na kumfanyia Kristo mwenyewe. Waathirika hawa wawe ni madaraja ya kuweza kukutana tena na Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kanisa liwe na ujasiri wa kuona na kugusa Madonda yake Matakatifu.

Askofu mkuu Mark Benedict Coleridge anendelea kufafanua kwamba, Kanisa limekuwa Mlimani Kalvari kuanzia tarehe 21-24 Februari 2019, ili kusikiliza kilio cha waathirika wa nyanyaso za kijinsia; kilio cha Kanisa kutoka katika usiku wa giza nene! Katika Mlima huu, Kanisa limebahatika tena kuwa na imani, matumaini na mapendo na kwamba, giza la Mlima Kalvari, limewasaidia kuona mwanga wa Mwanakondoo wa Mungu, Kristo Yesu anayewakirimia tena zawadi ya amani na kuwapatia nguvu ya Roho Mtakatifu anayefukuzia mbali roho ya woga na hivyo kuwawezesha tena viongozi wa Kanisa kuwa na ari na mwamko mpya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili inayopaswa kumwilishwa katika matendo, kielelezo cha imani tendaji!

Huu ni muda wa kutenda haki, kuganga na kuwaponya waathirika wa nyanyaso za kijinsia; kwa kuwasikiliza na kuambatana nao katika safari ya maisha yao; tayari kuwalinda na watuhumiwa kufikishwa mbele ya sheria ili haki iweze kushika mkono wake. Kanisa litaendeleza mchakato wa malezi na majiundo makini kwa viongozi wake; kwa kuwaelimisha maana ya ulinzi na usalama kwa watoto wadogo. Kanisa litaendelea kujizatiti ili makosa na mapungufu yaliyojitokeza huko nyuma hayarudiwi tena, ili Kanisa liendelee kuwa ni Mama mwema na mpendelevu, anayewatakia watoto wake amani, utulivu na wema.

Kanisa litaendelea kujifunza zaidi madhara ya nyanyaso za kijinsia, ili hatimaye, kuweza kuzing’oa, kwa kutambua kwamba, yote haya yanahitaji muda ili kutekelezwa na ufanisi wake kuanza kuonekana. Kwa njia hii, Kanisa litaweza kuona amani ya Kristo Mfufuka na kuweza kuwagawia watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Amani kwa namna ya pekee, inahitaji sadaka ya kuweza kusimama tena katika imani, matumaini na mapendo pamoja na kuendelea kujizamisha katika sadaka ya Kristo Yesu, aliyekuwa kafara na mshindi. Yesu ndiye atakayefuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwepo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita!

Mahubiri Misa: Nyanyaso
24 February 2019, 15:34