Maadhimisho ya Siku ya Pili ya Udugu wa Kibinadamu tarehe 4 Februari 2022. Maadhimisho ya Siku ya Pili ya Udugu wa Kibinadamu tarehe 4 Februari 2022. 

Siku ya Pili Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu 4 Feb. 2022: Upendo!

Udugu wa kibinadamu maana yake ni kushikamana, kusaidiana, kuthaminiana na kuheshimiana hata katika tofauti msingi. Majadiliano ni muhimu katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Ni watu wenye tamaduni tofauti, lakini wote ni ndugu wamoja. Kwa kuheshimu tamaduni, mapokeo na mahali anapotoka mtu yasaidie mchakato wa ujenzi wa udugu na umoja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waraka wa Kitume wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ni kitovu cha Mamlaka Matakatifu ya Ufundishaji katika Kanisa, mintarafu masuala ya kijamii kadiri ya Baba Mtakatifu Francisko. Huu ni muhtasari wa mafundisho, hotuba na mawazo yake tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kunako mwaka 2013. Waraka huu wa kijamii unachota amana na utajiri mkubwa kutoka katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu uliotiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake kuhusu Mtakatifu Yosefu na Ushirika wa Watakatifu, Jumatano tarehe 2 Februari 2022 amewakumbusha watu wa Mungu kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Pili ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu.

Hii ni siku maalum inayowaunganisha waamini wa dini mbalimbali duniani, ili kuiadhimisha kwa pamoja na hivyo kukoleza mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Udugu wa kibinadamu unafumbatwa katika Injili ya upendo, unaowawezesha waamini wa dini mbalimbali: kuheshimiana, kuthaminiana, kusikilizana na hatimaye, kusaidiana bila kichongo moyoni. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, mchakato huu wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, utaweza kumwilishwa zaidi katika uhalisia wa maisha ya watu wa Mungu. Watu wenye mapenzi mema, wanahamasishwa kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu kwa kuondokana na vitendo vinavyosababisha kinzani, mipasuko na watu kujenga tabia ya kujifungia katika ubinafsi wao. Baba Mtakatifu anawachangamotisha waamini wa dini mbali mbali kujielekeza zaidi katika ujenzi wa amani ya kudumu kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu wamoja licha ya tofauti zao msingi.

Siku ya Pili ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu
Siku ya Pili ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu

Ni katika amana na utajiri unaobubujika kutoka katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa likatangaza kwamba tarehe 4 Februari ya kila mwaka itakuwa ni Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu. Hii ni changamoto kwa waamini wa dini mbalimbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili hatimaye kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Majadiliano ya kidini si alama ya udhaifu, bali ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Majadiliano ya kidini hayana mbadala, kwani waamini wa dini zote wanapaswa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha utamaduni wa ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu, ili hatimaye, familia kubwa ya binadamu iweze kukua na kukomaa katika mchakato wa upatanisho, kwa kuwakirimia watu matumaini yanayobubujika kutoka katika huduma ya upendo. Dini mbalimbali duniani zina uwezo wa kujenga utamaduni wa kuwakutanisha watu ili kuimarisha umoja na udugu wa kibinadamu. Hati hii ni kikolezo cha ujenzi wa misingi ya usawa, haki, amani na maridhiano duniani. Waamini wa dini mbalimbali wanapaswa kushikamana ili kulinda na kuendeleza mazingira nyumba ya wote; kudumisha haki msingi za binadamu; kwa kutoa majibu muafaka dhidi ya vita, kinzani na migogoro sehemu mbalimbali za dunia. Waamini na watu wenye mapenzi mema wakishirikiana kwa dhati wanaweza kukomesha pia vita, rushwa na ufisadi; kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema; kwa kubainisha na kutekeleza sera na mikakati ya uchumi fungamani pamoja na kuwakirimia watu wa Mungu matumaini katika hija ya maisha yao.

Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu inakazia pamoja na mambo mengine, ujenzi wa utamaduni wa majadiliano ya kidini; umuhimu wa waamini wa dini mbalimbali kufahamiana, ili kushirikiana na kushikamana, kwa kutambua na kuheshimu tofauti zao msingi. Udugu wa kibinadamu ni sehemu ya utu wa mwanadamu unaowasukuma watu wa Mataifa kusumbukiana katika maisha na kusimikwa katika matendo. Lengo ni kuondokana na vizingiti vinavyowatenganisha watu kwa misingi ya udini pamoja na vita vya kidini. Hii ni changamoto ya kushikamana ili kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu sehemu mbalimbali za dunia. Ikumbukwe kwamba, majadiliano ya kidini yanapata chimbuko lake katika majadiliano kati ya Mungu na waja wake. Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu itaendelea kupokelewa kwa mikono miwili na Jumuiya ya Kimataifa, ili kujenga jamii stahimilivu inayosimikwa katika misingi ya haki, amani, utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Udugu wa Kibinadamu unasimikwa katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni
Udugu wa Kibinadamu unasimikwa katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni

Hizi ni juhudi zilizotekelezwa kwa kushirikiana na Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu: Wajumbe wa Kamati hii ni pamoja na Kardinali Miguel Angel Ayuso Guixot, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, Professa Mohamed Hussein Mahrasawi, Mkuu wa Chuo cha Al Azhar na Monsinyo Yoannis Lahzi Gaidi, Aliyekuwa Katibu muhtasi wa Baba Mtakatifu Francisko. Wengine katika kamati hii ni Jaji Mohamed Mahmoud Abdel Salaam, mshauri mkuu wa Mufti mkuu. Wajumbe wengine ni wale walioteuliwa kutoka Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu, Baraza la Wazee wa Kiislam Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na watu maarufu katika tasnia ya habari Umoja wa Falme za Kiarabu.

Kwa upande wao, viongozi wa Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na Amiri Jeshi Msaidizi, watahakikisha kwamba, Hati ya Udugu wa Kibinadamu inatekelezwa kwa dhati kabisa na Kamati iliyoundwa, ili kumwilisha malengo yaliyobainishwa kwenye Hati hii. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linapenda kutumia fursa hii, kuitia shime Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu, mintarafu malengo yaliyobainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Hati hiyo. Umoja wa Mataifa unazihamasisha Nchi wanachama, Mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na Vyama vya kiraia kuhakikisha kwamba, vyote vinasaidia kunogesha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu.

Udugu wa Kibinadamu
03 February 2022, 16:56