Kanuni maadili na utu wema ni msingi wa kuondokana na vitisho vya mashambulizi ya silaha za kinyuklia. Kanuni maadili na utu wema ni msingi wa kuondokana na vitisho vya mashambulizi ya silaha za kinyuklia. 

Utekelezaji wa kanuni maadili usaidie kuondokana na vitisho vya mashambulizi ya kinyuklia!

Umoja wa Mataifa unapaswa kwenda zaidi si tu kwa kuzuia, bali pia kuhakikisha kwamba, mitambo ya kuchakata nguvu za kinyuklia inadhibitiwa zaidi kwa ajili ya usalama, ustawi na maendeleo ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, akichangia hoja kwenye Mkutano mkuu wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa amekazia umuhimu wa kudhibiti silaha za kinyuklia kutokana na madhara yake makubwa kwa ustawi, maendeleo na mafungamano ya kijamii. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujikita katika utekelezaji wa kanuni maadili na utu wema, ili kuondokana na vitisho vya mashambulizi ya silaha za kinyuklia.

Umoja wa Mataifa unapaswa kwenda zaidi si tu kwa kuzuia, bali pia kuhakikisha kwamba, mitambo ya kuchakata nguvu za kinyuklia inadhibitiwa zaidi kwa ajili ya usalama, ustawi na maendeleo ya wengi. Askofu mkuu Auza anawashauri wajumbe kushikamana katika mambo msingi yanayogusa mchakato wa kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa; kwa kusimamia kikamilifu Mkataba wa Kimataifa wa kupiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za kinyuklia duniani uliotiwa mkwaju hapo tarehe 20 Septemba 2017.

Vijana wa kizazi kipya wana kiu ya kuona kwamba, ndoto ya amani inatekelezwa kwa ukamilifu zaidi Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwekeza katika sera na mikakati ya ulinzi na usalama na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote badala ya kuendekeza malumbano yasiyokuwa na tija wala mashiko kati ya mataifa! Silaha ya kinyuklia kama zikitumika zitaharibu mafanikio yote yaliyokwisha kufikiwa na Jumuiya ya Kimataifa hadi wakati huu. Kuna haja ya kuwa na uongozi wa kimataifa utakaokuwa na nguvu ya kisiasa na nyenzo zitakazo mwezesha kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Askofu mkuu Bernardito Auza anasema, malumbano kuhusu utengenezaji na umiliki wa silaha za kinyuklia kati ya Korea Kaskazini na Iran ni tishio kwa usalama wa Jumuiya ya Kimataifa. Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kupounguza kama sio kuliza kabisa vitisho vya vita, ili hatimaye, kujenga tabia na hali ya kuheshimiana. Anaendelea kufafanua kamba, kumekuwepo na maendeleo mazuri ya kudhibiti silaha za kinyuklia kati ya Korea ya Kusini na Kaskazini, jambo linalotia matumaini.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, Mashariki ya Kati haigeuzwi kuwa ni uwanja wa majaribio ya silaha za kinyuklia. Fedha itakayokuwa imekolewa kutokana na udhibiti wa nguvu za kinyuklia itumike katika maboresho ya maisha ya wananchi wake sanjari na kuwasaidia maskini kutoka katika nchi changa duniani.

19 October 2018, 14:58