Vatican News
Ajali ya Ndege nchini Indonesia imesababisha watu 189 kupoteza maisha! Ajali ya Ndege nchini Indonesia imesababisha watu 189 kupoteza maisha!  (AFP or licensors)

Papa Francisko asikitishwa na maafa ya ajali ya ndege nchini Indonesia

Baba Mtakatifu anapenda kuwapa pole wale wote walioguswa na msiba huu mzito nchini Indonesia. Baba Mtakatifu anasali kwa ajili ya kuiombea Indonesia na watu wake nguvu na amani katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na taarifa ya watu 189 waliofariki dunia Jumatatu, tarehe 29 Oktoba 2018 kutokana na ajali iliyolikumba Shirika la Ndege la Lion Air kutoka Indonesia. Ndege hiyo aina ya Boing 737 imeanguka muda mfupi tu baada ya kuondoka kutoka Uwanja wa Ndege wa Jakarta, nchini Indonesia, kuelekea mjini Pangkal Pinam. Kutokana na matatizo ya kiufundi, rubani wa ndege alikuwa ameomba kutua kwa dharura katika kiwanja wa ndege cha Jakarta na kabla ya kutekeleza dhamana hii, ndege ikaanguka.

Baba Mtakatifu katika salam za rambi rambi zilizoandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Piero Pioppo, Balozi wa Vatican nchini Indonesia, Baba Mtakatifu anapenda kuwapa pole wale wote walioguswa na msiba huu mzito nchini Indonesia. Baba Mtakatifu anasali kwa ajili ya kuiombea Indonesia na watu wake nguvu na amani katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.

Wakati huo huo, Rais Joko Widodo wa Indonesia katika salam zake za rambi rambi kwa taifa amesema, Serikali kwa sasa inaendelea kujielekeza katika kuokoa miili ya watu waliofariki dunia kutokana na ajali ya ndege. Hii ni ajali mbaya ya ndege kuwahi kutokea nchini Indonesia tangu mwaka 2014 wakati ndege ya Shirika la Ndege la AirAsia ilipoanguka na kusababisha watu 162 waliokuwepo ndani ya ndege hiyo kupoteza maisha!

Ajali Indonesia
30 October 2018, 11:23