Maadhimisho ya Jubilei ya Familia yatafanyika mwaka 2025 wakati ambapo Maadhimisho ya Siku XI ya Familia Duniani yatakuwa ni mwaka 2028. Maadhimisho ya Jubilei ya Familia yatafanyika mwaka 2025 wakati ambapo Maadhimisho ya Siku XI ya Familia Duniani yatakuwa ni mwaka 2028. 

Maadhimisho ya Jubilei ya Familia 2025 & Siku ya XI ya Familia 2028

Katika Maadhimisho ya Ibada ya Kufunga Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, imetangazwa kwamba, Jubilei ya Familia itaadhimishwa Mjini Roma mwaka 2025 na kwamba, Maadhimisho ya Siku ya XI ya Familia Duniani itakuwa ni Mwaka 2028. Hivi ni vipindi vya neema vinavyopania kugusa undani wa maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” yalizinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Machi 2021 na kuhitimishwa wakati wa kilele chamaadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani mjini Roma, kuanzia tarehe 22 hadi 26 Juni, 2022. Maadhimisho yamenogeshwa kwa kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”. Kardinali Kevin Joseph Farrell, Rais wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha katika hotuba yake ya shukrani kwa Baba Mtakatifu Francisko, katika Ibada ya Kufunga Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, ametangaza kwamba, Jubilei ya Familia itaadhimishwa Mjini Roma mwaka 2025 na kwamba, Maadhimisho ya Siku ya XI ya Familia Duniani itakuwa ni Mwaka 2028. Hivi ni vipindi vya neema vinavyopania kugusa undani wa maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo. Maadhimisho ya Mwaka Furaha ya Upendo Ndani ya Familia kimekuwa ni kipindi muafaka cha kufanya upembuzi yakinifu kuhusu maisha ya ndoa na familia, tayari kuanza mchakato wa maboresho ya utume na shughuli za kichungaji za maisha ya ndoa na familia.

Hii ni changamoto inayohitaji mihimili ya Uinjilishaji iliyofundwa barabara katika maisha na utume wa ndoa na familia. Hawa ni watu wanaotumwa na Mama Kanisa kuhubiri, lakini zaidi kutolea ushuhuda wa imani yao kwa njia ya maisha adili na utu wema, kwa kutambua kwamba, wanaendeleza ile kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo Yesu mwenyewe yapata miaka elfu mbili iliyopita, katika ulimwengu ambao una mwingiliano mkubwa wa watu kutoka katika kila lugha, kabila, jamaa na dini. Familia pia zinapaswa kupata malezi ya awali na endelevu; zisaidiwe na kusindikizwa, ili kukabiliana na changamoto mamboleo zinazoibuliwa katika medani za maisha adili na utu wema; kisiasa, kitamaduni, kijamii na kiuchumi. Familia ni kitovu cha elimu ya uraia mwema na kwamba, maisha ya ndoa na familia ni kielelezo cha: Ukuu, uzuri, utakatifu, ukweli na ushuhuda wa Injili ya familia unaobubujika kutoka katika sura na mfano wa Mungu. Ndani ya familia kuna matatizo na changamoto zake, lakini waamini wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwa kuwajibikiana na kuendelea kujenga mafungamano na ushirika wa Kikanisa.

Maadhimisho ya Jubilei ya Familia ni mwaka 2025
Maadhimisho ya Jubilei ya Familia ni mwaka 2025

Mama Kanisa anawaalika wanandoa kuendelea kujitajirisha kwa tafakari za Mafundisho ya Kanisa kuhusu Ndoa na Familia, ili kuziwezesha familia kuendelea kujiinjilisha na kuinjilisha walimwengu. Wito wa kwanza kwa familia ni utakatifu wa maisha unaofumbatwa katika Injili ya upendo, huruma na msamaha wa kweli; kwa kujiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu, kufunga Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” amekazia kuhusu: uhuru wa ndani unaowataka kutumikiana kwa upendo, kwani unapata chimbuko lake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko kwa Kristo Yesu kwa wafu. Familia ni mahali pa kwanza ambako mtu anajifunza, kupenda, kusamehe na kuhudumia. Wanandoa wakuze na kudumisha mafungamano baina ya kizazi na kizazi ili kurithishana amana na tunu msingi za maisha ya ndoa, familia na imani ya Kikristo. Wanandoa wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Wazazi wajitahidi kuwarithisa watoto wao: imani, maadili na utu wema, ili kukabiliana na changamoto za maisha na hatimaye, wajenge ulimwengu ulio bora zaidi. Wanandoa wawe ni mashuhuda na watangazaji wa upendo, uaminifu na ukweli.

Maadhimisho ya Siku ya XI ya Familia Duniani ni Mwaka 2028
Maadhimisho ya Siku ya XI ya Familia Duniani ni Mwaka 2028

Penye shida, mahangaiko na changamoto za maisha ya ndoa, wanandoa wajitahidi kupokeana, kufahamiana ili kupyaisha upendo na sadaka ya maisha, daima wakijitahidi kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao ya kila siku. Upendo wa kweli anasema Baba Mtakatifu unamwilishwa katika huduma ya upendo. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Siku ya X ya Familia Duniani mjini Roma, kuanzia tarehe 22 hadi 25 Juni, 2022 imenogeshwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”. Huu ni wakati muafaka wa kuendelea kuimarisha upendo ndani ya familia; kwa kufanya maamuzi, huku familia nzima ikitembea kwa pamoja, ili kutangaza na kushuhudia furaha ya upendo ndani ya familia. Upendo wa kweli uwasaidie kugusa, kuganga na kuponya madonda ya ndani. Upendo ndani ya familia usaidie kuwatakatifuza wanandoa na kuwaimarisha katika sadaka na upendo wao. Baba Mtakatifu anawataka vijana wa kizazi kipya kupiga moyo konde, ili hatimaye, kuamua kufunga ndoa. Upendo wa familia, uwasaidie vijana kukua, kukomaa na kuanza kuwajibika katika maisha yao. Wanandoa watambue kwamba, Kanisa liko kati pamoja nao. Kanisa ni matunda ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Familia ziwe ni mahali pa ushirika, umoja, amani na furaha hata pale ambapo kuna mitikisiko na mipasuko ya maisha ya ndoa na familia. Wanandoa wawe ni mashuhuda na watangazaji wa Habari Njema kwamba, Mungu ni upendo na chemchemi ya ushirika wa maisha.

Jubilei ya Familia 2025

 

 

26 June 2022, 15:06