Mkutano wa Vijana wa Taizè 2022-2023: Maisha ya Kiroho na Mshikamano wa Upendo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Zaidi ya vijana 5, 000 wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè kutoka sehemu mbalimbali Barani Ulaya, kuanzia tarehe 28 Desemba 2022 hadi tarehe 1 Januari 2023 wanakusanyika mjini Rockstock, nchini Ujerumani, ili kuadhimisha Mkutano wao wa 45 Kimataifa unaonogeshwa na kauli mbiu “Maisha ya Kiroho na Mshikamano, “Inner Life and Solidarity.” Vijana hawa katika umoja na ushirika wao; licha ya tofauti zao msingi, wanafanya hija ya kiekumene kimataifa, ili kuombea amani duniani. Mkutano huu ni kielelezo cha upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na watu wote wa Mungu wanaoendelea kuathirika kutokana na vita, kinzani, misigano na mipasuko ya kijamii, bila kusahau madhara makubwa ya mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kusigina utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa kuwatumbukiza watu katika baa la njaa, magonjwa na umaskini wa hali na kipato. Vijana 300 kutoka nchini Ukraine wanashiriki katika mkutano huu anasema, Fra Alois, Mkuu wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè kwamba, idadi kubwa ya vijana kutoka Ukraine hawakuweza kushiriki kutokana na vita inayoendelea kati ya nchi hii na Urusi. Hawa ni vijana wenye umri kati ya miaka 18-35. Wanashiriki Sala, Ibada ya Misa Takatifu na Tafakari katika makundi madogo madogo. Kati ya tema zinazojadiliwa ni pamoja na imani, maisha ya kiroho, mabadiliko ya tabianchi; dhamana na wajibu wa vijana wa kizazi kipya katika kutekeleza Mafundisho Jamii ya Kanisa, Kazi ya Uumbaji na Sanaa.
Jumamosi tarehe 31 Desemba 2022, utakuwa ni mkesha wa nguvu, kwa ajili ya kuombea amani duniani na baadaye kutafuatia tamasha la muziki, kila nchi ikishirikisha wimbo mmoja. Baadaye, tarehe Mosi, Januari 2023 vijana watashiriki katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu sanjari na maadhimisho ya Siku 56 ya Kuombea Amani Duniani. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani unanogeshwa na kauli mbiu “Hakuna mtu anayeweza kujiokoa mwenyewe. Kupambana na UVIKO-19 na kwa pamoja kujielekeza kwenye njia za amani.” Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe huu anagusia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa makini kwa kujikita katika haki na ukweli; madhara yaliyosababishwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; changamoto na mambo mazuri yaliyoibuliwa na UVIKO-19 na kwamba, walimwengu waendelee kujifunza kutokana na historia ya maisha ya mwanadamu. Sherehe ya Mwaka Mpya wa 2023 itakuwa ni fursa kwa vijana wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè kushiriki pia chakula cha mchana pamoja na wenyeji wao. Ulinzi na usalama wa vijana hawa ni kati ya mambo yaliyopewa kipaumbele cha pekee na waandaaji wa mkutano huu.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Edgar Peña Parra, Katibu mkuu Msaidizi wa Vatican anapenda kuwapongeza vijana wa kiekumene kwa kukutana mubashara baada ya kuvuka mawimbi mazito ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 uliowazuia kukutana mubashara mwaka 2021-2022. Changamoto ya vita Barani Ulaya ni kashfa inayoendelea kuwahuzunisha watu wengi ndani nan je ya Bara la Ulaya. Maisha ya kiroho na mshikamano, ni tema inayowahamasisha vijana wa kizazi kipya kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, bila kuwakatia tamaa walimwengu. Baba Mtakatifu anawaalika vijana kukuza, kudumisha na kuboresha maisha yao ya ujana, kwa kujikita katika mshikamano wa udugu wa kibinadamu; kwa kuondokana na hofu ya wageni isiyokuwa na mashiko; kwa kujiondoa katika upweke hasi na kuendelea kujielekeza katika ujenzi wa haki, amani na maridhiano duniani. Vijana wasimame kidete kupinga mifumo yote ya unyanyasaji, tayari kuonesha ukomavu unaowawezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo.
Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pia kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Huu ni utamaduni wa watu wa Mungu kusikilizana kwa makini! Ni kusikiliza Neno la Mungu, ili kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha katika uhalisia na vipaumbele vya maisha ya waamini. Kusikiliza ni kujenga utamaduni wa kusali pamoja na Neno la Mungu, “Lectio Divina.” Vijana wa kizazi kipya wanahamasishwa kusali pamoja na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu.
Kwa upande wake, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol anagusia umuhimu wa vijana kukutana mubashara, ili kupyaisha maono na matamanio halali ya vijana kwa mwaka 2023; kwa kukazia ushirika na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo; kielelezo cha imani tendaji. Waamini wajitahidi kujenga na kudumisha umoja na ushirika unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Maandiko Matakatifu yanasema, “Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo. Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga.” Efe 2: 13-14. Patriaki Bartolomeo wa kwanza anakaza kusema, hii ni changamoto kwa waamini kujenga na kudumisha umoja na ushirika, kama njia ya kukutana na Mwenyezi Mungu. Ushirika wa waamini ni jambo ambalo linapaswa kuvaliwa njuga na waamini wote kama njia ya kukoleza jitihada za majadiliano ya kiekumene.
Nalo Fungamano la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani, “The Lutheran World Federation”, (LWF) ambalo linayashirikisha Makanisa 149, yakiwa na zaidi ya waamini milioni 77, linakazia kwa namna ya pekee upendo unaomwilishwa katika safari ya maisha ya kila siku, kwa kujielekeza katika ujenzi wa haki, amani na upatanisho wa kweli, daima wakisimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Huu ni muda muafaka wa kusali na kuombea haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu nchini Ukraine na Rusia bila kusahau sehemu mbalimbali za dunia ambamo, bado vita, kinzani na mipasuko ya kijamii inapekenya utu, heshima na haki msingi za binadamu.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutteres ameipongeza Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè inayosimika maisha na utume wake katika nguzo ya matumaini, amani na huruma na kwamba, hata yeye alipokuwa bado mwanafunzi alikuwa akihudhuria mikutano kama hii. Kwa sasa Jumuiya ya Kimataifa inakabiliana na changamoto pevu. Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 umeibua udhaifu wa binadamu na ukosefu wa haki msingi; vita, kinzani na ukosefu wa usawa katika medani mbalimbali za maisha ni kati ya mambo yanayoendelea kuibuliwa kwa sasa; hotuba za chuki na uhasama sanjari na habari za kughushi ni kati ya mambo yanayowatumbukiza walimwengu katika katika mipasuko ya kijamii na maafa, hali inayohatarisha maisha ya binadamu katika ujumla wake. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutteres anasema, inafurahisha kuona na kusikia kwamba, vijana wa kizazi kipya wamekuwa mstari wa mbele kudai mabadiliko, jambo ambalo linapaswa kuungwa mkono, kwa ajili ya mustakabali wa Jumuiya ya Kimataifa kwa sasa na kwa siku za mbeleni. Ni katika muktadha huu, Umoja wa Mataifa umeanzisha Ofisi ya Vijana Kimataifa. Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika mchakato wa ujenzi amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu ili hatimaye, kujenga ulimwengu unaosimikwa katika haki, maendeleo fungamani ya binadamu na ulimwengu ambao kwa hakika ni jumuishi!