Vatican News
Askofu mkuu Edgar Pèna Parra aanza utume wake kama Katibu mkuu msaidizi wa Vatican. Askofu mkuu Edgar Pèna Parra aanza utume wake kama Katibu mkuu msaidizi wa Vatican.  (Vatican Media)

Askofu mkuu Edgar Pèna Parra aanza utume wake kama Katibu mkuu msaidizi wa Vatican

Askofu mkuu Edgar Pèna Parra, alizaliwa kunako mwaka 1960 huko Venezuela, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre mwaka 1985 na mwaka 1993 akaanza utume wake wa kidiplomasia mjini Vatican na kubahatika kufanya kazi katika Ubalozi wa Vatican nchini Kenya, Yugoslavia, Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva; Afrika ya Kusini, Honduras na Mexico.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 15 Oktoba 2018 amemtambulisha rasmi Askofu mkuu Edgar Pèna Parra, mwenye umri wa miaka 58 kutoka Venezuela aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Katibu mkuu msaidizi wa Vatican, kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Kardinali Giovanni Angelo Becciu aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu. Katika utambulisho huu, Baba Mtakatifu aliandamana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na hivyo kupata nafasi ya kukutana na kusalimiana na maafisa pamoja na wafanyakati wa Sekretarieti kuu.

Askofu mkuu Edgar Pèna Parra, alizaliwa kunako mwaka 1960 huko Venezuela, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre mwaka 1985 na mwaka 1993 akaanza utume wake wa kidiplomasia mjini Vatican na kubahatika kufanya kazi katika Ubalozi wa Vatican nchini Kenya, Yugoslavia, Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva; Afrika ya Kusini, Honduras na Mexico. Kunako mwaka 2011 akateuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa Askofu mkuu na kubahatika kufanya kazi nchini Pakistan na Msumbiji.

Katibu mkuu msaidizi wa Vatican ni kiongozi anayeshughulikia nyaraka zinazotolewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro; masuala ya uteuzi wa nyadhifa mbali mbali katika Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na taasisi za Vatican katika ujumla wake. Ni kiongozi anayeshughulikia na kuhariri nyaraka za Vatican pamoja na kusambaza taarifa mbali mbali za shughuli zinazotekelezwa na Baba Mtakatifu pamoja na viongozi wa Vatican katika ujumla wao! Katibu mkuu msaidizi wa Vatican ndiye mwenye dhamana ya kushughulikia masuala ya kawaida pamoja na kuratibu hija za kichungaji zinazotekelezwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

16 October 2018, 15:10