Papa:msizoee vita ni mambo ya kutisha sana dhidi ya Mungu na wanadamu
Vatican News.
Vitisho, “vitisho vikubwa sana”, dhidi ya Mungu na dhidi ya mwanadamu. Hivi ndivyo vita ambavyo Papa kwa mara nyingine tena amesisitiza na kulaani migogoro inayoendelea duniani ambayo tayari Dominika 22 Oktoba 2023 mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Mtakatifu Petro, alikuwa ameifafanua kuwa ni “kushindwa.” Hayo tena anaeleza kwenye X, kupitia akaunti yake ya @Pontifex katika lugha tisa, ambapo tunasoma kuwa: “Hatupaswi kuzoea vita, vita vyovyote. Hatupaswi kuruhusu mioyo na akili zetu kufa ganzi katika uso wa kurudiwa kwa maovu haya makubwa dhidi ya Mungu na wanadamu.”
Mivutano mingine duniani
Wito mwingine mpya, kwa hiyo, kutoka kwa Papa ambao unaungana na shutuma zilizotolewa tangu mwanzo wa upapa wake na kusisitiza kwa nguvu zaidi katika miezi ya uvamizi wa Warusi huko Ukraine na sasa mivutano ya kuibuka tena mashambulizi na vurugu katika Mashariki ya Kati. Wasiwasi ambao Papa pia alishirikisha katika simu aliyompigia Rais wa Marekani Joe Biden, Dominika Oktoba 22, na ambaye alitembelea Israel hivi karibuni, kwamba “kuna haja ya kutambua njia za amani.”
Wewe sio peke yako ni maneno ya kinabii
Na kwa kuzingatia machafuko ambayo ulimwengu unashuhudia, maneno ya Papa dhidi ya vita katika Kitabu cha “Wewe sio peke yako” ni maneno ya kinabii. Changamoto, majibu, na matumaini,ni katika mahojiano ya kitabu yaliyoandikwa na waandishi wa habari Francesca Ambrogetti, mkuu wa zamani wa Ansa nchini Argentina na Sergio Rubin, wa gazeti la El Clarin. Kitabu hicho kilikuwa tayari kimechapishwa katika mwezi Februari nchini Argentina kikiwa na kichwa El Pastor, yaani Mchungaji. Kwa njia hiyo Jumanne tarehe 24 Oktoba 2023, toleo la lugha ya Kiitaliano litakuwa kwenye maduka ya vitabu na mchapishaji Salani.
Ni janga,kupoteza kumbukumbu ya vita ya II ya Dunia
Katika dondoo za kitabu hicho Papa anasema: “Mwanzoni mwa upapa nilisema kwamba tulikuwa tukipitia Vita vya Kidunia vya Tatu vilivyomegeka vipande vipande, kisha nikabainisha kwamba vipande hivi vilikua vikubwa na sasa nadhani yote ni sehemu moja kubwa,” Papa anasema katika kifungu cha mazungumzo, yaliyoripotiwa na Ansa. “Ninaendelea kuamini kuwa ni janga kubwa kupoteza kumbukumbu ya Vita vya Pili vya Dunia. Wakati mmoja, nikitazama watawala wa nchi zilizoshiriki katika vita wakati wa ukumbusho wa kutua kwa Normandy, nilifikiri kwamba walipaswa kulia. Karibu watu elfu 30 walikufa huko peke yao. Vita ni matokeo ya mfululizo wa wazimu.”