Papa Francisko amekutana na kuzungumza na Ujumbe wa Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol kwa mwaka 2022 Papa Francisko amekutana na kuzungumza na Ujumbe wa Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol kwa mwaka 2022  

Papa: Majadiliano ya Kiekumene Yanogeshe Umoja, Upatanisho na Taalimungu

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kumshukuru kwa dhati Patriaki Bartholomeo wa kwanza kwa wajumbe pamoja na matashi mema aliyomtumia. Amekazia: Mchakato wa upatanisho kati ya Wakristo waliotengana; umuhimu wa ujenzi wa umoja wa Kikristo unaosimikwa katika udugu pamoja na kuendeleza Majadiliano ya Kitaalimungu kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox .

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol kwa mwaka 2022 kwenye Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume na Miamba wa imani uliowasili mjini Roma tangu tarehe 28 Juni hadi tarehe 30 Juni 2022 unaongozwa na Askofu mkuu Ihor Wladimir Getcha wa Jimbo kuu la Telmissos Job. Huyu pia ni Mwakilishi wa Kudumu wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza kwenye Baraza la Makanisa ya Kiekumene na Rais mwenza wa Tume ya Pamoja ya Kiekumene Kimataifa ya Majadiliano ya Kitaalimungu kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox. Ujumbe huu, Alhamisi tarehe 30 Juni 2022 umekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kumshukuru kwa dhati Patriaki Bartholomeo wa kwanza kwa wajumbe waliotumwa na Sinodi Takatifu pamoja na matashi mema aliyomtumia. Amekazia umuhimu wa mchakato wa upatanisho kati ya Wakristo waliotengana; umuhimu wa ujenzi wa umoja wa Kikristo unaosimikwa katika udugu wa kibinadamu pamoja na kuendeleza Majadiliano ya Kitaalimungu kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox baada ya kusitishwa kwa muda wa miaka miwili kutokana na kuzuka kwa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza ni ishara ya umoja wa Kanisa unaoonekana
Ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza ni ishara ya umoja wa Kanisa unaoonekana

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, mabadilishano ya wajumbe kutoka katika Makanisa haya mawili wakati wa Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume pamoja na maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Andrea Mtume, inayopewa uzito wa pekee na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol kama msimamizi wa Kanisa hilo. Hii ni alama inayoonekana katika mchakato wa kukuza majadiliano ya kiekumene. Shukrani zinapaswa kutolewa kwa Fumbo la Utatu Mtakatifu linaloyawezesha Makanisa kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene katika msingi wa udugu wa kibinadamu, ili hatimaye, kuweza kufikia umoja kamili na unaonekana kati ya Makanisa. Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol linajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu Patriaki Athenagoras alipofariki dunia tarehe 7 Julai 1972 huko Istanbul nchini Uturuki. Patriaki huyu ni kati ya viongozi wa Kanisa ambao walijisadaka bila ya kujibakiza kunogesha majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa na ambaye amekuwa ni chanzo cha msukumo wa ndani ambaye alikazia umoja wa Makanisa na Udugu wa Kibinadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anakazia mchakato wa upatanisho miongoni mwa Wakristo, ili kusaidia pia kuwapatanisha watu ambao wako vitani. Wakristo wanapigana wenyewe kwa wenyewe, changamoto na mwaliko kwa Wakristo kuhuzunika kwa kulia na kuwaombolezea waathirika wa vita; raia wanaouwawa bila ya hatia, uharibifu unaofanywa kwenye mazingira na miundo mbinu; kwa wananchi kulazimika yakimbia makazi kwa kuhofia usalama wa maisha yao. Ni mwaliko wa kuwasaidia watakatifu wa Mungu, kama kielelezo na ushuhuda wa upendo kwa maskini, wakimbizi na wahamiaji. Huu ni wito wa kuanza kujizatiti katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho wa kweli. Majadiliano ya kiekumene yanalenga kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika haki na mshikamano. Huu ni mwaliko kwa Wakristo kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu, daima wakijitahidi kuwa ni wakamilifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu. Rej. Mt 5:48. Wakristo watambue kwamba, Kristo Yesu ndiye amani yao aliyawaunganisha na hivyo kuwawezesha kuwa wamoja kwa kubomoa kile kiambaza cha kati kilichokuwa kinawatenganisha.

Majadiliano ya kiekumene yakoleze misingi ya haki, amani na maridhiano
Majadiliano ya kiekumene yakoleze misingi ya haki, amani na maridhiano

Wakristo wawe kweli ni manabii wa Injili ya amani inayosimikwa katika unyenyekevu, sala, ujasiri na “parrhesía.” Baba Mtakatifu Francisko anasema, ishara moja ya matumaini, katika safari ya kuelekea kurejeshwa kwa umoja kamili wa Wakristo, inatokana na mkutano wa Kamati ya Uratibu ya Tume ya Pamoja ya Kimataifa ya Majadiliano ya Kitaalimungu kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox. Lengo ni kurejesha umoja kamili wa Kanisa, unaonekana. Baba Mtakatifu amewashukuru Maaskofu wakuu waliowakirimia wajumbe wa Tume hii ya pamoja wakati wa mkutano wao. Majadiliano ya kitaalimungu yanapania pamoja na mambo mengine, kuibua mwelekeo mpya, ili kuondokana na makosa ya zamani, ili kuyakabili mambo ya sasa na yale yajayo, bila kuelemewa na maamuzi mbele yaliyojitokeza katika maisha na historia ya Kanisa kwa kuyapyaisha kwa sala na ushirikiano, huku Kristo Yesu na Injili yake, vikipewa kipaumbele cha kwanza.

Majadiliano ya Kiekumene
30 June 2022, 15:44