Siku ya Kupambana na Biashara ya binadamu na utumwa mamboleo 2019: Tushikamane kwa pamoja! Siku ya Kupambana na Biashara ya binadamu na utumwa mamboleo 2019: Tushikamane kwa pamoja! 

Siku ya Kupambana na Biashara ya Binadamu & Utumwa mamboleo 2019

Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu na utumwa mamboleo unaoendelea kudhalilisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni siku ya sala na tafakari ya kina kuhusu madhara ya biashara ya binadamu na viungo vyake, pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo ambayo ni uhalifu mkubwa dhidi ya ubinadamu. Tushikamane kwa pamoja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Februari, anaadhimisha kumbu kumbu ya Mtakatifu Josefina Bakhita aliyezaliwa kunako mwaka 1868 huko Sudan Kongwe na kufariki dunia tarehe 8 Februari 1947. Mtakatifu Yohane Paulo II akamtangaza Josefina Bakhita kuwa Mwenyeheri tarehe 17 Mei 1992, na hatimaye, akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe 1 Oktoba, mwaka 2000. Katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Josefina Bakhita, kunako mwaka 2015, Kanisa lilianzisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu na utumwa mamboleo unaoendelea kudhalilisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Hii ni siku ya sala na tafakari ya kina kuhusu madhara ya biashara ya binadamu na viungo vyake, pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo ambayo ni uhalifu mkubwa dhidi ya ubinadamu. Maadhimisho haya kwa mwaka 2019 yanaongozwa na Kauli mbiu: “Tushikamane kwa pamoja kupambana na biashara ya binadamu”. Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu kama sehemu ya maadhimisho ya Siku hii hadhimu, Alhamisi, tarehe 7 Februari 2019 limefanya kongamano kwa kuwashirikisha wadau mbali mbali katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, kwa kukazia umuhimu wa wadau kushikamana katika mapambano dhidi ya vitendo hivi viovu ndani ya jamii. Hawa ni watu wanaotumbukizwa katika biashara ya ngono, kazi za suluba,  ndoa za shuruti pamoja na watoto kupelekwa mstari wa mbele kama chambo cha vita!

Padre Michael Czerny, Katibu mkuu msaidizi, Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza ya Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu anasema kwamba, hivi karibuni, Baraza lake lilichapisha Mwongozo wa Shughuli za Kichungaji Kuhusiana na Biashara ya Binadamu. Mwongozo huu unafafanua kwa kina na mapana janga kubwa la biashara ya binadamu linaloendelea kukua na kupanuka kila mwaka sehemu mbali mbali za dunia. Serikali zinapaswa kuwa makini kulinda maisha na usalama wa raia wake. Wahusika watafutwe, wakamatwe na sheria ishike mkondo wake.

Kwa upande wake, Padre Frederic Fornos, Mkurugenzi wa Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa anasema, Baba Mtakatifu Francisko yuko mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya biashara ya binadamu na utumwa mamboleo. Baba Mtakatifu anasikitika kusema, watu wengi wanajikuta wakihatarisha maisha yao kwa kujitumbukiza hata katika mitego haramu inayohatarisha maisha, utu na heshima yao. Matokeo yake ni wahamiaji na wakimbizi kutumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Makundi ya kigaidi na magenge ya uhalifu wa kimataifa yanatumia njia za wakimbizi na wahamiaji kujipatia fedha haramu.

Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuunganisha nguvu zao ili kupambana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; kwa kuwalinda na kuwasaidia kwa dhati waathirika. Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaongoa wafanyabiashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo na awajalie matumaini ya kuweza kujipatia tena uhuru wale wote wanaoteseka kutokana na janga hili la aibu katika maisha yao! Hiki ni kilio cha sala ya watu wanaoteseka kutokana na biashara ya binadamu na utumwa mamboleo.

Wakati huo huo, Sr. Gabriella Bottani kutoka Shirika la Wacomboni, anasema, “Talita Kum”  ni mtandao wa Mashirika  ya Kitawa na Kazi za Kitume Kimataifa  unaotekeleza dhamana na wajibu wake katika nchi 77 duniani. Mtandao huu ukipewa ushirikiano wa dhati na vyombo vya ulinzi na usalama kitaifa na kimataifa, uhalifu dhidi ya ubinadamu unaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu; kwa kuwatambua waathirika, kuwasaidia pamoja na kuhakikisha kwamba, wanatendewa haki, ili wahusika waweze kufikishwa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama na sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Hapa kuna haja ya kujikita katika mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato kwa kutoa elimu makini; kwa kuendesha kampeni za uragibishaji sanjari na kuwalinda watu ambao wanaweza kutumbukizwa katika mifumo ya utumwa mamboleo. Kauli mbiu ya maadhimisho kwa mwaka 2019 ni changamoto pevu ya kutaka kuunganisha nguvu ili kupambana kufa na kupona na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.

Mtakatifu Bakhita 2019
08 February 2019, 08:52