Jukwaa la Kazi la Laudato si, “Laudato si Plaform of Action, LSAP”, lilizinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Mei 2021. Jukwaa la Kazi la Laudato si, “Laudato si Plaform of Action, LSAP”, lilizinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Mei 2021. 

Papa Francisko: Jukwaa la Kazi la Laudato si: Wongofu wa Kiikolojia & Mfumo Mpya wa Maisha

Jukwaa la Laudato si ni jibu la kusikiliza na kujibu kwa makini kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini, ili kuwaletea watu matumaini. Hii ni changamoto ya watu kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira nyumba ya wote. Juhudi hizi ziende sanjari na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii kwa sababu hawa ndio waathirika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jukwaa la Kazi la Laudato si, “Laudato si Plaform of Action, LSAP”, lilizinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Mei 2021 kama sehemu ya mchakato wa Kanisa la Kiulimwengu kuunganisha nguvu pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, ili kutekeleza kwa vitendo wito wa Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Huu ni mwaliko wa kudumisha ushirikiano na mafungamano ya kina yanayojikita katika: upole, huruma sanjari na kuwajali wengine dhidi ya biashara haramu ya binadamu pamoja na viungo vyake; kwa kuwajali maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni wito wa kujikita katika msamaha kama kielelezo cha upendo na kama kinavyofafanuliwa na Mtakatifu Francisko wa Assisi katika utenzi wake wa “Laudato si.” Huu ni mwaliko wa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kweli na ya dhati kabisa, kwa kujikita katika haki jamii ili kutafuta suluhu ya matatizo, fursa na changamoto za kijamii katika ulimwengu mamboleo. Rej. Laudato si, 91.

Toba na wongofu wa kiikolojia ni muhimu katika utunzaji wa mazingira
Toba na wongofu wa kiikolojia ni muhimu katika utunzaji wa mazingira

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 13 Novemba 2022 amewakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, tarehe 14 Novemba 2022 Jukwaa la Kazi la Laudato si, “Laudato si Plaform of Action, LSAP”, linafanya kumbukizi ya mwaka mmoja tangu kuzinduliwa kwake. Lengo ni kusaidia mchakato wa toba na wongofu wa kiikolojia na mfumo wa maisha. Jukwaa hili hadi wakati huu, linawashirikisha wanachama zaidi ya elfu sita. Hawa ni watu binafsi, familia, mashirika na vyama vya kitume, makampuni, mashirika ya kitawa na kazi za kitume, wafanyakazi katika sekta ya utamaduni na afya. Huu ni mchakato ambao utekelezaji wake unafanyika katika awamu mbalimbali kama jibu la kusikiliza na kujibu kwa makini kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini, ili kuleta matumaini kwa kizazi cha sasa na kile kijacho! Hii ni changamoto kwa waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira nyumba ya wote. Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii kwa sababu hawa ndio waathirika wakuu wa mabadiliko ya tabianchi sehemu mbalimbali za dunia!

Kuyeyuka kwa barafu kunaongeza kina cha bahari hatari kwa maisha ya watu
Kuyeyuka kwa barafu kunaongeza kina cha bahari hatari kwa maisha ya watu

Mazingira yanaonesha mahusiano na mafungamano yaliyopo kati ya maumbile na jamii inayoishi ndani mwake. Binadamu ni sehemu ya mazingira kumbe, anawajibu wa kushirikiana kikamilifu katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Utambuzi wa sababu zinazofanywa sehemu fulani kuchafuliwa unahitaji elimu jamii, uchumi, mfumo wa tabia na jinsi mtu anavyoyaelewa maumbile. Kumbe, mifumo ya kijamii na maumbile ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana. Sera na mikakati ya kuelekea ufumbuzi wa migogoro inadai njia halisi ya kupambana na baa la umaskini, kurejesha utu, heshima na haki msingi kwa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii sanjari na jamii kuendelea kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Rej. Laudato si, 139. Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa elimu ya ikolojia na maisha ya kiroho, mambo msingi yanayomwezesha mwanadamu kufahamu asili yake, mahusiano na mafungamano ya kijamii na mustakabali wa jamii ambao kila mtu anapaswa kuushiriki. Kuna changamoto kubwa ya kiutamaduni na maisha ya kiroho, changamoto na mwaliko wa kujikita katika safari ndefu ya wongofu wa kiikolojia na upyaisho wa maisha ya watu. Mahusiano haya yanafumbatwa katika utambuzi wa uwepo angavu wa Mungu, jirani pamoja na dunia yenyewe. Rej. Laudato si, 66, 202, 220 na 221.

Utunzaji bora wa mazingira udumishe upendo kwa Mungu na jirani
Utunzaji bora wa mazingira udumishe upendo kwa Mungu na jirani

Kama sehemu ya mchakato wa kufunga rasmi maadhimisho ya “Mwaka wa Laudato si”, tarehe 25 Mei 2021, Baba Mtakatifu Francisko alitangaza kuzinduliwa kwa Jukwaa la Kazi la Laudato si, “Laudato si Plaform of Action, LSAP”, safari shirikishi ya miaka saba, kama sehemu ya mchakato wa kujizatiti kikamilifu katika maendeleo na ikolojia fungamani. Kumbe, kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kila mtu akichangia kadiri ya nafasi na uwezo wake. Ni mwaliko wa kushirikishana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna haja ya kuanzisha majadiliano mapya kuhusu namna ya kuujenga mustakabali wa dunia hii, kwa kuwahusisha watu wote kwa sababu changamoto za mazingira zinawahusu na kuwaathiri watu wote. Vipaji vya kila mmoja na ushiriki wake vinahitajika kama vyombo vya Mungu kwa ajili ya kuyatunza maumbile, kila mmoja kadiri ya utamaduni, mang’amuzi, shughuli na vipaji vyake. Rej. “Laudato si”, 14. Jukwaa la Kazi la Laudato si, “Laudato si Plaform of Action, LSAP”, linatekelezwa katika kipindi cha miaka saba.

Laudato si ni dira na mwongozo wa utunzaji bora wa mazingira.
Laudato si ni dira na mwongozo wa utunzaji bora wa mazingira.

Mwaka wa kwanza ni mchakato wa ujenzi wa jumuiya, ushirikishanaji wa rasilimali na utengenezaji wa sera na mikakati ya utekelezaji kadiri ya mwono wa ikolojia fungamani, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na kilio cha maskini; kwa kujielekeza katika uchumi unaosimikwa katika ikolojia; kwa kujikita katika mtindo wa maisha ya kawaida sanjari na kuendelea kukazia elimu na tasaufi ya ikolojia pamoja na ushirikishwaji wa jumuiya! Mwaka wa Saba, utatumika kumsifu na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya Kazi ya Uumbaji. Utekelezaji wa sera na mikakati ya Jukwaa la Kazi “Laudato si Plaform of Action, LSAP”, unafanyika mintarafu dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Kuna Kamati kuu ya “Laudato si Plaform of Action, LSAP”, inayoratibiwa na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu kwa kushirikiana na Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, Umoja wa Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Kimataifa, USG na UISG, CIDSE, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Kanisa Katoliki, Vyama na Mashirika ya Kitume, “Mtandao wa Kanisa Amerika ya Kusini”, (Pan-Amazon Ecclesial Network of the Latin American Church, REPAM” pamoja na makundi mbalimbali kutoka Barani Afrika na Asia katika ujumla wake.

Kuna haja ya kujikita katika wongofu wa kiikolojia
Kuna haja ya kujikita katika wongofu wa kiikolojia

Sekta ya familia inaongozwa na Wafokolari. Sekta ya Parokia na Majimbo na Mabaraza ya Maaskofu iko chini ya Shirika la Misaada na Maendeleo Kimataifa la Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza, CAFOD. Sekta ya shule inaongozwa na Shirika la Mtakatifu Bosco lijulikanalo kama “Don Bosco Green Alliance” pamoja na Kikundi cha Laudato si kutoka Ufilippini. Sekta ya Shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu inaongozwa na Wayesuit na wadau wengine kutoka Vyuo vikuu. Sekta ya Hospiltali itakuwa chini ya Chama cha Afya Cha Wakatoliki nchini India, CHAI, Vyama vya Afya kutoka Marekani na viongozi wengine kutoka sekta ya afya. Sekta ya Uchumi itaratibiwa na “Economy of Francesco” yaani “Uchumi wa Francisko”, CIDSE, VIS, Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC, USG na UISG. Huu ni mchakato unaosimikwa katika majadiliano na utekelezaji wake kama jitihada za makusudi za kuyatunza mazingira, kwa ajili ya sas ana wakati ujao. Kwa habari motomoto unaweza kuangalia kwenye anuani ifuatayo: (www.laudatosi.va).

Jukwaa Laudato si

 

14 November 2022, 16:17