Viongozi wakuu wa Makanisa wataendelea kuwasindikiza watu wa Mungu Sudan ya Kusini katika mchakato wa upatanisho, haki na amani chini ya maombezi na tunza ya Bikira Maria Malkia wa amani, Viongozi wakuu wa Makanisa wataendelea kuwasindikiza watu wa Mungu Sudan ya Kusini katika mchakato wa upatanisho, haki na amani chini ya maombezi na tunza ya Bikira Maria Malkia wa amani,   (Vatican Media)

Viongozi Wakuu wa Makanisa Kusindikiza Mchakato wa Upatanisho Sudan ya Kusini

Papa Francisko, Askofu mkuu Justin Welby na Mheshimiwa Dr Iain Greenshields Mkuu wa Kanisa la “Presbyterian” la Scotland wataendelea kuwasindikiza watu wa Mungu Sudan ya Kusini katika mchakato wa upatanisho na amani chini ya maombezi na tunza ya Bikira Maria Malkia wa amani, ili aendelee kuwaombea watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini na Afrika katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 5 Februari 2023 mara baada ya Ibada ya Misa Takatifu na Neno la shukrani kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya “John Garang” Juba, Sudan ya Kusini amehitimisha hija yake ya 40 ya Kitume Barani Afrika Barani tayari kurejea mjini Vatican kuendelea na maisha na utume wake. Baba Mtakatifu Francisko alikuwa ameambata na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani na Mheshimiwa Dr Iain Greenshields Mkuu wa Kanisa la “Presbyterian” la Scotland kama kielelezo cha ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika huduma, maisha ya kiroho, damu na sala. Huu kimsingi ni ushuhuda hija ya uekumene wa amani na watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini. Hija ilinogeshwa na kauli mbiu “Wote wawe na umoja” Yn 17:21, changamoto na mwaliko wa kujikita na kuzama katika Injili ya matumaini na amani. Askofu mkuu Stephen Ameyu Martin Mulla wa Jimbo kuu la Juba, Sudan ya Kusini, mara baada ya Misa Takatifu, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko na ujumbe wake, kwa kuwatembelea na kuwafariji katika shida na mahangaiko yao kutokana na madhara ya vita, alama ya mshikamano wa udugu wa kibinadamu na watu wa Mungu Sudan ya Kusini wanaotamani amani na utulivu vikitawala tena. Baba Mtakatifu amewatembelea ili kuwakumbusha watu wa Mungu Sudan ya Kusini pamoja na Sudan Kongwe umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kudumisha amani na mafao ya wengi sanjari na upatanisho kama sehemu ya mchakato ya amani ya kudumu, changamoto aliyoitoa kunako mwaka 2019 kwa kuwapigia magoti viongozi wa Serikali kujikita katika mchakato wa amani, ambao umekuwa ukisua sua kwa muda mrefu.

Viongozi wakuu wa Makanisa watasindikiza mchakato wa upatanisho
Viongozi wakuu wa Makanisa watasindikiza mchakato wa upatanisho

Askofu mkuu Stephen Ameyu Martin Mulla anasikitika kusema kwamba, vita Sudan ya Kusini imesababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao; kuna watu wengi wamepoteza maisha, makazi ya watu kuchomwa moto na kubomolewa; mazao mashambani na mifugo kuporwa. Hali hii imepelekea watu wengi kuikimbia nchi yao ili kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Kuna mamilioni ya watu wasiokuwa na makazi maalum wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi. Ni vyema wananchi wakajikita katika mchakato wa ujenzi wa amani kwani vita ina madhara makubwa katika maisha ya watu. Sudan ya Kusini na Sudan Kongwe, licha ya historia ngumu ya nchi zao, lakini wamebahtika kuadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya Imani Katoliki na matunda ya Uinjilishaji huu ni watakatifu Daniel Comboni na Mtakatifu Josephine Bakhita. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Daniele Comboni Alizaliwa huko Limone sul Garda, Italia 15 Machi 1831 na kufariki dunia mjini Khartoum, Sudan, tarehe 10 Oktoba 1881), Muasisi wa Shirika la Wamisionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu na Shirika la Masista wa Afrika, wanaofahamika sana kama Wamisionari Wakomboni na Masista Wakomboni. Alitangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa mtakatifu tarehe 5 Oktoba 2003.

Wananchi wa Sudan ya Kusini wana kiu ya haki na amani
Wananchi wa Sudan ya Kusini wana kiu ya haki na amani

Mtakatifu Josefina Bakhita maana yake “Bahati” alizaliwa kunako mwaka 1868 huko mjini Darfur, Sudan Kongwe. Akatekwa nyara na “watu wasiojulikana” akauzwa utumwani, na hatimaye, akanunuliwa na Balozi wa Italia mjini Khartoum aliyempeleka mjini Venezia. Akafundishwa katekesi na hatimaye, kubatizwa. Baadaye alijiunga na Shirika la Mabinti wa Upendo wa Mtakatifu Madgalena wa Canossa akijitoa sadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma. Alifariki dunia tarehe 8 Februari 1947 huko Schio, Italia. Mtakatifu Yohane Paulo II akamtangaza Josefina Bakhita kuwa Mwenyeheri tarehe 17 Mei 1992, na hatimaye, akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe Mosi Oktoba, mwaka 2000 katika maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo. Katika maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mtakatifu Josefina Bakhita, kunako mwaka 2015, Kanisa likaanzisha Siku ya Kimataifa ya Sala na Tafakari ili kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo inayoendelea kudhalilisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Kuna Mashuhuda wa imani kutoka katika Kanisa mahalia waliosadaka maisha yao kama ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake katika Vita ya kwanza ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan inayojulikana sana kama “Anyanya One” ni Bwana William Deng, Padre Saturlino Ohure pamoja na Padre Leopoldo Anyuar. Mapigano yaliyozuka hivi karibuni yamepelekea kuibuka tena kwa mashuhuda wa imani. Hawa ni Sr. Veronika Teresa Rackova, SSpS, mtawa na daktari wa binadamu aliyeuwawa kikatili tarehe 16 Mei 2016 alipokuwa anatekeleza utume wake kwenye Jimbo Katoliki la Yei. Sr Mary Abbud na Sr Regina Roba wa Shirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu waliuwawa kikatili tarehe 16 Agosti 2021 walipokuwa wakitoka Jimbo kuu la Juba kuadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Parokia ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni, Loa, Jimbo Katoliki la Torit. Sudan ya Kusini ni nchi ambayo imesheheni mateso na mahangaiko makubwa ya watu, kumbe, amani na upatanisho ni muhimu sana kwa ajili ya mustakabali wa watu wa Mungu nchini humo. Watu wa Mungu Sudan ya Kusini wanataka amani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu mwenyewe aliyewaambia Mitume wake “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.” Yn 14:27. Hii ni amani inayoongozwa na ukweli na upendo. Hivi ndivyo Askofu mkuu Stephen Ameyu Martin Mulla alivyohitimisha shukrani za watu wa Mungu kutoka Sudan ya Kusini kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na ujumbe wake.

Watu wa Mungu wanataka amani kutoka kwa Kristo Yesu
Watu wa Mungu wanataka amani kutoka kwa Kristo Yesu

Baba Mtakatifu Francisko akitoa neno la mwisho, amewashukuru watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini kwa kwa sadaka na majitoleo yao ili kuhakikisha kwamba, anafanikisha hija ya 40 ya Kitume Barani Afrika na kwa namna ya pekee kabisa Sudan ya Kusini. Anawashukuru wale wote waliotoka ndani na nje ya Sudan ya Kusini ili kushiriki katika hija uekumene wa amani na matumaini, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Josephine Bakhita, “Mwanamke wa shoka” aliyebahatika kwa neema na baraka ya Mwenyezi Mungu kugeuza mateso na mahangaiko yake yote kuwa ni chemchemi ya Injili ya matumaini iliyogeuka hatimaye na kuwa ni mbegu ya matumaini. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wanawake wote wa Sudan ya Kusini, kwa kuendelea kuwa ni kielelezo cha matumaini licha mateso, changamoto na fursa mbalimbali wanazokumbana nazo katika maisha yao ya kila siku. Watu wateule wa Mungu wataumbe kwamba, wanathaminiwa na kuhifadhiwa katika moyo wa Baba Mtakatifu na nyoyo za watu wengine sehemu mbalimbali za dunia. Amewaombea amani na matumaini watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini. Baba Mtakatifu Francisko, Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani na Mheshimiwa Dr Iain Greenshields Mkuu wa Kanisa la “Presbyterian” la Scotland wataendelea kuwasindikiza watu wa Mungu Sudan ya Kusini katika mchakato wa upatanisho, haki na amani chini ya maombezi na tunza ya Bikira Maria Malkia wa amani, ili aendelee kuwakumbuka na kuwaombea watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini na Afrika katika ujumla wake. Hawa ni watu wanaoteseka kutokana na: vita, madhulumu, magonjwa na umaskini. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema kamwe wasikubali kupoteza matumaini na amani.

Bakhita 2023

 

 

05 February 2023, 16:12