Papa:msukumo wa kueneza Injili haujawahi kushindwa katika Kanisa
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 16 Mei 2022, ametuma ujumbe wake kwa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa, (PMS), yaliyokusanyika pamoja kuanzia Jumatatu tarehe 16 Mei hadi tarehe 23 Mei, kwenye Kituo cha Valpré huko Lyon, nchini Ufaransa kwa ajili ya Mkutano Mkuu. Takriban wakurugenzi wa kitaifa 120 wa PMS na rais wake, Monsinyo Giampietro Dal Toso, wamechagua kukutana katika mji huo wa Ufaransa katika fursa inayoendana na kutangazwa mwenyeheri, Dominika ijayo, kwa Pauline Jaricot, ambaye kwa miaka 200 iliyopita alianzisha mojawapo ya kazi nne za kimisionari ile ya “Kueneza Imani”. Katika Ujumbe wa Papa anaandika kuwa: “Pauline Jaricot alipenda kusema kwamba Kanisa ni la kimisionari kwa asili na kwa hiyo kila mbatizwa ana utume; hakika ni utume. Kusaidia kuishi mwamko huu ni huduma ya kwanza ya Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa”.
Pauline alikuwa kijana alipoanza utume wa kimisionari wa Kanisa
Katika Ibada ya Misa Takatifu itaongozwa na Kardinali Luis Antonio Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu. Pauline alikuwa na umri wa miaka 23 alipoanzisha kusaidia shughuli ya umisionari wa Kanisa. Miaka michache baadaye alianzisha 'Rozari Hai', shirika linalojitoa kwa ajili ya sala na kushiriki matoleo ya sadaka. Kutoka katika familia tajiri, alikufa katika umaskini na kwa kutangazwa kuwa mwenyeheri, Papa amesisitiza kwamba Kanisa linathibitisha kuwa aliweza kukusanya hazina Mbinguni, hazina zinazotokana na ujasiri wa zawadi na kufichua siri ya maisha ambayo ni kwa kujitoa tu unaweza kumiliki, kwa kupoteza tu unaweza kupata tena".
Maadhimisho mbali mbali yanayohusiana na Baraza la Kipapa
Lakini hata hivyo mwaka huu, Papa Francisko anaongeza katika ujumbe wake, kuwa kuna maadhimisho ya miaka mia moja tangu kuanza Shughuli za Uenezaji wa Imani, pamoja na zile za Utoto Mtakatifu na mfuko wa Mtakatifu Petro Mtume, hadi kufikia Baraza la “Kipapa”. Na pia mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 150 tangu kuzaliwa kwa mwanzilishi wa Umoja wa Kimissionari wa Kipapa, Mwenyeheri Paolo Manna. Maadhimisho haya, anafafanuliwa Papa Francisko, kwamba ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 400 ya Baraza la Kipapa la ‘Propaganda Fide’, la wakati ule ambalo Matendo ya Kimisionari yana uhusiano wa karibu na ambayo yanashirikiana nayo katika kusaidia Makanisa katika maeneo yaliyokabidhiwa kwa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu lililoanzishwa kusaidia na kuratibu uenezaji wa Injili katika nchi zisizojulikana hadi wakati huo.
Uongofu wa kimisionari, sala na uthabiti wa mapendo
Papa ameweka wazi kwamba msukumo wa kueneza Injili haujawahi kushindwa katika Kanisa na daima unasalia kuwa nguvu yake msingi. Kwa sababu hiyo amefafanua jinsi alivyotaka, pamoja na Katiba ya Kitume Praedicate Evangelium juu ya mageuzi ya Curia Romana, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji lichukue jukumu la pekee la kuhamasisha uongofu wa kimisionari wa Kanisa, ambalo sio kugeuza imani, bali kushuhudia; kwa kutoka ndani mwake na kwenda nje kutangaza na maisha ya bure ya upendo wa Mungu mwokozi na kwa kuokoa wote walioitwa kuwa kaka na dada”. Katika ujumbe wake, wa Papa Fransisko amekazia mambo matatu ambayo, kwa shukrani ya utendaji wa Roho Mtakatifu, yamechangia sana katika kueneza Injili katika historia ya PMS. Mantiki tatu hizi ni uongofu wa kimisionari, sala na uthabiti wa mapendo. Kuhusiana na ya kwanza, amebainisha kwamba wema wa utume hutegemea safari ya mtu kujitoa mwenyewe, juu ya shauku ya kutojifikiria maisha juu yako mwenyewe, bali juu ya Yesu, aliyekuja kutumikia na si kutumikiwa.
Kuiga mfano wa Pauline Jaricot kupitia mateso aliyopitia
Mfano ni Pauline Jaricot ambaye alijaribu kujitambulisha na Bwana wake, pia kupitia mateso aliyopitia, kwa lengo la kuwasha moto wa upendo wake kwa kila mtu. Hapo ndipo penye chanzo cha utume yaani katika bidii ya imani isiyoridhika binafsi na ambayo, kwa njia ya uongofu, inaiga siku baada ya siku ili kuelekeza huruma ya Mungu kwenye barabara za ulimwengu. Kuhusu sala, Papa Fransisko amekazia kusema, ni mtindo wa kwanza wa utume na kwamba si kwa bahati kwamba Pauline alijiunga na Kazi ya Uenezaji wa Imani kwa njia ya Rozari Hai, kana kwamba anathibitisha kuwa utume huanza na sala na hawezi kufikiwa bila hiyo. Baba Mtakatifu amebainisha kuwa “Kwa sababu ni Roho wa Bwana anayetangulia na kuruhusu kazi zetu zote nzuri na ambazo ukuu daima ni neema yake.
Mchango wa watu wengi rahisi yalikuwa majaliwa kwa historia ya utume
Vinginevyo, utume hungeisha vibaya. Na baadaye kuna misaada ya nyenzo, uthabiti wa upendo. Pauline Jaricot alianzia kutokana na mtandao wa sala na wakati huo huo alitoa uhai kwa mkusanyiko wa matoleo kwa kiwango kikubwa na kwa mtindo wa ubunifu, akisindikizana na habari juu ya maisha na shughuli za wamisionari. Na michango ya watu wengi rahisi ilikuwa ya majaliwa kwa historia ya utume, Hatimaye, Papa Francisko amehitimisha ujumbe wake kwa kuwatakia PMS kutembea katika njia iliyanzishwa na Pauline Jaricot, mwanamke mkuu mmisionari, ili kuruhusu kuhamasishwa na imani yake thabiti, kwa ujasiri wake wa nguvu na kwa ukarimu wake bunifu.