Vatican News
Kanisa na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Saratani: Mkazo: Kanuni maadili, utu wema; haki jamii; utu na heshima ya binadamu! Kanisa na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Saratani: Mkazo: Kanuni maadili, utu wema; haki jamii; utu na heshima ya binadamu!  (AFP or licensors)

Sera na mikakati ya Kanisa kupambana na ugonjwa wa Saratani

Zaidi ya washiriki 60, wengi wao wakiwa ni watafiti, wahudumu, watunga sheria, wanadiplomasia na wawakilishi vya vyama na mashirika mbali mbali dhidi ya ugonjwa wa Saratani. Lengo lilikuwa ni kuibua mbinu mkakati utakaotekelezwa hadi kufikia mwaka 2030 kwa kuwa na tafiti za ugonjwa wa Saratani ili kukinga, kutibu na kutoa huduma kwa waathirika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Huduma kwa wagonjwa ni mchango mkubwa unaosaidia kutoa utambulisho wa Kanisa kama Sakramenti inayomwilisha mpango na upendo wa Mungu kwa ajili ya mwanadamu. Huu ni utume na dhamana ya Kanisa, kama sauti ya kinabii, kwa ajili ya kulinda na kutetea zawadi ya maisha, utu na heshima ya mwanadamu.  Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika Barua yake ya Kichungaji "Mungu ni Upendo" anakazia umuhimu wa taaluma katika huduma kwa mwanadamu, ili kuwawezesha kutekeleza wajibu wao kikamilifu na kwa kujiamini zaidi, bila kubahatisha wala kubabaika.

Mwelekeo huu wa kibinadamu lazima upate chimbuko lake katika moyo wa daktari, unaomsukuma kwa namna ya pekee, kumwonjesha mgonjwa upendo wa dhati, kwa kuthamini na kuheshimu utu wake kama binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Madaktari wanakumbushwa kwamba, maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wao kama madaktari wanayo dhamana kwanza kabisa ya: kuilinda na kuitetea zawadi hii dhidi ya hatari zote zinazoendelea kujitokeza kwa mwanadamu!

Kwa kulitambua Kanisa kama sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, ni mwaliko kwa madaktari katika tafakari na utendaji wao wa kazi, kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kadiri ya uwezo na nyenzo zilizopo kuboresha huduma kwa wagonjwa kwa kuwapatia tiba yenye uhakika na matumaini katika huduma inayotolewa na wahudumu wa sekta ya afya. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi na mashirika ya kimataifa mwanzo mwa mwaka 2018 alisema, kuna haja ya kuunganisha nguvu ili kutekeleza sera na mikakati itakayowasaidia wagonjwa kupata dawa kwa gharama nafuu, kuendelea kufanya tafiti na kuboresha huduma ya tiba kwa wagonjwa badala ya kuelemewa na uchu wa kupata faida kubwa; kwani mambo haya ni muhimu sana kwa ajili ya kulinda uhai wa binadamu!

Ugonjwa wa Saratani ni changamoto kubwa kwa jamii kwani athari zake zinajionesha katika mifumo ya afya, uchumi, wagonjwa na familia zao. Inakadiriwa kwamba, kuna wagonjwa wapya wa Saratani milioni 4,23 Barani Ulaya na kwamba, kila mwaka takribani wagonjwa milioni 1,94 wanafariki dunia. Kuna ongezeko kubwa la ugonjwa wa Saratani duniani, changamoto inayohitaji kuwa na sera na mikakati makini itakayosaidia kupambana na Saratani Barani Ulaya, ili kuleta mabadiliko katika maisha ya familia nyingi ndani na nje ya Bara la Ulaya!

Haya ni kati ya mambo ambayo yamebainishwa na Taasisi ya Sayansi za Saratani Ulaya “European Academy of Cancer Sciences, EACS” kwa kushirikiana na Taasisi za Kipapa za Sayansi katika kikao chao, kuanzia tarehe 16-17 Novemba 2018. Zaidi ya washiriki 60, wengi wao wakiwa ni watafiti, wahudumu, watunga sheria, wanadiplomasia na wawakilishi vya vyama na mashirika mbali mbali dhidi ya ugonjwa wa Saratani. Lengo lilikuwa ni kuibua mbinu mkakati utakaotekelezwa hadi kufikia mwaka 2030 kwa kuwa na tafiti za ugonjwa wa Saratani zinazoratibiwa na Umoja wa Ulaya pamoja na kuunda Jukwaa la utekelezaji wa sera hizi katika: kinga, tiba na huduma makini kwa wagonjwa.

Wajumbe wameamua kuongeza juhudi katika tiba na kinga; kuunganisha tafiti na elimu makini, ili kuzuia na kutibu; huduma ambayo inapaswa kutolewa kwenye vituo vya afya, tangu dalili za Saratani zinapoanza kujitokeza. Wajumbe wamekazia ubora wa tafiti na huduma zinazotolewa sanjari na kuwa na mfumo sahihi utakaosaidia kupima mafanikio haya kadiri uchumi katika sekta ya afya. Wanasema, kinga haina budi kusaidia pia mchakato wa kutibu na kuhudumia.

Inakadiriwa kwamba, kiasi cha asilimia 40% ya ugonjwa wa Saratani kinaweza kudhibitiwa, ikiwa kama tangu mwanzo hatua za kuzuia Saratani zingechukuliwa tangu awali, kwa kuchunguza afya mara kwa mara! Mchakato wa kuzuia ugonjwa wa Saratani uhakikishe kwamba, hakuna mtu anayeachwa nyuma na kwamba, kuna haja ya kuwa na ushirikiano wa karibu kati vituo vya uchunguzi wa ugonjwa wa Saratani na mitandao ya kudhibiti ugonjwa wa Saratani. Rasilimali fedha ielekezwe zaidi kwenye vituo vya afya vya majaribio, dhamana inayoweza kutekelezwa vyema zaidi na wanadiplomasia. Taasisi ya Sayansi za Saratani Ulaya pamoja na Taasisi za Kipapa za Sayansi wamekazia: kanuni maadili na utu wema; haki jamii, utu na heshima ya binadamu.

Ugonjwa wa Saratani
23 November 2018, 13:47