Miaka 70 ya Haki Msingi za Binadamu na Miaka 25 ya Tamko la Vienna ni amana na utajiri wa binadamu! Miaka 70 ya Haki Msingi za Binadamu na Miaka 25 ya Tamko la Vienna ni amana na utajiri wa binadamu! 

Tamko la Haki Msingi za Binadamu & Tamko la Vienna Miaka 25

Kardinali Turkson anakaza kusema, haki msingi za binadamu ziliimarishwa tena katika Tamko la Vienna lililotolewa mwaka 1993 kwa kuzishirikisha nchi 171, ikilinganishwa na nchi 58 zilizoweka sahihi katika Tamko la Haki Msingi za Binadamu kunako mwaka 1948. Tamko la Vienna ni amana na utajiri wa binadamu wote na ni alama ya matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican

Kwa muda wa siku mbili kuanzia tarehe 10 -11 Desemba 2018, Baraza la Kipapa la Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian kilichoko mjini Roma, limekuwa likiendesha mkutano wa kimataifa unaoongozwa na kauli mbiu “Haki Msingi za Binadamu katika Ulimwengu Mamboleo: Mafanikio; Yaliyoachwa, Yaliyofutwa”. Hii ni sehemu ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu Tamko la Haki Msingi za Binadamu lilipochapishwa sanjari na kumbu kumbu ya Miaka 25 ya Tamko ya Vienna na Mbinu Mkakati wa Utekelezaji wa Haki Msingi za Binadamu!

Kardinali Peter  Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu mkutano wa kimataifa ambao umeongozwa na kauli mbiu “Haki Msingi za Binadamu katika Ulimwengu Mamboleo: Mafanikio; Yaliyoachwa, Yaliyofutwa” amekazia: umuhimu wa utekelezaji wa haki msingi za binadamu kama kiini cha utume wao unaofumbatwa katika mchakato wa kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Haki msingi za binadamu haziamishiki wala kutenganishwa; ni sehemu ya utu na heshima ya binadamu na kwamba, haki hizi zinajikita katika usawa wa binadamu na kuwawajibisha wote mbele ya sheria. Hizi ni haki zinazoingiliana na kutegemeana; zinashirikisha na kujumuisha.

Kardinali Turkson anakaza kusema, haki msingi za binadamu ziliimarishwa tena katika Tamko la Vienna lililotolewa mwaka 1993 kwa kuzishirikisha nchi 171, ikilinganishwa na nchi 58 zilizoweka sahihi katika Tamko la Haki Msingi za Binadamu kunako mwaka 1948. Tamko la Vienna ni amana na utajiri wa binadamu wote na ni alama ya matumaini. Lakini changamoto kwa sasa ni kuangalia, mahali ambapo matumaini ya haki msingi za binadamu yametekelezwa kwa dhati. Hapa kuna haja ya kuwa na utashi wa kisiasa ili kutekeleza maazimio haya ya Umoja wa Mataifa, vinginevyo zitakuwa ni nyaraka zinazofungiwa makabatini pasi na mafao kwa binadamu.

Kumekuwepo na uvunjaji mkubwa wa haki msingi za binadamu, hali inayosigina utu na heshima ya binadamu na madonda ya zamani kuendelea kuchuruzika damu, kama ilivyo kwa utumwa ambao leo hii kuna mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Kumekuwepo na ongezeko kubwa la umaskini na ukosefu wa haki jamii; matumizi ya nguvu yanayopelekea hata wakati mwingine kuibuka kwa vita na waathirika na raia wa kawaida. Haya ni matokeo ya biashara haramu ya silaha inayofumbatwa katika uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka!

Yote haya ni uvunjifu wa haki ya maisha! Bado kuna umati mkubwa wa watu wasiokuwa na haki ya kupata tiba, elimu bora, kazi na mahali pazuri zaidi pa kuishi. Amani ni mhimili mkuu wa haki nyingine zote za binadamu, ambayo inapaswa kufumbatwa katika mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Ni matumaini ya Kardinali Turkson kwamba, maoni ya mkutano huu wa kimataifa yatalisaidia Kanisa kuendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu.

Kardinali Turkson: Utu wa binadamu
11 December 2018, 10:00