Wakuu wa Shirika Na Wawakilishi wa Wakarmeli Peku Wakutana na Papa Francisko
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Wakuu wa Shirika na Wawakilishi wa Wakarmeli Peku “The Discalced Carmelite Nuns” wamekusanyika mjini Roma ili kupitia Katiba ya Shirika lao kwa kuendelea kusoma alama za nyakati, ili kukidhi mahitaji halisi ya watawa hawa mintarafu maisha ya kijumuiya, huku wakijiaminisha chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu katika sala na mang’amuzi ya ndani. Ni wakati muafaka wa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwachangamotisha kugundua lugha mpya na njia mpya zinazotoa ari na mwamko katika maisha ya taamuli wanayoitiwa na Mungu, ili waweze kuyakumbatia, ili hatimaye, karama ya Wakarmeli ilete mvuto kwa nyoyo nyingi, kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ustawi, maendeleo na mafao ya Mama Kanisa. Kimsingi mapitio ya Katiba ya Shirika ni mchakato unaopania kupitia ya kale, kwa kuangalia ya mbeleni, ili moto wa maisha ya taamuli uendelee kuwaka na hivyo kuleta joto ndani ya Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake. Kumbukumbu hai ya historia ya Katiba yao ambayo imekuwepo kwa miaka mingi ni amana na utajiri unaopaswa kuendelea kuwa wazi kwa Roho Mtakatifu, kama upyaisho wa Injili na alama ambazo Mwenyezi Mungu anawaonesha watu wake mintarafu uzoefu, mang’amuzi pamoja na changamoto za maisha. Wakuu wa Shirika na Wawakilishi wa Wakarmeli Peku, Alhamisi tarehe 18 Aprili 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amekazia umuhimu wa watawa wa ndani katika maisha na utume wa Kanisa kama ilivyokuwa kwa Maria na Martha; matumaini yanayopata chimbuko lake katika Injili inayowakirimia furaha katika maisha ya taamuli katika historia ya sasa pamoja na kuwajalia nguvu ya kuweza kuyaangalia ya mbeleni kwa matumaini.
Baba Mtakatifu anasema, kama watawa ndani wanatambua kinzani na mivutano kati yao inayokuwa ni sababu ya wao kujitenga na malimwengu na ile nguvu inayotaka kuwatumbukiza katika malimwengu. Mbali na kutafuta kimbilio katika faraja za maisha ya kiroho, watambue kwamba, wananaswa na upendo wa Kristo unaowaunganisha naye, ili hatimaye, upendo wake uweze kueneza uwepo wake wote na hivyo kujidhihirisha katika yote wanayoyasema na kutenda. Njia ya kutafakari, kimsingi ni njia ya upendo na hutumika kama ngazi inayomwinua mwamini kwa Mungu na wala si kwa ajili ya kutengwa na malimwengu, bali kuwajengea msingi zaidi wa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo wa Mungu ulioko ndani mwao. Hili ndilo somo ambalo, kwa hekima na imani yake thabiti, Mama yao Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu alipenda kuwafundisha. Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu alikuwa na hakika kwamba muungano wa fumbo na wa ndani ambao Mungu huifungia nafsi nafsi yake, “kuitia muhuri,” kana kwamba, kwa upendo wake, unapenya na kubadilisha maisha yao yote, bila kuwaondoa kutoka kwenye majukumu yao ya kila siku na hivyo kujificha katika maisha ya kiroho peke yake. Alikazia ukimya na maisha ya sala; utume na huduma kwa Mama Kanisa. Kimsingi alikazia kazi na sala kama ilivyokuwa kwa Watakatifu Martha na Maria, walivyokuwa wanamhudumia kwa ukarimu Kristo Yesu alipowatembelea nyumbani kwao. Wanapaswa kuhakikisha kwamba licha ya kusikiliza, kama watawa wa ndani wanapaswa kuvuta roho za watu ili waweze kuokolewa na hatimaye, kumsifu Mungu milele yote.
Kwa njia hii maisha ya taamuli hayataweza kuhatarishwa wala kuzoroteshwa kutoka katika shughuli na maisha ya kila siku na badala yake, yataendelea kutoa mwanga wa ndani unaohitajika kwa utambuzi. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, huu ndio mwanga unaohitajika kurekebisha Katiba, kwa kushughulikia matatizo, changamoto na fursa katika maisha ya monasteri na yale ya kijamii. Nuru hii si nyingine bali ni tumaini linalobubujika kutoka katika Injili Tumaini la Kiinjili linatofautiana na udanganyifu unaotegemea mahesabu ya kibinadamu. Huu ni mwaliko wa kujikabidhi kwa Mwenyezi Mungu, kujifunza kusoma alama za nyakati ili kutambua wakati ujao; sanjari na kuwa na ujasiri wa kufanya maamuzi fulani ya ujasiri na hatari, hata bila kujua hatimaye yake. Zaidi ya yote, inamaanisha kutofikiria tu kwa maneno ya kibinadamu na ya kujihami wakati wa kutafakari juu ya kuhifadhi au kufunga monasteri, juu ya miundo ya maisha ya jamii, juu ya miito. Mikakati ya kujilinda mara nyingi ni tunda la kutamani sana mambo yaliyopita, ambapo tumaini la kiinjili huwapatia furaha katika kutafakari historia yao hadi sasa, lakini pia huwawezesha kutazama mbele kwa siku zijazo. Baba Mtakatifu anawataka Wakarmeli Peku kuyaangalia ya mbeleni kwa matumaini ya Kiinjili, katika uhuru pamoja na kujizamisha kabisa kwa uwepo wa Kimungu, unaowajaza furaha isiyokuwa na kifani.