Kardinali Filoni: Elimu ni chombo cha uinjilishaji, utamadunisho na majadiliano Kardinali Filoni: Elimu ni chombo cha uinjilishaji, utamadunisho na majadiliano 

Kardinali Filoni: Elimu ni chombo cha uinjilishaji, utamadunisho na majadiliano

Papa Francisko katika Wosia wake wa kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” kuhusu umuhimu wa kurithisha Injili, mchakato wa utamadunisho na ushuhuda unaofumbatwa katika ukatoliki unaoonesha uzuri wa uso wa Kanisa katika mionekano tofauti, matunda ya kazi ya Roho Mtakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu ambaye pia ni mkuu wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kilicho mjini Roma, hivi karibuni, amefungua mwaka wa masomo 2018- 2019 kwa kukazia umoja na utofauti unaofumbatwa katika jumuiya ya wasomi chuoni hapo sanjari na mchakato wa umisionari kama sehemu ya vipaumbele vya Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Kardinali Filoni alifungua mwaka wa masomo kwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu, ili kumwomba Roho Mtakatifu aweze kuwajalia mapaji yake, ili hatimaye, waweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao. Ametumia fursa hii kutafakari kwa kina na mapana kuhusu Wosia wa Kitume wa Papa Francisko “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” kuhusu umuhimu wa kurithisha Injili, mchakato wa utamadunisho na ushuhuda unaofumbatwa katika ukatoliki unaoonesha uzuri wa uso wa Kanisa katika mionekano tofauti, matunda ya kazi ya Roho Mtakatifu.

Kardinali Filoni amegusia pia kuhusu Katiba ya Kitume “Veritatis gaudium” yaani “Furaha ya ukweli” iliyotolewa hivi karibuni na Papa Francisko ambamo anatoa vigezo muhimu vinavyopaswa kuzingatiwa katika sekta ya elimu, kwani lengo ni kujenga na kukuza umoja na udugu, upendo na mshikamano, daima maskini wakipewa kipaumbele cha kwanza! Hii ndiyo dhamana ya umissionari wa Kanisa linatoka kifua mbele ili kuinjilisha na kutamadunisha mintarafu furaha ya ukweli wa Kikristo! Kigezo cha pili ni majadiliano katika ukweli na uwazi mintarafu mwanga wa Injili na Mafundisho ya Kanisa ili kukuza na kudumisha utamaduni wa watu kukutana.

Kigezo cha tatu ni mwingiliano makini wa masomo mbali mbali yanayotolewa na vyuo vikuu pamoja na taasisi za elimu ya juu kwa kuzingatia ubunifu kadiri ya mwanga wa Ufunuo. Majiundo, tafiti, mbinu za ufundishaji na maudhui yanayotolewa yanapaswa kuzingatia Ufunuo na Utume wa Kanisa katika dhamana ya uinjilishaji. Mkazo unaotolewa na Mababa wa Kanisa katika mfumo wa elimu unajikita katika mambo makuu manne yaani: umoja wa kisayansi, mawasiliano ya utakatifu, maisha adili na umwilishaji wa upendo katika maisha ya watu mambo yanayobubujika kutoka katika Neno la Mungu, vinginevyo, sayansi haina mizizi na wala kamwe haiwezi kuacha kumbu kumbu hai katika akili na nyoyo za vijana wa kizazi kipya! Sayansi na utakatifu ni sawa na “uji kwa mgonjwa”.

Kigezo cha nne ni kuunda mtandao wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu ili kuweza kufanya upembuzi yakinifu katika shida, changamoto na hatimaye kuibua suluhu ya mambo yote haya mintarafu mwanga wa Injili, kwa kuwa na mradi wa pamoja unaotekelezwa na Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume! Lengo ni kufahamu matatizo haya na hatimaye, kuyapatia maana na ufumbuzi wake kadiri ya mwanga wa Injili, Mapokeo ya Kanisa Uinjilishaji na Utamadunisho. Maboresho yote haya yanapania kutangaza ukweli wa Injili bila kubezwa ukweli wa mambo na mafao yake kwa wengi.

Kardinali Filoni amegusia pia mchango wa Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu vijana, iliyohitimishwa hivi karibuni hapa mjini Vatican kwa kukazia umuhimu wa kupyaisha mfumo wa elimu unaotolewa na Mama Kanisa, kwa kujikita zaidi katika maandalizi makini na endelevu ya viongozi wa Kanisa, watakaojisadaka kwa ajili ya utume kwa vijana, ili kukabiliana pia na changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Lengo ni kuwawezesha vijana kupata hekima na busara, ili kumwilisha mang’amuzi, uzoefu na ukweli katika uhalisia wa maisha yao.

Vyuo vikuu vya kipapa pamoja na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa zinao mchango mkubwa katika majiundo na malezi ya viongozi mbali mbali wa Kanisa. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, walezi wanapata nafasi ya kujinoa mara kwa mara, kwa kusoma alama za nyakati ili kutoa mchango unaohitajika katika malezi na majiundo ya vijana wa kizazi kipya!

Kardinali filoni
07 November 2018, 12:11