Sherehe ya Pentekoste: Sala za Waamini Kumwomba Roho Mtakatifu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa kwa maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste, Siku ya Kuzaliwa kwa Kanisa na Siku ya Waamini walei anahitimisha kipindi cha Pasaka. Hii ni fursa ya kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kumshusha Roho Mtakatifu kwa Kanisa na kwa ulimwengu. Ni katika muktadha huu, Mama Kanisa amesali na kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kulijalia Roho Mtakatifu, Roho wa umoja na amani katika Kanisa lake. Katika ulimwengu uliojeruhiwa na majeraha, migogoro na vita, Kanisa liangaze kama Sakramenti ya utakatifu na muungano na watu wafikie ufalme wake wa haki, wa upendo na amani. Sr. Maria Veronica Mwanandenga wa Shirika la Masista Waabuduo Moyo Mtakatifu wa Yesu, kutoka Jimbo Katoliki la Mbeya, Tanzania ndiye aliyesoma sala ya waamini wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste, Dominika tarehe 28 Mei 2023 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Ibada iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko.
Kanisa limesali pia kwa ajili mihimili ya Uinjilishaji. Ili neema inayobubujika kutoka katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa awashe moto wa Roho Mtakatifu aliyewashukia Mitume katika tukio la ajabu, Siku ile ya Pentekoste. Kanisa limesali na kuwaombea waamini walioimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara, waweze kufanana na Kristo Yesu na wawe na furaha kupokea mwaliko wa kumtumikia Kristo Yesu ndani ya Kanisa lake, kwa kuwa ni mashuhuda wa Injili hususan miongoni mwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii Kanisa limesali na kuwaombea pia wanachama wa Mashirika ya Kikanisa na Vyama vya Kitume ili Mwenyezi Mungu Muumbaji awawashie moto wa Roho wake Mtakatifu wanachama wake wote. Ili karama zao mbalimbali zinazopata asili na chanzo chake kutoka kwa Roho Mtakatifu zizae matunda mema kwa Kanisa na kwa ulimwengu katika ujumla wake. Katika Ibada hii ya Misa Takatifu Sherehe ya Pentekoste kwa Mwaka 2023, Kanisa limesali na kuwaombea wale ambao bado hawamwamini Mwenyezi Mungu, ili Roho Mtakatifu aweze kuwaangazia nyoyo zao, ili hatimaye waweze kuona alama za uzuri wake katika maisha yao, huku wakivutwa na ushuhuda wa waamini waweze kumfahamu Mungu mmoja na Baba wa wote.